Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Michezo

Arsenal moto uleule, United Hoi!

MABINGWA watetezi Ligi Kuu ya England (EPL), Arsenal ‘The Gunnners’ wameuwasha moto na kusimamisha bendera kwa msimu mpya wa 2026/27 baada ya kuwakaribisha Coventry kwa kichapo cha mabao 3-0.

Jumatatu, 24 Agosti 2026 · 06:00Dakika 1 kusomaToleo 179, uk. 37
Saka akipambana kumiliki mpira
Saka akipambana kumiliki mpira — Mtandao

Mtanange huo ulirindima Ijumaa, Agosti 21 katika Dimba la Emirates jijini London, ukiwa ni mchezo wa kwanza wa msimu, ambapo ulitazamwa na mashabiki 60,098 kati ya 60,704 wanaopaswa kuujaza uwanja huo.

Mabao ya Arsenal yaliwekwa kambani na Kai Havertz, Bukayo Saka na Martin Odegaard. Ni mchezo ambao washika mitutu hao waliutawala kwa kiwango kikubwa, wakiwa na umiliki wa kandanda wa asilimia 64, wakipiga mashuti 20 huku sita yakilenga lango, na usahihi wa pasi ukiwa asilimia 92.

Wakati Arsenal wakipepewa kwa ushindi, mahasimu wao Manchester United wameuanza msimu kwa kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Hull City, mchezo ulipigwa kwenye dimba la MKM, mjini Hull.

United walionyesha kiwango kibovu kwenye mchezo huo huku timu ikionyesha kukosa muunganiko katika maeneo matatu ya uwanja, eneo la ulinzi, kiungo na ushambuliaji, timu ilionekana kuwa wazi maeneo nyeti na kuwafanya wapinzani wao kutamba.

Ni kama mashabiki wa ‘Mashetani Wekundu’ walianza kujisahau kuwa bado timu yao haijakaa sawa, lakini mchezo mmoja umeanza kutonesha kidonda cha kukosa timu ya upinzani na zaidi ya miaka 14 hawajatwaa taji la EPL, licha ya kuwa mabingwa wa kihitoria sambamba na Liverpool ambapo timu zote zimetwaa mara 20.

Swali ni hili; je, ni kwa namna gani kocha wao, Michael Carrick atayatumia maingizo mapya ndani ya timu kufukia mashimo ambayo yameonekana mapema kuigharimu timu?

  • EPL
  • Arsenal
  • Manchester United

Soma Pia