Mtazamo
Dkt Nchimbi kumkuta ya Rais Aboud Jumbe
Aboud Jumbe, Rais wa Zanzibar alipata shinikizo la kujiuzulu, kama ilivyotokea kwa Dkt. Emmanuel Nchimbi. Jumbe aliamuriwa kuishi Mjimwema, Kigamboni huku uhuru wake ukiminywa. Je, haya yatamkuta Nchimbi?

MASWALI kwenye chumba cha habari cha Pambazuko yamekuwa mengi kutoka kwa wasomaji wake kuhusu alipo aliyekuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi.
Mbali na kutaka kujua alipo Dkt. Nchimbi, wasomaji wamekuwa wakitaka kujua hatma yake kwenye medani za siasa.
Gazeti hili linatambua kwamba hata baada ya kuandika barua ya kujiuzulu wadhifa aliokuwa akiushika hadi jana, Dkt. Nchimbi haikuwa tiketi ya kuacha kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya CCM.
Dkt. Nchimbi alihojiwa na kutajwa yaliyoelezwa kuwa makosa yake dhidi ya chama chake na uongozi wa juu.
Katika madai ya makosa hayo alionyeshwa pale alipokosea, huku akitakiwa kujitetea. Hata hivyo, alisema hana utetezi ingawa alieleza kwamba; “siamini kama haya yanayoelekezwa kwangu ni makosa.”
Uamuzi wa kumuondoa kwenye daftari la wanachama wa CCM, na kwa kuzingatia wadhifa wake, unamuweka Dkt. Nchimbi katika hatari ya kuzuiwa uhuru wake kama ilivyokuwa kwa aliyekuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Alhaj Aboud Jumbe.
Jumbe aliondolewa kwenye nafasi ya urais baada ya kuonekana kushabikia kuwepo kwa serikali tatu ndani ya Muungano, kinyume na imani ya chama chake.
Baada ya kuondoshwa, Alhaj Jumbe aliamuriwa kuishi Kigamboni, Dar es Salaam, huku uhuru wake ukiminywa hadi mauti kumkuta. Jumbe alifariki dunia Agosti 14, 2016 akiwa na umri wa miaka 96.
Jumbe aliamua kuachia ngazi Januari 29, 1984, akiwa mjini Dodoma wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC). Alikoma kuwa Rais wa Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, na Makamu Mwenyekiti wa CCM.
- jumbe
- nchimbi
- tanzania
- ikulu