Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

El-Nino yashtua serikali, mikakati yaanza kukabili

MIKAKATI ya kukabiliana na athari zinaoweza kujitokeza kutokana na mvua za El-Nino imeshika kasi, huku serikali ikisisitiza wakuu wa mikoa, taasisi za umma, binafsi na wananchi kuhakikisha wanaandaa mazingira ya kupunguza athari zinazotokana na mvua hizo.

Jumatatu, 31 Agosti 2026 · 06:00Dakika 4 kusomaToleo 180, uk. 14
Mashara ya mvua kubwa za El-Nino. Serikali imetoa tahadhari.
Mashara ya mvua kubwa za El-Nino. Serikali imetoa tahadhari. — Picha kutoka Maktaba ya Pambazuko

Hatua hizo zinakuja siku chache baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutoa tahadhari ya uwezekano wa kutokea kwa mvua za El Niño katika mikoa 14 nchini kuanzia mwishoni mwa Septemba hadi Desemba mwaka huu, zitakazotokana na mvua za vuli.

Tayari tahadhari nyingine imetolewa na Umoja wa Ulaya (EU) kuhusu hali ya mabadiliko ya tabianchi, ikieleza kuwa taarifa hiyo inaeleza kuwa bahari duniani zimefikia viwango vya juu zaidi vya joto kuwahi kurekodiwa, huku hali hiyo ikihusishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na shughuli za binadamu.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Agosti 22, Rais Samia Suluhu Hassan, aliwataka wakuu wa mikoa, wilaya na taasisi za serikali kujiandaa mapema kukabiliana na mvua kubwa zinazotabiriwa nchini, ili kuepusha maafa na madhara kwa wananchi.

“Niwaombe nendeni mkajitayarishe, mkaweke mazingira sawa ili mvua hizo zitakapoanza zisilete maafa makubwa kwa wananchi wetu,” alisema.

Alisema tahadhari ambazo TMA imeanza kutoa zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito na viongozi kuhakikisha mazingira yanaandaliwa ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.

“Kwa hiyo niwaombe sana, tahadhari zimeanza kutolewa, hatua zichukuliwe ili mvua hizi zisilete madhara kwa wananchi wetu,” alisema Rais Samia.

Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi mkoani Pwani mara baada ya kuzindua mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 2,115 wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JHPP).

Tahadhari hizo za serikali zikaendelea kupitia Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, kueleza bungeni Alhamisi Agosti 27, 2026 kuwa Serikali imejipanga kukabiliana na athari zinaoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo za El-Nino.

Dkt. Nchemba aliwahakikishia wabunge kuwa serikali imejipanga vyema kuhakikisha kwamba maeneo yatakayoathirika yanapatiwa misaada ya haraka.

“Bunge lilipitisha mabadiliko ya sheria kwenye sheria ya fedha yanayoelekeza fedha kwenda moja kwa moja kwenye mifuko ya barabara na mingine...”

“Nawapongeza Wizara ya Fedha na TRA kwa kuanza kuzipeleka fedha hizo ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 320 na kuiwezesha mifuko kukabiliana na mambo kama haya,” alisema.

Alielekeza Wakala wa Barababara Tanzania (Tanroads) na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) kupitia maeneo yote korofi yanayoweza kufanya mrundikano wa maji na kuleta mafuriko na kuhakikisha yanatengenezewa mifereji.

Alitoa rai kwa Watanzania wote kuwa na tahadhari na jambo hili ambalo limeshatolewa taarifa na kila Mtanzania kufanya tathmini ya pale anapoishi kwa kuangalia mazingira yao kwa kuwa wanajua historia ya mikondo ya katika maeneo wanayoishi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, amewataka wananchi kutunza sehemu ya chakula walichovuna mwaka huu, kwani mvua hizo za El Niño zinaqweza kuathiri mazao mashambani au kwenye maghala.

Silinde alitoa mwito huo Agosti 26, 2026, wakati wa kipindi cha maswali na majibu katika mkutano wa Nne wa Bunge la 13 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CCM Mkoa wa Iringa, Nancy Nyalusi, aliyetaka kujua Serikali itaanza lini kununua mahindi ya wakulima.

Silinde alisema Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, tayari ameelekeza mamlaka ya mazao mchanganyiko kuanza ununuzi wa mazao, huku Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ukitarajiwa kuongeza nguvu katika ununuzi haraka.

Akizungumzia tahadhari za hali ya hewa, Silinde alisema utabiri unaonyesha uwezekano wa mvua nyingi katika baadhi ya maeneo ya Afrika Mashariki kutokana na kuimarika kwa El-Niño.

Aliwataka wananchi kuepuka kuuza chakula chote baada ya mavuno, akisema tabia hiyo imekuwa ikiwafanya baadhi yao kukumbwa na upungufu wa chakula baadaye na kulazimika kutegemea msaada.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makala, amezielekeza kamati za usalama mkoa na wilaya za Karatu na Ngorongoro, pamoja na timu ya menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA), kuweka mikakati ya kukabiliana na mvua za El-Nino.

Katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano Makao makuu ya NCAA wilaya ya Karatu Agosti 26, 2026, Makala alizikumbusha kamati za maafa katika kila wilaya zikutane na kuweka mikakati ya kukabiliana na mvua hizo kama ambavyo Rais Samia ameelekeza.

Agosti 18, 2026 TMA ilitoa angalizo kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa mvua kubwa zinazohusishwa na hali ya hewa ya El Niño yenye nguvu kuanzia Septemba na hadi Desemba 2026, huku athari zake zikitarajiwa kuendelea hadi mwanzoni mwa mwaka 2027.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Ladislaus Chang'a, alisema El Niño yenye nguvu inaweza kusababisha vipindi vya mvua kubwa pamoja na kuanza mapema kwa mvua za msimu katika baadhi ya maeneo.

Chang'a alizitaka Idara na taasisi nchini, ikiwemo Mamlaka za Bandari, reli, usafiri wa anga pamoja na sekta ya afya, kuchukua tahadhari na kujiandaa mapema kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.

El-Nino inatarajiwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, ambapo wanasayansi wana wasiwasi kuhusu El-Nino ya mwaka huu kwa sababu mbili moja ikiwa ni ukubwa wake.

El-Nino iliyowahi kuwa mbaya zaidi ni ile ya mwaka 1998, na Umoja wa Mataifa umeonya, hali ambayo itaongeza joto katika sayari ambayo tayari inakabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi. Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) limesema El-Niño hii huenda ikatokea mwaka 2026, na kusababisha hali mbaya zaidi za hewa katika sehemu kubwa za dunia. Utabiri kadhaa kutoka mashirika ya kitaifa ya hali ya hewa unaonyesha huenda ikawa mojawapo ya El-Niño zenye nguvu zaidi kuwahi kurekodiwa — kinachoweza kuitwa 'super' El-Niño.”

  • El-Nino
  • TMA
  • Mabadiliko ya tabianchi
  • Maafa

Soma Pia