Tafakuri ya Bagonza
Haya yalikuwa makosa ya kimkakati, yamepokonya fursa!
TAIFA linahitaji maridhiano. Yawe ya kweli au ya hila, ni muhimu kutambua makosa matatu ya kimkakati yaliyotupokonya fursa na sifa nzuri ya taifa letu.

Haya ndiyo makosa ya kujutia iwe kwa uwazi au kwa siri.
Mosi, kumfunga Freeman Mbowe – aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema kwa miezi minane kulitoa mwanya kwa wanasiasa wenye misimamo mikali kukiteka chama.
Watu kama Tundu Lissu, Godbless Lema, Joseph Mbilinyi (Sugu), John Heche, Peter Msigwa, Ezekiel Wenje na wengine, walijiimarisha kwenye chama wakati Mbowe yuko gerezani.
CCM na serikali wakakosa mtu wa “kuridhiana” naye kwa sababu aliyekuwa akiwasaidia walimweka gerezani. Alipoachiwa, chama kiliishaenda mikononi mwa wenye msimamo mkali.
Mbowe aliwahi kuionya serikali lakini haikujali. Aliyeshauri Mbowe awekwe ndani, shetani anamuona.
Pili, kukataa maridhiano kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 lilikuwa kosa jingine ambapo wanasiasa wenye msimamo mkali ndani ya CCM walikataa maridhiano kabla ya uchaguzi.
Wangeweza kwenda mezani na “kuwatuliza”
wenye msimamo mkali kule Chadema na kuwaingiza kwenye uchaguzi, halafu goli la mkono lisingekomba kila kitu, bali lingeacha masalia ya wabunge na madiwani.
Kwa CCM kukataa maridhiano kukawafanya wenye msimamo mkali ndani ya Chadema kugomea uchaguzi. Kilichotokea Oktoba 29 kingeepukwa kama CCM ingekubali maridhiano. Kukataa maridhiano lilikuwa kosa kubwa la kimkakati.
Tatu, kumweka ndani Tundu Lissu lilikuwa kosa jingine la kimkakati ambapo wenye misimamo mikali ndani ya CCM na mfumo walishinikiza Lissu akamatwe na kufunguliwa kesi mbaya.
Hatua hii ikaiongeza vuguvugu ndani ya Chadema na pia hatua hii ikaigawa hata CCM, jumuia ya kimataifa, hata na taasisi nyeti zenye utakatifu fulani ndani na nje ya serikali.
Utekaji wa wana CCM na wapinzani, ukafunga uwezekano wa maridhiano. Kwa mara ya kwanza, hata viongozi wakuu “wakaonekana” kupoteza mwelekeo na kuwa wenye msimamo mkali. Badala ya maridhiano wakaanza kuimba “kujisalimisha tu!”
jifunga pingu mikononi na miguuni.
Chadema ina misimamo mikali. CCM ina misimamo mikali na jeuri. Mbowe alipokuwa madarakani alidhalilishwa na CCM mpaka Chadema ikamweka chini. Sasa dola inamwona Mbowe wa maana wakati ni yenyewe ilimwangusha?! Chadema sasa inamzodoa aliyekuwa mwamba wao. Mwe! Bora ukose akiba ya chakula, lakini uwe na akiba ya maneno.
Kama hayati Edward Lowassa, alichafuliwa na kusafishwa na vyama vyote CCM na Chadema. Alikufa akiwa mshindi kwa vyote.
Wazee wa Kikurya husema “Mdharau mwiba..”, lakini wajanja wa Kijaluo wao husema, “unaweza kudharau siafu, lakini usiwakalie kwa makalio yasiyo na kinga”.
Ni muda sasa wa kuwatoa watu magerezani, nasi tujitoe gerezani. Turudi mezani bila hila wala aibu.
Mwandishi wa safu hii ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe. Ni mchangiaji maalum wa safu na makala ndani ya Pambazuko.
Mpaka hapa tukubaliane. Tulimfunga Mbowe, wenye msimamo mkali wakachukua chama. Tumemfunga Lissu, chama chote kimekuwa na wakubwa wenye misimamo mikali. Kuwekana ndani siyo dawa nzuri ya kushughulikia upinzani.
Makosa haya matatu ya kimkakati yameifanya nchi ionekane imejiteka, imejifunga pingu na kupoteza funguo.
Fursa nyingi za kumaliza jambo hili kisiasa zimepotea. Mahakama zinateseka kulimaliza huku zimefungwa au ku-
- Maridhiano
- Siasa