Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari Kuu

Lissu ahofia uaminifu wa mashahidi

Kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu inaendelea leo Mahakama Kuu, Dar es Salaam, ambapo mbele ya majaji watatu amehoji uaminifu wa baadhi ya mashahidi wa Jamhuri.

Jumatano, 26 Agosti 2026 · 14:03Dakika 1 kusoma
Lissu akiaga wananchi waliofika mahakamani kwenye kesi inayomkabili
Lissu akiaga wananchi waliofika mahakamani kwenye kesi inayomkabili — Na Mapigapicha Wetu

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, leo Agosti 26, 2026 ameendelea kutoa utetezi wake katika kesi ya uhaini inayomkabili, huku akitilia shaka uaminifu wa mashahidi wa Jamhuri.

Katika utetezi huo, Lissu pia amepinga uzito wa ushahidi wa baadhi ya mashahidi wa upande wa Jamhuri.

Amesema baadhi ya mashahidi hao walikamatwa na polisi baada ya kutuhumiwa kupanga kufanya vurugu wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,2026.

Kwa mujibu wa maelezo yake, wote walikamatwa ndani ya siku nne; kati ya Aprili 4 na 8, 2026, na baadaye walikiri kupanga kufanya fujo.

Lissu amesema pamoja na kukiri kwao, mashahidi hao waliachiwa na baadaye wakawa mashahidi dhidi yake.

 Akahoji uaminifu wa ushahidi wa watu waliowahi kukiri kupanga kufanya uhalifu, lakini wakaachiwa bila kuchukuliwa hatua.

Akirejea ushahidi wa PW16, Amini Mahamba, Lissu amesema shahidi huyo alikiri kuwa alikuwa katika timu ya upelelezi iliyochunguza matukio ya Oktoba 29,2026.

Lissu alimhoji kama watu waliodaiwa kupanga kufanya fujo walichukuliwa hatua baada ya kukamatwa, ambapo Mahamba alijibu kuwa hakuna hatua iliyochukuliwa.

“Waheshimiwa majaji, ushahidi wa wahalifu wa aina hii una uzito gani kisheria?” Lissu amehoji, akisema ushahidi huo “haufai na hauamini kamwe.”

Mwanasiasa huyo amesema hali hiyo inapaswa kuifanya Mahakama kuhoji uzito wa ushahidi wao.

Aidha, Lissu ameomba Mahakama ipokee na kuangalia vielelezo D1, D15 na D16, akisema vinaweza kusaidia kuthibitisha hoja zake kuhusu maelezo yaliyotolewa na baadhi ya mashahidi.

Pia amemzungumzia PW1 George Bagyemu, akisema shahidi huyo alieleza kuwa aliona nia ya kutenda kosa la uhaini katika kauli alizodai Lissu alitoa.

Lissu amepinga tafsiri hiyo na kusisitiza kuwa ushahidi wa upande wa Jamhuri unapaswa kuchunguzwa.

Kesi hiyo inaendelea mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru.

  • lissu
  • mahakama
  • uhaini
  • chadema

Soma Pia