Vituko vya Wakubwa
‘Maajabu’ ya Rais Mobutu akiwa Ikulu
MOBUTU Sese Seko Kuku Ngwendu Wazambanga aliwahi kuwa Rais wa Zaire, ambayo sasa inaitwa Jamhuri ya Kidemokrasia na Congo – DRC.

Jina halisi alilopewa na wazazi wake ni Joseph Désiré Mobutu. Baadaye, kutokana na mbwembwe zake, alijiongezea majina mengine.
Alizaliwa Oktoba 14, 1930 katika Mji wa Lisala, wakati huo nchi hiyo ikiwa ni koloni la Ubelgiji, ikijulikana kwa jina la Zaire. Lugha yake kuu ni Lingala, ingawa katika baadhi ya maeneo, hasa mijini, Kifaransa kinazungumzwa zaidi.
Wakongo wengi wanamkumbuka Rais Mobutu kuwa ni kiongozi mwenye kiburi, tamaa, mpenda sifa, mlafi na mroho wa madaraka.
Alipochukua madaraka ya nchi alifanya chochote alichopenda na kuwataka raia wake wafanye alichopenda na kumfurahisha yeye.
Eneo hilo alilozaliwa lipo ndani ya Jimbo la Mongala na Mji wa Lisala ndio mji mkuu wa jimbo hilo na ulipewa hadhi ya kuwa mji mkuu kuenzi historia ya Mobutu ambaye alijenga kasiri la kifahari eneo ambalo kilizikwa kitovu chake na lilipo kaburi la baba yake mzazi.
Mobutu alipenda kwenda kwenye eneo hilo kupumzika na baadaye kujenga kasiri kubwa kule Gbadolite, eneo alikokulia na kulelewa na mama yake; eneo lile kwa sasa lipo ndani ya Jimbo la Nord Ubangi. Mama yake; “Mama Yemo” alizikwa huko na Mobutu aliamua kujenga uwanja mkubwa wa ndege na kuanzisha mbuga ya wanyama ambako sherehe zake zote za kifahari alizifanyia hapo.
Pia katika eneo la Lisala, ndipo Mobutu alipenda kufanya kazi zake na mara nyingi alitumia eneo hilo kutangaza uamuzi mgumu kuhusu nchi.
Moja ya uamuzi mgumu unaokumbukwa kufanywa pale ni kutoa hukumu ya kifo kwa Pierre Mulele kwa kukatwa katwa vipande.
Maisha na ndoa
Katika uhai wake Mobutu alipata watoto 21 ambao alieleza anawatambua, aliwahi kuoa mara mbili katika ndoa rasmi. Ndoa yake ya kwanza ni binti wa ujana wake, Marie-Antoinette, ambaye alifariki dunia kwa tatizo la moyo Oktoba 22, 1977 huko Genolier, Switzerland, akiwa na umri wa miaka 36 tu.
Baada ya hapo Mobutu alioa Mei 1, 1980, ambapo alifunga ndoa na Bobi Ladawa, mwanamke mrembo kutoka Bandundu.
Siku ya harusi yake, Papa John Paul II alikuwa na ziara ya kuitembelea Zaire (sasa DRC), Mobutu alimkaribisha Papa awe mgeni rasmi katika sherehe za harusi yake ingawa Papa alikataa.
Jambo lisilojulikana kwa watu ni kwamba siku hiyo Mobutu alioa wanawake wawili kwa siku moja, yaani mtu na pacha wake, Bobi Ladawa na Kosia Ladawa; na ndoa hiyo ilitambulika kama ndoa moja.
Watoto wengi wa Mobutu wapo Kinshasa mpaka sasa na wengine wanaishi Ulaya, kati ya watoto wake wawili wa kiume aliowapata katika ndoa yake ya kwanza walifariki Mobutu akiwa madarakani ambao ni Nyiwa aliyefariki Septemba 16, 1994 — anatajwa kufariki dunia kwa maradhi yanayotokana na Ukimwi, na Konga alifariki mwaka 1992.
Wengine wawili walifariki kwa kufuatana katika kipindi ambacho Mobutu akiwa amefariki dunia. Hao ni Kongulu aliyefariki Septemba 24, 1998 na Manda aliyefariki Novemba 27, 2004.
Watoto wake wengine ni Nzanga Mobutu Ngbangawe, ambaye ni mtoto mkubwa kwenye ndoa yake ya pili, kwa sasa ndiye amebaki kuwa msimamizi mkuu wa familia ya Mobutu.
Nzanga Mobutu aliwahi kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2006, hata hivyo hakushinda na baadaye alifanya kazi kwenye Serikali ya Joseph Kabila, akiwa waziri wa nchi anayeshugulikia kilimo.
Mtoto mwingine ni binti aitwaye Yakpwa (wakongo hupenda kumwita Yaki), huyu ameolewa huko Ubelgiji na mtu anayeitwa Pierre Janssen.
Yakpwa ni mwandishi wa vitabu na ameandika kitabu cha maisha ya Mobutu kinachoitwa “Mobutu’s lifestyle in vivid detail” ikimaanisha kwa tafsiri isiyo rasmi; “Maelezo ya kina kuhusu mtindo wa maisha ya Mobutu.”
Mbali kuwa wake zao watatu, pia Mobutu alibahatika kuwa na watoto kadhaa kupitia kwa wanawake wengine ambao hawakuwa wake zake. Kuna mwanamke mwingine alijulikana kwa jina maarufu la “Mama 41,”puko wake, alizaa naye watoto watatu ambao ni Senghor, Dongo na Nzanga.
Mwanamke mwingine ambaye alipata naye mtoto alijulikana kwa jina la Mbanguula, pia alizaa naye kijana mmoja ambaye hafahamiki sana. Aidha, huko Brazzaville alizaa mtoto na mwanamke asiyejulikana sana, mtoto aliitwa Robert.
Makala haya takayoendelea wiki ijayo imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali mtandaoni.
- Mobutu
- DRC
- Historia