Jicho la Tai
Mabasi yote yaendayo mikoani yaanzie Stendi ya Magufuli
Kwa tafsiri rahisi, basi lisimfuate abiria Sinza, Shekilango, Mabibo au sehemu nyingine iliyo karibu naye. Abiria ndiye afuate basi, hata kama safari ya kulifuata inahitaji safari nyingine yenye foleni, mizigo na gharama ya ziada.

Hapo ndipo Dar es Salaam inapogeuzwa darasa la mazoezi ya uvumilivu. Mama mwenye watoto wawili na mabegi matatu kutoka Mbeya ashushwe Mbezi, halafu aambiwe aende Kigamboni kwa daladala, mwendokasi au bajaji.
Mzee anayekwenda hospitali Tabata naye aanze kwanza ziara ya kutalii jiji. Inaonekana tiketi ya basi sasa itakuja na somo la lazima la kubeba mizigo kwa kichwa.
Chalamila anasema wanaopanda ndege huifuata uwanja wa ndege na wanaotumia SGR huenda stesheni; kwa hiyo na wa mabasi waende Kituo cha Magufuli.
Mfano huo unasikika vizuri jukwaani, lakini umejaa maswali mengi. Chalamila anatambua kabisa kuwa ndege haiwezi kutua Shekilango, wala treni kugeuza reli na kumfuata abiria Manzese.
Basi, tofauti na ndege na treni, linatumia barabara zilizopo na linaweza kupakia kwenye kituo kilichoidhinishwa bila kuvuruga safari.
Aidha, viwanja vya ndege na vituo vya reli hujengwa pamoja na mipango ya usafiri unganishi. Kama Magufuli inataka kuwa “uwanja wa ndege wa mabasi,”
basi ipewe kwanza teksi za bei nafuu, mwendokasi wa kutosha, nafasi ya mizigo, maegesho, usalama, vyoo na njia za haraka kwenda maeneo yote ya jiji.
Mimi kwa kuwa nimekuwa mtumishi wa serikali na sasa nimestaafu, nafahamu mantiki ya kuondoa vituo bubu, kudhibiti foleni, kukagua mabasi na kuhakikisha mapato ya serikali hayapotei.
Lakini Gavana Chalamila na wakubwa wenzake wa jiji wanapaswa kutambua kuwa dawa ya kupooza maumivu ya kichwa siyo kukata kichwa.
Taarifa za waendeshaji zinaonyesha kituo kina takribani nafasi 108 za maegesho, wakati mabasi yanaweza kuzidi 400 kwa siku na kufikia 800 msimu wa sikukuu.
Kuyakusanya yote hapo kunaweza kuhamisha msongamano kutoka katikati ya jiji na kuupeleka Mbezi, kisha tukatangaza tumeshinda foleni kwa kuihamisha tu anwani.
Tatizo jingine ni gharama iliyofichwa, inawezekana abiria akiongezewa nauli ya kufika Mbezi au kutoka huko, muda wa safari na malipo ya kubeba mizigo, bei hiyo haiandikwi kwenye tiketi, lakini inatoka mfukoni mwake.
Mfanyabiashara mdogo anayesafirisha bidhaa naye ataongeza gharama hiyo kwenye bei ya bidhaa.
Mwishowe, agizo linalodaiwa kuleta nidhamu linaweza kuwa kodi isiyoandikwa kwa maskini.
Serikali haipaswi kumrahisishia msimamizi kazi kwa kumtwisha mwananchi mzigo. Huo siyo utawala bora.
Sasa suluhisho siyo kuruhusu kila basi kusimama popote. Jiji liidhinishe vituo vichache vya kampuni vinavyokidhi masharti ya eneo, usalama, vyoo na maegesho.
Mabasi yaruhusiwe kushusha au kupakia kwa muda maalumu bila kuegesha barabarani, huku ukaguzi mkuu ukifanyika Stendi ya Magufuli. Ratiba, tiketi na vituo visimamiwe kidijitali ili wanaokiuka waadhibiwe. Uongozi mzuri haupimi mafanikio kwa kuona kituo kimejaa mabasi; hupima kama wananchi wamepunguziwa muda, gharama na mateso.
Chalamila aelewe kuwa abiria siyo makontena ya kukusanywa bandarini. Ni watu wenye watoto, mizigo, uzee, ulemavu, miadi na fedha kidogo.
Kwa hiyo, Chalamila – katika jambo hili, amepotoka siyo kwa kutaka utaratibu, bali kwa kudhani utaratibu lazima uume.
Gavana Chalamila anapaswa kuisikiliza Dar na watu wake kabla Dar haijamjibu kwa honi, foleni na mabegi yanayoburuzwa.
Huduma ya usafiri imejengwa kumfuata mwananchi kwa mipango, siyo kumshikisha adabu – kama kweli anastahili, kwa kumchosha.
- Usafiri
- Dar es Salaam