Habari
Musukuma: Ndejembi hajasaka cheo kwa kuumiza wenzake
Mbunge Musukuma amemsifia makamu wa rais mteule, Deogratius Ndejembi kuwa ni kiongozi mahiri ambaye anapanda vyeo bila "kuumiza wenzake."

MBUNGE wa Geita, Joseph Musukuma, amesema hajawahi kusikia wala kushuhudia Deogratius Ndejembi "akihangaika kuumiza wenzake," ili kupata cheo.
Musukuma amesema Ndejembi, mwanasiasa kijana wa miaka 43, ameonyesha kwamba vijana wanaweza kupata nafasi kubwa za uongozi bila kutumia uwezo wao kuwatendea wengine mabaya kwa sababu tu ya kushika vyeo vikubwa.
Akieleza kuhusu Ndejembi baada ya jina lake kuthibitishwa na Bunge ili kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Musukuma amesema uteuzi wa waziri huyo wa nishati - hadi jana, ni pendekezo la busara lililofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan akimtaka Ndejembi kujiamini katika kazi alizowahi kufanya na alizopangiwa.
“Mheshimiwa Rais amefanya pendekezo la busara kubwa sana, hii inaonyesha kwamba jiamini kwenye kazi ulizofanya na ulizopangiwa, cheo kikubwa kinachokufuata nyuma kitakufuata kwa bidii yako, siyo kwa kumpiga shoti mtu mwingine.
“Taifa hili tunakoelekea ni taifa la vijana, Gen Z sasa umepewa nafasi ya kufungua milango, tunahitaji kupata viongozi vijana wenye mawazo mapya, wanaotumika na wenye nidhamu,” amesema.
- ndejembi
- musukuma
- tanzania
- samia
- ikulu