Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari Kuu

Safari ya uhuru wa Lissu kuanza

Leo kesi yake kusikilizwa mfululizo, huku Jumuiya ya Madola ikishinikiza aachwe huru haraka ikiwa ni ukomo wa sharti lao.

Jumatatu, 10 Agosti 2026 · 03:00Dakika 2 kusomaToleo 177, uk. 6 & 7
Tundu Lissu
Tundu Lissu — Picha na BBC

Kuna dalili kwamba serikali inajipanga kuachana na mashitaka dhidi ya Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambaye anakabiliwa na kesi ya uhaini.

Akiwa korokoroni kwa siku 106 hadi sasa, kesi yake imepangwa kuanza kusikilizwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, masjala ndogo ya Dar es Salaam, kuanzia leo Agosti 10 hadi Septemba 7, 2026.

Taarifa ambazo zimefika kwa Pambazuko zinaeleza kuwa upo uwezekano mkubwa kwa kiongozi huyo wa upinzani kuwa huru, kwa serikali kueleza kwamba “haina nia ya kuendelea na kesi.”

Kumekuwepo na shinikizo kubwa kutoka kwa taasisi, mashirika na hata baadhi ya nchi kuhimiza kuachiwa kwa Lissu, ikielezwa kuwa mashitaka yake yamejikita kwenye masuala ya kisiasa kuliko uzito wa mashitaka yenyewe.

Hata hivyo, serikali mara zote imekuwa “ikijiweka pembeni” madai ya kushinikiza Lissu aendelee kushitakiwa kwa maelezo kwamba haiwezi kuingilia uhuru wa mahakama.

Pamoja na kuwa ni ratiba iliyopangwa tangu awali, usikilizwaji wa kesi hiyo wakati huu unaonekana kama hatua muhimu kwa serikali kujaribu kujinasua katika mtego uliowekwa na Kundi la Mawaziri wa Jumuiya ya Madola la Demokrasia na Haki za Binadamu (CMAG).

Mtego uliowekwa na CMAG ni kuwepo kwa masharti baada ya kumtuma mjumbe wake, Lazarus Chakwera, Rais mstaafu wa Malawi, kuja kufuatilia hatma ya vurugu za wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana; ni kuachiwa kwa kiongozi huyo wa upinzani ambaye yuko rumande kwa takribani mwaka mmoja sasa.

Kesi hiyo inaanza kusikilizwa katika siku ya mwisho iliyowekwa na kundi hilo la mawaziri wa CMAG, ambayo ni leo Agosti 10, kupitia uamuzi wa kikao chao cha 73 kilichofanyika Julai 10, 2026 kwa dharura.

Mawaziri hao walitoa tamko la kuhitimisha baada ya kujadili hali ya kisiasa na haki za binadamu hapa nchini Tanzania.

Kesi hiyo inatarajiwa kuvuta hisia na usikivu mkubwa wa umma nchini, huku jopo la mawakili wake likithibitisha kuwa limejipanga kikamilifu kuendelea na mapambano ya kisheria Mahakama Kuu.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa kwa siku 27 mfululizo na wengi wanadhani kuwa muda huo umepangwa mahsusi ili kuisogeza mbele kesi hiyo kwa haraka.

Katika ujumbe wake alioutoa kwa umma kupitia kwa mmoja wa mawakili wake, Paul Kisabo, waliomtembelea gerezani Ukonga, Dar es Salaam, Agosti 6, 2026, Lissu aliomba Watanzania wamuombee.

  • Tundu Lissu
  • Chadema
  • Mahakama Kuu
  • Jumuiya ya Madola

Soma Pia