Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Jicho la Tai

Serikali isijifunge, itakata pumzi

SERIKALI yetu siku hizi inafanana na mtu aliyefika sokoni akiwa na orodha ndefu, lakini mfukoni ana pochi nyembamba na kichwani hajui aanzie wapi.

Jumatatu, 17 Agosti 2026 · 05:15Dakika 2 kusomaToleo 178, uk. 5

Anataka kununua mchele, mafuta, dawa, sare za watoto na kulipa deni la jirani; mwisho wake anasimama katikati ya soko akihema, huku wauzaji wakimuuliza: “Mzee, unachukua nini?”

Hivyo ndivyo serikali ilivyo mbele ya msululu wa mambo makubwa yanayotaka uamuzi, siyo hotuba. Mezani kuna Katiba Mpya, tume mbalimbali, maridhiano ya kitaifa, majeraha ya kisiasa na ahadi ya kujenga Tanzania mpya.

Sahani imejaa mpaka punje zilizo juu zinaanza kuanguka, lakini mpishi bado anajadili kijiko gani kitumike.

Suala la Katiba Mpya limekaa sebuleni muda mrefu kiasi kwamba sasa linaweza kudai hati ya umiliki.

Kila mara linaambiwa: “Subiri, wageni wataondoka.”

Wageni hawaondoki; wanaongezeka. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2029 unasogea, na Uchaguzi Mkuu wa 2030 nao hauko mbali.

Tukitaka sheria, taasisi na taratibu mpya zitumike kwa ufanisi, mchakato lazima uanze mapema, kwa uwazi na ushirikishwaji wa kweli.

Katiba haiandikwi kwa pupa ya dakika za majeruhi. Siyo chapati ya kugeuzwa haraka jikoni kwa sababu wateja wameanza kugonga meza.

Mimi Mzee Tai naamini kuwa tunahitaji mjadala mpana, makubaliano, sheria zinazoeleweka, elimu kwa wananchi na muda wa taasisi kujiandaa. Serikali ikichelewa, itatuambia tena muda hautoshi; kana kwamba muda huo uliibwa na wasiojulikana.

Naona pia kuna tume inayoongozwa na Jaji Shabani Ally Lila, inayochunguza makosa ya jinai yanayohusishwa na matukio ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 na yaliyofuata. Tume hiyo inahitaji uhuru, ushirikiano, ushahidi na majibu yanayoaminika.

Wananchi hawahitaji ripoti nyingine nzuri ya kupamba kabati. Wanahitaji ukweli, uwajibikaji na hatua zinazoonekana.

Halafu kuna maridhiano—neno tamu sana masikioni, lakini gumu sana kwa baadhi ya wanasiasa. Wanapiga danadana. Maridhiano siyo viongozi kupiga picha, kutabasamu na kunywa chai huku walioumia wakibaki nje ya ukumbi.

Ni kukubali yaliyokwenda kombo, kusikiliza maumivu, kurejesha haki, kuondoa hofu na kujenga mazingira ambayo mpinzani wa kisiasa haonekani kama adui wa taifa.

Na uzee wangu huu ninaamini kuwa Katiba Mpya itajenga uwanja sawa wa siasa, matokeo ya tume yanaweza kurejesha imani, na maridhiano yanaweza kupunguza joto la taifa.

Mambo yote haya mazito kuwa mabegani mwa serikali, naihurumia sana na kuona kana kwamba imejikaba shingo kwa kuahidi mambo mengi bila kuyawekea mpangilio unaoonekana.

Yaani naiona kabisa serikali inapumua kwa shida, siyo kwa sababu kazi haziwezekani, bali kwa sababu uamuzi unasukumwa kwa mwendo wa kobe anayesubiri kibali cha kuvuka barabara.

Ni muda muafaka sasa kwa serikali kuweka ratiba ya wazi, kutaja nani anawajibika, kutoa taarifa kwa wananchi na kutekeleza uamuzi bila hila.

Tanzania mpya haitajengwa kwa mafumbo, wala kwa kuahirisha kesho inayofika kila asubuhi.

Serikali ivute pumzi, ifungue mshipi, ipange vipaumbele na ianze kazi.

Taifa haliwezi kuendelea kuhema milele likisubiri uamuzi wa kuamua lini litaamua.

  • Katiba Mpya
  • Maridhiano
  • Serikali

Soma Pia