Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Kona ya Dkt. Bisimba

Siku ya Ubinadamu Duniani ina maana halisi kwa watu?

KATIKA mlolongo wa siku zinazoazimishwa kidunia, ipo siku ya Kimataifa ya Ubinadamu (World Humanitarian Day), ambayo huadhimishwa Agosti 19 kila mwaka.

Jumatatu, 24 Agosti 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 179, uk. 11
Dkt. Bisimba
Dkt. Bisimba — Na Mpigapicha Wetu

Siku hii hutumika kuwakumbuka na kuwaheshimu watu wanaojitoa kuwasaidia wengine walio katika mazingira magumu, wakati mwingi wakihatarisha maisha yao wenyewe.

Katika siku hii, watu wote wanaalikwa kutafakari iwapo bado tunauona ubinadamu wa mwingine. Unamuangaliaje mtu mwingine katika mazingira yoyote yale aliyonayo?

Siku hii ilianzishwa ikihusishwa na tukio la kusikitisha sana lililotokea Baghdad, Iraq mnamo Agosti 19, 2003.

Katika siku hii lilitokea shambulio la bomu katika makao ya Umoja wa Mataifa na waliuawa watu 22 waliokuwa wakifanya kazi za kibinadamu kwa kuwasaidia waathirika wa vita.

Kati ya waliouawa ni Sergio Vieira de Mello, aliyekuwa mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq.

Hii ni siku muhimu iliyowekwa kukumbuka madhila hayo ya maisha yaliyopotea kwa ajili ya kuwahudumia wengine.

Ni siku ya kutambua ujasiri wa maelfu ya watu duniani wanaofanya kazi za kibinadamu wakati wa vita, majanga, njaa, magonjwa na misiba mbalimbali.

Tunapoitazama siku hii kwa jicho pana zaidi tunaona kwamba ubinadamu siyo jukumu la mashirika ya misaada pekee.

Ubinadamu unaanza pale tunapoweza kumuona binadamu mwingine kama mwanadamu mwenye utu, heshima na haki kama sisi wenyewe.

Mtu anapokumbwa na janga, mtoto kuteseka, mtu mwenye ulemavu kukosewa fursa, familia inapopoteza makazi au tunapoona mtu ananyanyaswa kwa sababu yoyote ile, swali kwetu tunaoona siyo tu kwamba ‘nani anapaswa kumsaidia, bali tujihoji kama jamii tunafanya nini?

Nimekumbuka kisa kilichotokea kwenye eneo la mahakama moja Dar es Salaam, ambapo askari walikuwa wanamshambulia raia mmoja kwa mateke na virungu na wapo watu wengi wamezunguka hapo wakiangalia.

Baadaye akatokea mwanadada mmoja, akaamua kumvuta yule aliyekuwa anapigwa bila kujifikiria kuwa naye yangeweza kumkuta kama ya huyo aliyekuwa anashambuliwa.

Huo ndiyo mfano mdogo wa ubinadamu.

Ubinadamu unahitaji huruma, lakini huruma pekee haitoshi, unahitaji zaidi ni kuheshimu haki na utu wa mwingine katika sehemu yoyote ulipo kama binadamu, uwe kiongozi, uwe mtendaji katika dola au hata mhudumu katika taasisi.

Usidhani kuwa ni lazima msaada mkubwa ni kumpatia mtu fedha, au chakula, bali ukiweza kumsikiliza, kumlinda mtu dhidi ya manyanyaso, kumtetea anaponyimwa haki yake au hata kumpa nafasi ya kusimama kwa miguu yake mwenyewe.

Tunapoitazama dunia iliyojaa migogoro, chuki na tofauti zinazotugawa kama binadamu, siku hii ya kimataifa ya ubinadamu inatukumbusha jambo moja muhimu, maumivu ya mwanadamu mwenzako hayapaswi kuwa jambo lisilokuhusu.

Hata nasi Watanzania kwa hali tuliyonayo nchini kipindi hiki tunahitaji kujihoji tunawachukuliaje watu walio katika dhiki mbalimbali ikiwa ni pamoja na kudhulumiwa, kupotelewa na ndugu kwa njia zisizoeleweka.

Je, tunawapa usaidizi wowote hata kama ni wakuwafariji tu? Tumewahi kusimama dhidi ya dhulma na kuonewa kwa mwingine?

Ujumbe mkubwa wa siku hii si kuwasaidia wengine pekee ni kukumbusha kuwa na ubinadamu kwa binadamu wenzetu.

Tunaposhindwa kuuona ubinadamu wa mwingine tunakuwa katika hatari ya kupoteza sehemu ya ubinadamu wetu wenyewe.

Mwandishi wa safu hii ya kila wiki, ni mwanaharakati wa demokrasia, haki za binadamu na mwanazuoni wa falsafa ya sheria. Anapatikana kwa namba .

  • Haki za binadamu

Soma Pia