Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Makala

TPA iwe kioo cha ufanisi kwa mashirika ya umma

UWEKEZAJI na maboresho yanayoendelea katika Bandari ya Dar es Salaam na bandari nyingine nchini tayari “mavuno” yake yameanza kuonekana.

Jumatatu, 10 Agosti 2026 · 09:15Dakika 2 kusomaToleo 177, uk. 16 & 17

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) – kwa miaka mitatu mfululizo, imekuwa kinara miongoni mwa taasisi za umma kwa kutoa gawio kubwa serikalini, ikiwa ni ushahidi kwamba uongozi wenye dira, uwekezaji sahihi, weledi na uwajibikaji vinaweza kubadilisha taasisi ya umma.

Mwaka 2026, TPA imetoa gawio la Shilingi bilioni 205.5, kutoka 181.54/- mwaka 2025 na 153.917/- mwaka 2024.

Kwa wastani, gawio limekuwa likiongezeka kwa takribani Shilingi bilioni 26 kila mwaka.

Mwenendo huu unaonyesha kuwa TPA haitimizi tu malengo yake ya mapato, bali pia huanzia pale ilipoishia mwaka uliotangulia na kuweka viwango vipya vya utendaji.

Mafanikio hayo yamechangiwa na uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na ushirikiano na sekta binafsi kupitia DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited.

Maboresho ya miundombinu, usimamizi na huduma yameongeza uwezo wa bandari kuhudumia meli kubwa na mizigo mingi kwa ufanisi zaidi.

Yapo maboresho mengi yaliyofanywa na yanaendelea ikiwamo kuongezwa kwa kina cha magati kadhaa katika Bandari ya Dar es Salaam na bandari zingine ili kuruhusu meli kubwa zaidi kutia nanga.

Katika kipindi cha miaka minne, TPA imeweza kuongeza shehena zinazopokelewa na kusafirishwa nje ya Tanzania kutoka tani milioni 23 mwaka 2023/2024 hadi tani milioni 27 mwaka 2024/2025.

Wakati huohuo, muda wa kuhudumia meli umepungua kutoka siku saba hadi siku tatu. Haya siyo mafanikio kwenye karatasi, ni mabadiliko yanayohisiwa na wafanyabiashara na wasafirishaji, huku malalamiko kuhusu ucheleweshaji yakipungua kwa kiasi kikubwa.

Kuimarika kwa huduma kumevutia zaidi wateja wa ndani na kutoka nchi jirani, zikiwamo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia, Burundi, Rwanda na Zimbabwe. Hivyo, Bandari ya Dar es Salaam inazidi kuimarisha nafasi yake kuwa lango muhimu la biashara na uchumi wa Afrika.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, amehusisha mafanikio hayo na uwekezaji, miundombinu bora, weledi na kuachana na utendaji wa mazoea.

Kauli hiyo ya mtendaji mkuu wa mamlaka hiyo, inabeba somo muhimu; taasisi ya umma haiwezi kupata matokeo mapya ikiwa itaendelea kufanya kazi kwa mtindo wa zamani.

Gawio la TPA ni zaidi ya takwimu kwenye karatasi, kwani fedha hizo zinaisaidia serikali kujenga barabara, hospitali, vituo vya afya na zahanati, kununua dawa na vifaa tiba, kuboresha huduma za jamii na kupunguza utegemezi wa mikopo ya nje. Kwa hiyo, ufanisi wa TPA una manufaa ya moja kwa moja kwa Watanzania.

Kutokana na mafanikio hayo, mashirika mengine ya umma yanapaswa kuiangalia TPA kama kioo cha kujipima.

Yanahitaji viongozi wanaoelewa dhamana zao, bodi zenye uwezo, watumishi wenye nidhamu, uwekezaji wenye tija, ubunifu, uwazi na malengo yanayopimika. Serikali nayo iendelee kuyawekea mazingira bora na kuyawajibisha.

TPA imeonyesha kuwa shirika la umma linaweza kujiendesha kwa ufanisi, kushindana, kuongeza mapato na kutoa gawio kubwa.

Mfano huu ukiigwa, Tanzania itaimarisha uchumi wake, kupanua huduma kwa wananchi na kupunguza utegemezi wa fedha kutoka nje.

Na mashirika mengi yakifikia viwango vya TPA na hata kuipiku, hapo ndipo mashirika ya umma yatakapokuwa injini halisi za maendeleo ya Tanzania na watu wake.

  • TPA
  • Bandari
  • Mashirika ya umma

Soma Pia