Tahariri
Tulinde tunu za Tanzania kwa wivu mkubwa
Uongozi unaosikiliza, unaojali na unaowajibika ndio msingi wa kurejesha imani ya wananchi.
Viongozi wanapaswa kutekeleza wajibu wa dhamana waliyopewa. Wafanye kazi kwa bidii na uadilifu, watende haki bila upendeleo, na wajiepushe na vitendo vya ubadhirifu, matumizi mabaya ya madaraka na mienendo mingine isiyofaa.
Wananchi wanapoona wazi kwamba kuna maeneo ambapo uongozi na utumishi wa umma umegeuka kuwa eneo la kuchuma isivyokuwa halali, au hata kuwa fimbo ya kuwachapa, imani yao hupungua na mshikamano wa kitaifa kudhoofika.
Viongozi wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa. Wanapaswa kuonyesha kwa vitendo kwamba madaraka ni kwa ajili ya kuhudumia, siyo kutawala kwa nguvu. Uongozi unaosikiliza, unaojali na unaowajibika ndio msingi wa kurejesha imani ya wananchi na kuimarisha umoja wa kitaifa.
Katika kutekeleza wajibu wao, wananchi wanapaswa kuendelea kuheshimu sheria, kufanya kazi kwa bidii, kutumia maarifa kujiletea maendeleo, na kuchangia kwa dhati katika ustawi wa taifa.
Uzalendo wa kweli hauishii kwenye maneno; unaonekana katika vitendo: kulinda mali za umma, kulipa kodi kwa uaminifu, kuheshimu haki za wengine, na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii.
Tanzania ni yetu sote, na hatuna nchi ya ziada ya kukimbilia endapo tutaivuruga sisi wenyewe, kwa njia zozote zile.
- Tahariri
- Uongozi
- Uwajibikaji