Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Kodi

Tutakwama kujenga uchumi wa kidijiti

Sheria ya Fedha ya 2026 inaanzisha ushuru kwa huduma za kidijitali za kigeni, lakini bila mfumo wa kujisajili wala kanuni za utekelezaji.

Jumatatu, 10 Agosti 2026 · 06:30Dakika 2 kusomaToleo 177, uk. 9 & 14
Uchumi wa Kidigitali
Uchumi wa Kidigitali — Picha na Maktaba

Sheria ya Fedha ya 2026 imefanya mabadiliko kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa kwa Huduma za Kidijitali (sura 147). Chini ya mabadiliko hayo yaliyo katika kifungu cha 8, Kifungu cha 126 cha Sheria ya Ushuru wa Bidhaa kimerekebishwa ili kuanzisha utaratibu wa kutoza ushuru wa bidhaa kwenye huduma za kidijitali zinazotolewa na kampuni za kigeni kwa wateja walio nchini Tanzania kupitia mtandao wa intaneti au njia nyingine za kielektroniki.

Chini ya mabadiliko hayo ya sheria, watoaji wa huduma hizi wanatakiwa kujisajili, kuwasilisha ritani za kodi na kulipa ushuru.

Pili, mabadiliko yamefanyika katika Sheria ya VAT kwa Masoko ya Kidijitali (sura 148), ambapo kifungu cha 94 kinamfanya mwendeshaji wa soko la kidijitali kutambulika kama mtoa huduma rasmi kwa madhumuni ya VAT. Hii inajumuisha majukwaa kama vile tovuti, programu za simu, na milango ya intaneti.

Tatu, kuna mabadiliko ya Sheria ya Urasimishaji wa Malipo ya Kielektroniki (sura 185). Mabadiliko katika kifungu cha 6 sasa yanampa waziri husika mamlaka ya kuagiza malipo fulani kufanyika kwa njia ya kielektroniki, ikijumuisha sharti la kuwa na uthibitisho wa malipo ya kielektroniki wakati wa kuhamisha umiliki wa ardhi, majengo na vyombo vya moto.

Mabadiliko hayo yamelenga kampuni zinazotoa huduma za software kama vile Amazon Web Services, Microsoft Azure, Google Cloud, Microsoft 365, Adobe Creative Cloud, Zoom na Salesforce; maduka ya programu za simu kama Apple App Store na Google Play Store; matangazo ya mtandaoni yanayotolewa na Google Ads, Meta na LinkedIn Ads; pamoja na kampuni zinazotoa huduma za akili unde.

Kasoro nyingine ni kwamba Sheria ya Fedha ya 2026 inaunda mfumo wa kujitathmini mwenyewe bila kuweka taratibu au miundombinu ya kiutendaji iliyokamilika.

Pia, sheria inatamka kuwa usajili, uwasilishaji wa ritani, na ulipaji wa ushuru utafanyika “kulingana na kanuni zitakazotungwa na waziri.” Lakini mwezi mmoja baada ya sheria hiyo kuanza kutumika, bado haijatangazwa kama kanuni hizo zimetungwa.

Aidha, sheria yenyewe haianzishi mfumo au tovuti rasmi ya mtandaoni itakayotumiwa na kampuni za kigeni kujisajili, njia za malipo ya fedha za kigeni au sarafu zitakazotumika kulipia ushuru huo, pamoja na fomu na tarehe za mwisho za kuwasilisha ritani hizo.

Kwa upande mwingine, sheria hiyo haijatoa mamlaka au maelekezo ya kiutendaji kwa TRA kuhusu namna ya kuwachukulia hatua watoa huduma wa kigeni watakaokaidi sheria hiyo.

Umoja wa Ulaya ulipoanzisha sheria za VAT kwa huduma za kielektroniki, uliunda mfumo ujulikanao kama Mini One Stop Shop (MOSS) na baadaye One Stop Shop (OSS), ambao unarahisisha ukusanyaji wa kodi hiyo. Mfumo huu uliruhusu kampuni zisizo na makazi katika umoja huo kujisajili katika nchi moja mwanachama na kuwasilisha VAT kwa njia rahisi ya mtandaoni kabla ya sheria kuanza kubana kikamilifu.

  • Sheria ya Fedha
  • TRA
  • Kodi ya kidijitali
  • VAT

Soma Pia