Kona ya Dkt. Bisimba
Vijana ni nguvu ya mabadiliko leo
AGOSTI 12 ya kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Vijana.
Hii siyo siku ya kufanya sherehe, ni nafasi ya vijana kutafakari kuhusu nafasi yao ndani ya jamii, changamoto zinazowasonga na hata wajibu wao katika kujenga jamii wanayoitaka.
Siku hii haikutokea tu, bali ni vijana wenyewe waliliinua wazo hili mwaka 1991 walipokutana Vienna, Austria katika kikao cha kwanza cha Jukwaa la Vijana Ulimwenguni, chini ya Mfumo wa Umoja wa Mataifa.
Baada ya vijana kupendekeza uwepo wa siku yao kimataifa mwaka 1998, kongamano la mawaziri wanaohusika na vijana lililofanyika Lisbon, Ureno, walitoa pendekezo la kuwa na siku ya vijana kila Agosti 12.
Hatimaye Desemba 17, 1999, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio 54/120 kuidhinisha rasmi pendekezo hilo la mawaziri na siku hiyo ilianza rasmi 12/8/2000.
Ukitazama chimbuko hili la siku ya vijana ni ujumbe mzito kabisa kwa vijana kuwa siku hii haikutoka kwa serikali au viongozi bali lilitoka kwa vijana wenyewe na likafikia kutekelezwa.
Hii siku haipaswi kuwa siku ya watu wazima kuwaambia vijana wanachopaswa kufanya.
Hii ni siku ya vijana kuitambua sauti yao, uwezo walionao na nafasi yao katika kufanya maamuzi na hasa katika kufikia mabadiliko chanya katika jamii.
Siku hii inatukumbusha kwamba vijana ni wadau muhimu katika kujenga jamii na kwamba sauti waliyo nayo, mawazo yao na ushiriki wao katika kufanya maamuzi ni muhimu sana katika jamii zetu.
Mara nyingi tumewasikia viongozi wakisema ‘vijana ni taifa la kesho’. Ukweli ni kuwa hiyo kesho huwa haifiki.
Vijana hawapaswi kusubiri kesho kwani wao wanaishi leo wakiwa na nguvu na ufahamu. Vijana hawapaswi kabisa kuwa watazamaji wa maendeleo.
Wao ni sehemu muhimu ya nguvu kazi, ubunifu, mabadiliko ya kiteknolojia, utamaduni na hata harakati za kutetea haki na uhuru wa binadamu.
Historia iko wazi kuhusu mabadiliko makubwa katika jamii yalivyohusisha vijana. Vijana wamekuwa mstari wa mbele katika kupigania uhuru, usawa, haki za binadamu na demokrasia. Hii ni kweli hata hapa nchini Tanzania.
Pamoja na kuwa vijana wa sasa wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa ajira, fursa ndogo za kiuchumi, gharama za elimu, ukosefu wa ujuzi, kukosa nafasi za kutosha katika kufanya maamuzi, bado vijana wanapaswa kuinua sauti zao na kutafuta njia mbadala zakushikilia nafasi zao.
Vijana wawe wa kwanza kuisaidia jamii kubadili mtazamo ya kuwa vijana hawataweza kwa kukosa uzoefu.
Uzoefu wa wazee ni hazina, lakini nguvu, ubunifu na mawazo ya vijana ni mtaji wa taifa.
Pawepo na kuzungumza na kusikilizana kati ya vijana na wazee, pasiwepo na hali ya kizazi kimoja kukiona kingine kuwa mpinzani.
Vijana wanapoadhimisha siku yao watambue wana wajibu katika jamii wanapaswa kudaka fursa zitakazojitokeza na hata kuibua fursa na kuzitumia kujielimisha, kujenga ujuzi na kuitumia teknolojia kwa manufaa na zaidi kushiriki katika masuala ya jamii.
Vijana wana nafasi adhimu kulinda demokrasia, utawala wa sheria na haki za binadamu. Vijana waweze kuhoji kwa kushiriki katika mijadala ya kitaifa, kudai uwajibikaji, wainue sauti zenye hoja, maarifa na matumaini.
Vijana msisubiri kuwa viongozi wa kesho.
Ninyi ni nguvu ya mabadiliko leo. Mshiriki kuijenga Tanzania muitakayo leo.
Mwandishi wa safu hii ya kila wiki, ni mwanaharakati wa demokrasia, haki za binadamu na mwanazuoni wa falsafa ya sheria. Anapatikana kwa namba.
- Vijana
- Siku ya Vijana
- Demokrasia