Tabianchi
WFP yaonya madhara makubwa El Niño
ENEO la Afrika Mashariki, limetakiwa kujiandaa kwa madhara makubwa yatakayotokana na hali ya hewa ya El Nino inayotarajiwa kuikumba dunia baadaye mwaka huu.
Shirika la Chakula Duniani (WFP), katika ripoti yake ya hivi karibuni imeonya kuwa takribani watu milioni 49 duniani kote wapo katika hatari ya kukabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula kutokana na El Nino.
WFP inasema hali hiyo inatarajiwa kutokea hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika yametajwa kama maeneo ambayo nayo yataathirika zaidi na hali hiyo.
Zaidi ya watu milioni 18 katika maeneo hayo mawili wanatarajiwa kukabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 ikilinganishwa na viwango vya sasa.
Lakini kwa nchi za Afrika Mashariki athari zinaenda mbali zaidi ya suala la upungufu wa chakula na kutikisa uchumi wa nchi hizo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, hali hiyo ya El Nino itaathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji katika sekta ya kilimo.
Wachumi wanaonya kuwa kilimo ni moja ya sekta ambazo zinaajiri watu wengi katika eneo hilo, hivyo kuna uwezekano wa mapato ya watu binafsi na yale ya serikali kuyumba kwa kiasi kikubwa na hivyo kuathiri uchumi.
Nchi nyingi katika eneo hilo hutegemea pia kuongeza mapato yake ya mauzo ya nje kutokana na kilimo inaelezwa kuwa athari za El Nino zinaweza kusababisha kushuka kwa mapato hayo na hivyo kuathiri uwezo wa serikali hizo kuwahudumia wananchi wake.
Inaelezwa pia kuwa viwanda vya kusindika mazao, ambavyo kwa kiasi kikubwa vinategemea malighafi kutoka kwenye kilimo, navyo vitaathirika kwa kukosa malighafi za kutosha.
Hivyo, WFP inaonya kuwa changamoto za tabianchi zinaweza kuwa hatari kubwa ya kiuchumi zinazoweza kupunguza kasi ya ukuaji, kuongeza mfumuko wa bei na kuweka shinikizo kwenye bajeti za serikali.
El Niño inatarajiwa kufikia kilele chake kati ya Septemba na Desemba mwaka huu, lakini athari zake kiuchumi zinaweza kuendelea hadi mwaka 2027 kutokana na kuvurugika kwa misimu ya mvua na kilimo.
Tofauti na ukame au mafuriko ya kawaida, El Niño inaweza kusababisha mifumo tofauti kabisa ya hali ya hewa katika maeneo yanayokaribiana.
Baadhi ya maeneo yanaweza kupata mvua nyingi zinazosababisha uharibifu wa mazao, barabara na miundombinu ya kuhifadhi chakula, huku maeneo mengine yakikumbwa na vipindi virefu vya ukame vinavyopunguza uzalishaji wa kilimo na tija ya mifugo.
Athari hasi
WFP inabainisha kuwa kupungua kwa uzalishaji wa mazao bila shaka kutapunguza upatikanaji wa chakula, kuongeza shinikizo la kupanda kwa bei na kuongeza gharama za maisha wakati serikali zikijitahidi kudhibiti mfumuko wa bei ndani ya viwango vinavyolengwa.
Wakati Benki Kuu zinaweza kukabiliwa na shinikizo la kuongeza ukali wa hali ya kifedha, lakini uwezo wa wananchi kununua unaweza kupungua, huku bidhaa zitokanazo na kilimo sokoni zikipanda bei kutokana na ongezeko la gharama za uzalishaji.
- El Nino
- Chakula
- Tabianchi
- WFP