Kuhusu Pambazuko
Pambazuko ni neno la Kiswahili ambalo tafsiri yake nyingine ni mawio; kuanza kwa jambo/siku, na pengine, awali.


Hili ni jina la gazeti la watu wa kada zote; gazeti la ubunifu la kila wiki, linaloandikwa kwa lugha ya Kiswahili, ambalo linaunganisha kwa upana zaidi wazungumzaji wa lugha hiyo adhimu wanaofika milioni 300 duniani kote.
Pambazuko ni gazeti linalosambazwa kupitia WhatsApp na pia kwa njia zingine za kimtandao; Signal, na email.
Ni gazeti linalotolewa bure, kwa kila mtu anayejua kusoma Kiswahili na hata wale wanaojifunza lugha hiyo.
Ni gazeti linaloleta mbinu mpya katika kukuza ubora wa uandishi wa habari katika Afrika na duniani, ambapo lugha ya Kiswahili inatumika au kufundishwa.
Watendaji wa Pambazuko wanaamini kwamba vyombo vya habari, hasa vya kidijitali, vinaweza kuwa daraja na kubeba jukumu kubwa la kuunganisha – kwa mizania sawa, serikali na wananchi katika utawala wa kidemokrasia na ugatuzi wa kutenda haki.
Msukumo mkubwa wa kuanzishwa kwa Pambazuko na kuwa na uamuzi wa kusambaza bure gazeti hilo, ulitokana na matamanio ya mwanzilishi na mhariri mkuu wa Pambazuko, Simon Mkina, kuhakikisha haki ya kupata habari kwa kila mtu, inakuwa bure au kupatikana kwa gharama nafuu zaidi.
Kwa miaka kadhaa, uwezo wa watu kununua gazeti umekuwa tu kwa watu wenye uwezo, hivyo watu wasiokuwa na kipato cha uhakika, kunyimwa haki hiyo ya msingi, na badala yake kuegamia habari za vijiweni, ambazo nyingi hazina ukweli na kukosa usahihi.
Simon Mkina akaamini kuwa njia rahisi na yenye gharama nafuu ya kusambaza habari za kweli, uhakika na sahihi kwa watu wote, ni kwa njia ya mtandao, ndiyo maana Julai 10, 2022, gazeti la kwanza la Pambazuko lilichapishwa, kutoka kwenye mfumo wa kusambazwa kupitia Facebook, ulioanza mwaka 2021.
Kwa kauli mbiu ya Pamabzuko; “Ukweli Hauna Kutu”- gazeti hili halitasita kuandika habari yoyote, yenye maslahi kwa wananchi, bila kujali ilipaswa kuwafikia lini wananchi. Kwa Pambazuko, hakuna habari iliyochacha.
Pambazuko ni chapisho la Afrika Mashariki lenye mtazamo wa kimataifa.
Malengo yetu makuu ni kuwezesha waandishi kuandika bila kubanwa wala kuminywa na wamiliki ama wahariri wa vyombo vya habari; kuwezesha wananchi kupitia ukuu wa vyombo vya habari vya kisasa, kuelewa haki zao; na zaidi sana, kuchangia maendeleo ya nchi zao.
Pambazuko linaamini kwamba jumuia yenye ujuzi na haki – kupitia vyombo vya habari, ni bora zaidi katika kuelewa na kulinda rasilimali na mazingira yao.
Pambazuko pia linajikita kujenga daraja linalounganisha wasomi, watunga sera, watendaji na wananchi, bila kujali viwango vya elimu, vipato, mahali wanapoishi na hata imani zao za dini na itikadi za siasa.
Matumaini ya Pambazuko ni kwamba gazeti litaendelea kuhimiza wananchi kujihusisha katika masuala ya kudai haki, kupigania maendeleo – kwa kufanya kazi kwa bidii, na kuzitaka serikali kuhakikisha zinawatumikia vyema wananchi.