Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

CCM: Tunaomba Mungu Polepole apatikane hai

Chama tawala, CCM kimeeleza kusikitishwa na tukio la kupotea kwa aliyekuwa kada wake, Humprey Polepole. kikieleza kuwa "kinaomba Mungu apatikane haraka."

Jumatatu, 7 Septemba 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 181, uk. 13
Polepole
Polepole — Picha kutoka Maktaba ya Pambazuko

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea kusikitishwa kutopatikana kwa Humphrey Polepole, aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Cuba.

Akizungumza katika mahojiano na Edwin Odemba wiki iliyopita, katibu wa halmashauri ya chama hicho – Itikadi, Mafunzo na Uenezi, Kenani Kihongozi amesema kuwa CCM inaendelea kufuatilia alipo Polepole na kuhimiza vyombo vya usalama kuongeza nguvu kumpata.

“CCM haitamani kuona hata mtu mmoja anapotea, tunaomba Mungu Polepole apatikane na vyombo vya usalama vinafanya kazi kubwa kufuatilia jambo hili,” amesema Kihongosi.

Kihongozi amesema CCM inaamini vyombo vya usalama vinaendelea kufanya uchunguzi wake kuhusu alipo Polepole na vikikamilisha kazi zake, vitaeleza nini kilitokea na pengine kueleza alipo kada huyo.

Polepole aliyewahi pia kuwa katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho tawala alitekwa na watu wasiojulikana akiwa maeneo ya Ununio, Dar es Salaam alfajiri ya Oktoba 6, 2025.

Familia yake ilisema watu wasiojulikana walivamia nyumba hiyo na kumchukua kwa nguvu, milango ilikutwa imevunjwa, nyaya za umeme zimekatwa na damu ikiwa ndani na nje ya nyumba. Polisi walitangaza uchunguzi, lakini hadi sasa hakuna taarifa ya wazi kuhusu alipo wala waliomchukua.

Kesho yake, mawakili wake waliwasilisha maombi ya habeas corpus Mahakama Kuu, wakitaka mamlaka zimfikishe mahakamani.

Maombi hayo yalitupiliwa mbali Oktoba 24, mwaka jana baada ya mahakama kusema hakuna ushahidi uliothibitisha kwamba taasisi za serikali zilihusika na kutoweka kwake.

Humphrey Polepole Uamuzi huo haukujibu hadharani swali la msingi; Polepole yuko wapi hadi leo?

Kihongosi amesema CCM inaamini uchunguzi unaendelea na kwamba vyombo husika vitatoa maelezo baada ya kukamilisha kazi yake.

Hata hivyo, msimamo huo unakabiliwa na shinikizo la wanaharakati wanaotaka majibu ya haraka na uwajibikaji.

Tigere Chagutah wa Amnesty International amesema kutoweka kwa Polepole kunatia hofu, akiitaka serikali kuweka nguvu zote kumpata, kuhakikisha usalama wake na kuwafikisha wahusika mbele ya sheria.

Mwanaharakati Maria Sarungi Tsehai amesema tukio hilo lilivuka “mstari mwingine mwekundu,” huku Human Rights Watch ikilitaja kuwa jambo la kutisha na kutaka mamlaka ziache kuzima sauti za ukosoaji.

Wanaharakati na watu wengi bado wanahitaji kujua yuko wapi mwanasiasa huyo ambaye baada ya kuamua kuondoka kwenye utumishi wa serikali na kuachia dhamana ya ubalozi, alikuwa “mwiba” kwa watawala akiwatuhumu kwa masuala kadhaa makubwa yakiwamo ya rushwa, uonevu na uvunjifu wa katiba.

“Ikiwa Polepole anashikiliwa kwa tuhuma yoyote, Katiba na sheria vinataka afikishwe mahakamani, ikiwa alitekwa na watu binafsi, serikali ina wajibu wa kuwatafuta na kumrudisha salama,” amesema Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Boniface Mwabukusi.

Mwabukusi amekuwa akieleza kuwa CCM, ikiwa chama tawala na taasisi aliyowahi kuitumikia, ina wajibu mkubwa kuhakikisha Polepole anapatikana akiwa hai, kuliko kueleza masikitiko.

  • Humphrey Polepole
  • CCM
  • Utekaji
  • Haki za binadamu

Soma Pia