Habari
OMO awapa wawakilishi jukumu zito
MWENYEKITI wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, almaarufu OMO, amewataka wajumbe wa wawakilishi kutoka chama hicho kutumia nafasi zao kujenga taasisi imara za uwajibikaji.

Pia, amewahimiza kuhakikisha maridhiano yaliyofikiwa kati ya chama hicho na CCM yanazaa mabadiliko yanayogusa maisha ya Wazanzibari.
Othman amesema mafanikio ya maridhiano hayo hayatapimwa kwa makubaliano yaliyosainiwa pekee, bali kwa uwezo wa viongozi na taasisi za serikali kubadili mfumo wa uendeshaji wa nchi na kuleta matokeo ya kiuchumi na kijamii.
Ametoa kauli hiyo huko Dunga, Wilaya ya Kati, Unguja, alipokutana na viongozi wa ACT Wazalendo kutoka majimbo matatu ya mkoa huo kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kuhusu yaliyomo katika makubaliano yaliyofikiwa kati ya ACT Wazalendo na CCM na kusainiwa Julai 9, 2026, Ikulu Zanzibar.
Akizungumza mbele ya viongozi hao, Othman amesema Zanzibar haiwezi kujenga uchumi wenye ushindani wala kuharakisha maendeleo bila kuwa na viongozi na watendaji wenye uwezo, uadilifu, umakini na utayari wa kuwajibika.
Amesema uzoefu wa mataifa yaliyofanikiwa, ikiwemo Singapore, unaonyesha kuwa rasilimali pekee hazitoshi kujenga uchumi imara bila kuwa na mifumo mizuri ya utawala na watu wenye uwezo wa kuisimamia.
“Kiongozi anayetaka kujenga nchi hatizami uchaguzi; anaangalia hatma na mustakabali wa nchi. Anaangalia namna ya kuijenga nchi, hasa anapoona mwelekeo uliopo siyo mzuri na unaelekea kuwa mbaya zaidi,” amesema.
Kauli hiyo inaweka uzito mpya kwenye nafasi ya wawakilishi katika kipindi ambacho Zanzibar inaingia katika hatua ya utekelezaji wa makubaliano ya kisiasa yaliyolenga kupunguza migawanyiko na kujenga mazingira mapya ya kisiasa.
Wawakilishi na mabadiliko
Othman, ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar mstaafu, amesema moja ya maeneo muhimu katika utekelezaji wa maridhiano ni kujenga taasisi zinazoweza kuisimamia serikali na kuhakikisha viongozi wanawajibika kwa wananchi.
Amesema Baraza la Wawakilishi linapaswa kuwa miongoni mwa mihimili yenye uwezo wa kuihoji serikali na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Kwa mtazamo huo, amesema ubora wa Baraza la Wawakilishi hauanzi siku linapokutana kufanya shughuli zake, bali huanzia katika mchakato wa kisheria unaomuwezesha mwakilishi wa wananchi kupata nafasi hiyo.
“Nidhamu kubwa ya kuendesha nchi ni kuhakikisha tuna watumishi na viongozi bora wenye uwezo wa kusukuma kasi ya ufanisi, sambamba na kuwa na vyombo madhubuti vya kuichunga serikali,” amesema. Amesisitiza kwamba taaluma pekee haiwezi kuwa kipimo cha uongozi bora bila kuambatana na uadilifu.
Uchumi bado ni changamoto
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Othman amesema Zanzibar imefikia hali ngumu kiuchumi na kimaendeleo licha ya kuwa na rasilimali ambazo, kwa mtazamo wake, zingeweza kubadili maisha ya wananchi.
Amesema hali hiyo inahitaji viongozi kuangalia zaidi mustakabali wa nchi kuliko maslahi ya kisiasa ya muda mfupi.
OMO amesema mwelekeo huo ndio uliokuwa msingi wa mazungumzo kati ya ACT Wazalendo na CCM, akisisitiza kwamba dhamira kuu ilikuwa kujenga nchi.
- ACT Wazalendo
- Zanzibar
- Maridhiano
- CCM