Uchambuzi
Kujiuzulu Dkt Nchimbi mwisho au mwanzo wa mgogoro?
KUJIUZULU kwa Dkt. Emmanuel Nchimbi kutoka nafasi ya Makamu wa Rais kumeongeza machungu mengine ya kufukuzwa kwake uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hatua hiyo imezua mshituko, mshangao, wasiwasi na hofu kwa watu wengi.
Ingawa wengi wana uhakika kuwa hatua hiyo inaweza isilete migongano itakayosababisha hitilafu kubwa, lakini wachambuzi wanasema ni dhahiri kuwa jambo hilo litasababisha mtikisiko ambao - usipodhibitiwa vyema, unaweza kuliyumbisha taifa.
Dkt. Nchimbi alitangaza Agosti 25 kwamba angejiuzulu nafasi ya Makamu wa Rais na kustaafu siasa pamoja na utumishi wa umma kuanzia Septemba 4.
Katika barua yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan, alisema amefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kwamba Rais alitaka makamu mwingine wa rais. Rais Samia alikubali kujiuzulu kwake.
Siku iliyofuata, CCM ilitangaza kumvua Dkt. Nchimbi uanachama wakimvika tuhuma za kukiuka maadili, kanuni na taratibu za chama.
Ingawa wengi tulitarajia jambo kama hili kutokea, lakini wengi hawakutarajia litatokea kwa namna lilivyotokea au kwa kasi namna hiyo.
Ndio maana mfuatano huo wa matukio umeibua maswali kuhusu mambo yaliyokuwa yakitokea nyuma ya pazia.
Ingawa hakuna ushahidi uliowekwa wazi hadharani unaothibitisha kwamba Dkt. Nchimbi alilazimishwa kujiuzulu, lakini kauli yake kuwa alikuwa amejithibitishia kuwa rais alihitaji mabadiliko inaleta taswira kuwa kujiuzulu kwake hakukutokana na utashi wake, bali alisukumwa. Vivyo hivyo, ingawa hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai yanayosambaa kuhusu alipo au kwamba amezuiwa kufanya shughuli zake, ukimya uliotawala tangu kujiuzulu kwake, na wasiwasi ulioibuliwa na baadhi ya watu ambao walishawahi kukutwa na kadhia kama hizo, kumezusha hofu nyingine kuhusiana na usalama wa kiongozi huyo mstaafu.
Waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, ambaye wakati fulani alisema kuwa aliwahi kupokea vitisho kuhusu usalama wake baada ya kutoa maoni kuhusiana na masuala mbalimbali ya kisiasa, ni mmoja wa watu walioonesha hofu kuhusu usalama wa Dkt. Nchimbi.
Wengi wanakumbuka madhila yaliyowakuta watu kama Aboud Jumbe, ambaye baada ya “kujiuzulu” nafasi ya makamu wa rais, aliishia kuwekwa katika kifungo cha ndani nyumbani kwake Kigamboni.
Wengine wamemkumbuka Horace Kolimba ambaye alifariki katika mazingira yenye utata baada ya kuitwa kuhojiwa na chama chake huko Dodoma baada ya kukikosoa hadharani akiwa Katibu Mkuu.
Ombwe laibuka.
Hata hivyo, ukiacha hofu hiyo, kasi na mazingira ya kuondoka kwa Dkt. Nchimbi vimeacha ombwe la kisiasa ambalo limezalisha zaidi minong’ono na kutoa tafsiri mbalimbali.
Muhimu zaidi, tukio hili limefufua swali la muda mrefu katika siasa za Tanzania; je, ndani ya CCM au serikali kuna nafasi ya kutofautiana kimtazamo kwa mwanasiasa mwenye cheo cha juu bila kuonekana kuwa anapingana na mwelekeo wa chama au serikali?
Kuna orodha ndefu ya viongozi wa aina hiyo, lakini wa mwisho anayekumbukwa sana ni Humphrey Polepole.
Kivuli cha Aboud Jumbe.
Kwa Watanzania wengi, tukio la Nchimbi limefufua kumbukumbu za Aboud Jumbe, makamu mwingine wa rais ambaye safari yake ya kisiasa ilifikia kikomo kwa namna ya kushangaza baada ya kutofautiana na uongozi wa wakati huo.
Jumbe alijiuzulu (baadhi wanaamini kuwa kwa kulazimishwa) Januari 1984 akiwa Rais wa Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Makamu Mwenyekiti wa CCM, wakati kukiwa na mvutano mkubwa kuhusu mustakabali wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar.
Msimamo wake wa kuunga mkono muundo wa Muungano wa serikali tatu ulimweka katika mvutano na mfumo wa serikali mbili uliokuwa ukiungwa mkono na chama. Baada ya kujiuzulu, uhuru wake wa kisiasa na kijamii ulizuiwa kwa kiasi kikubwa, na hatimaye akaishi nje ya kitovu cha siasa hadi alipofariki mwaka 2016.
Kwa muda sasa kumekuwa na minong’ono kuwa kauli za Dkt. Nchimbi, hasa kuhusu Katitoelewana kwake na baadhi ya vigogo wenzake ndani ya CCM na serikali.
Ndio maana kujiuzulu kwake kunaonekana kuwa ni kwa kulazimishwa na hakukutokana na utashi wake binafsi.
Ulinganisho huo unatiwa nguvu kwa sababu visa vyote viwili vinamhusu mwanasiasa mwenye cheo cha juu ndani ya mfumo wa utawala ambaye msimamo wake wa kisiasa ulionekana kukinzana na mwelekeo ndani ya chama na serikali.
Ndiyo maana kauli za Jaji Mkuu mstaafu Joseph Warioba zimevuta hisia. Warioba, ambaye pia ni mwanasiasa mkongwe wa CCM na Waziri Mkuu mstaafu, alihoji msingi wa madai kwamba Nchimbi anaweza kuwa kizuizini, huku akitambua kwamba kutokuwepo kwake hadharani kumezua wasiwasi.
Wasiwasi huo wenyewe ni jambo la kuzingatiwa. Katika mfumo wa kisiasa ambao bado una kumbukumbu za migogoro ya ndani ya chama, kutokuonekana hadharani kwa mwanasiasa maarufu kunaweza kugeuka kuwa suala la maslahi ya umma.
Katiba Mpya, mvutano wa kisiasa.
Msimamo wa Dkt. Nchimbi kuhusu mabadiliko ya Katiba ni sehemu nyingine ambayo inaelezwa kuwa imechochea mazingira ya kuondoka kwake.
Kwa hiyo, ingeshangaza kama isingezua Mwezi Julai, Dkt. Nchimbi alisikika akiwataka Watanzania kupambana kudai Katiba Mpya.
Aliuaminisha umma kuwa hilo ni takwa la Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa mtazamo mpana, msimamo huo ulikwenda sambamba na mjadala wa kisiasa nchini, kwa kuwa suala la Katiba Mpya limekuwa sehemu ya mijadala ya siasa Tanzania kwa miaka mingi na pia limewahi kutajwa hata katika ilani za CCM. Pengine ndio maana Dkt. Nchimbi akatoa kauli kuwa hata Rais naye anaitamani Katiba Mpya.
Lakini siku chache baadaye ikaanza kusikika minong’ono kuwa “wakubwa” kadhaa ndani ya CCM na serikali hawakufurahishwa na kauli hiyo.
Baadhi walihoji hadharani kuwa Dkt. Nchimbi anataka watanzania wapambane na nani!
Jambo moja ni dhahiri. Katika migongano ya kisiasa kuhusiana na suala la Katiba Mpya, kauli ya Dkt. Nchimbi, ambaye alikuwa Makamu wa Rais aliyekuwa madarakani, ilikuwa na uzito mkubwa zaidi kisiasa, pengine kuliko hata mashinikizo ya miaka mingi ya wanasiasa wa upinzani na wanaharakati.
liko ya Katiba ni miongoni mwa masuala nyeti yanayoikabili Tanzania.
Suala hilo pia linaingiliana na uhusiano kati ya CCM na taasisi zenye ushawishi nje ya chama.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), kwa mfano, limekuwa likitoa kauli kuhusu utawala, demokrasia, mabadiliko ya Katiba na masuala mengine ya kitaifa.
Mtazamo wa Dkt. Nchimbi kuhusu baadhi ya mijadala hiyo umeongeza tafsiri kuhusu uwepo wa tofauti za kisiasa ndani ya mfumo wa uongozi, huku baadhi ya wanasiasa wakimnasibisha Dkt. Nchimbi na TEC, hasa kwa kuwa naye ni Mkatoliki kindakindaki.
Athari kwa CCM.
Ukizingatia kuwa haya yanatokea wakati ambapo CCM inajiandaa kwa uchaguzi ndani ya chama, kuondoka kwa Dkt. Nchimbi, ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, ni dhahiri kutaleta misuguano.
Uzoefu unaonesha kuwa chaguzi hizi hutumiwa na baadhi ya watu wenye dhamira ya kuwania vyeo vya juu ndani ya chama au serikali kupanga safu kuelekea uchaguzi mkuu, wakitafuta uungwaji mkono.
Kwa miongo kadhaa, chama hicho kimeweza kusimamia makundi yenye maslahi tofauti, matarajio ya kisiasa na mitandao ya uongozi, huku kikidumisha utawala wake.
Wanasiasa wakuu wamepanda na kushuka, miungano ya kisiasa imebadilika na makundi yameibuka na kutoweka, lakini CCM imeendelea kuonyesha uwezo wa kujipanga upya.
Ndio maana kuvuliwa kwa Dkt. Nchimbi uanachama kunatafsiriwa na baadhi ya wachambuzi kama sehemu ya upangaji upya wa safu ndani ya chama kuelekea uchaguzi mkuu.
Baadhi ya wachambuzi wamehusisha kuondoka kwake na kupungua kwa ushawishi wa mitandao ya kisiasa ambayo wakati mmoja ilikuwa na nafasi muhimu katika michakato ya uchaguzi wa viongozi ndani ya CCM. Iwapo tafsiri hiyo ni sahihi, muda ndio utakaothibitisha.
Kitu kilicho wazi, hata hivyo, ni kwamba Tanzania inaingia katika kipindi ambacho maswali na majadiliano kuhusu nani anadhibiti chama, nani anaunda mwelekeo wa sera na nani anashikilia nafasi muhimu za kimkakati yatazidi kuwa muhimu.
Mchakato ujao wa kisiasa ndani ya chama, kwa hiyo, utafuatiliwa kwa karibu.
Swali jingine kubwa ni iwapo kuondoka kwa Dkt. Nchimbi ni mgogoro wa mtu mmoja au ni sehemu ya upangaji upya mpana zaidi wa mfumo wa kisiasa kuelekea chaguzi zijazo na mchakato wa urithi wa uongozi ndani ya chama na serikali.
Ni mtihani mkubwa zaidi.
Suala la kujiuzulu kwa Dkt. Nchimbi linaenda mbali zaidi ya hatima yake binafsi.
Tukio hili limeipa CCM fursa ya kuonyesha namna chama kikubwa na chenye muda mrefu madarakani kinavyoweza kushughulikia tofauti za kimtazamo miongoni mwa viongozi wake wakuu.
Kila chama cha siasa kinahitaji nidhamu, lakini mfumo wa kisiasa uliokomaa pia unahitaji njia ambazo tofauti za maoni zinaweza kuwasilishwa bila moja kwa moja kutafsiriwa kuwa tishio kwa mustakabali wa mwanasiasa.
Kwa Tanzania, suala hili ni muhimu kwa sababu CCM si chama cha kawaida tu. Kikiwa madarakani tangu uhuru, mienendo yake ya ndani ina athari kubwa kwa serikali na jamii kwa ujumla.
Kwa hiyo, kuondoka kwa Dkt. Nchimbi hakutakuwa tu mabadiliko ya kawaida ya uongozi, bali kutaumba historia ndefu ya mamlaka, utii na kutofautiana ndani ya CCM.
Hapa, watu wasijikite tu kuhusu hatima ya Dkt. Nchimbi bali pia namna CCM itakavyoweza kuogelea katika wimbi hili.
Kwa upande mwingine serikali nayo ina mtihani wa itakavyoshughulikia maswali kuhusu hali ya Dkt. Nchimbi baada ya kuondoka madarakani, na iwapo viongozi waandamizi wataendelea kuwa na nafasi ya kueleza mitazamo inayotofautiana.
Historia imetoa mifano kadhaa ya namna tofauti za kimtazamo ndani ya uongozi wa juu zinavyoweza kugeuka kuwa migogoro mikubwa zinapogeuka kuwa masuala ya mtu binafsi.
Kuondoka kwa Nchimbi kumeifufua historia hiyo na changamoto kwa uongozi wa sasa ni kuhakikisha kwamba historia isiendelee kujirudia.
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- Emmanuel Nchimbi
- CCM
- Katiba Mpya
- Aboud Jumbe