Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Vituko vya Wakubwa

‘Maajabu’ ya Rais Mobutu akiwa Ikulu - III

TUNAENDELEA simulizi na visa, vituko na mikasa vilivyofanywa na Rais wa Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), Mobutu Sesseseko Kuku wa Zabanga.

Jumatatu, 14 Septemba 2026 · 03:00Dakika 4 kusomaToleo 182, uk. 32

TUNAENDELEA simulizi na visa, vituko na mikasa vilivyofanywa na Rais wa Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), Mobutu Sesseseko Kuku wa Zabanga.

Kiongozi aliyechukua madaraka baada ya mapinduzi, miaka michache baada ya kifo cha rais wa kwanza baada ya wakoloni, Patrice Lumumba.

Mobutu, kwa lugha ya vijana, alikuwa ‘chuma’ kweli. Nani angethubutu kumnyoshea kidole katika zama zake?

Hata hivyo, hakuna marefu yasiyokuwa na ncha, hatimaye Mobutu aliyekuwa mtu wa ‘kula bata’ na mvinyo kutoka Paris Ufaransa, Monaco na Rabat alifika mwisho.

Siku chache kabla ya kuondolewa madarakani kupitia mapinduzi yaliyoongozwa na Laurent-Désiré Kabila, waliomshuhudia Mobutu siku chache kabla ya kupinduliwa kwake mwaka 1997, walisema alikumbwa na wasiwasi mkubwa, kiasi cha kushindwa kula kwa siku kadhaa.

Ikumbukwe kuwa kabla ya kupinduliwa alianza kukumbwa na majaribio kadhaa ya mapinduzi na baadaye akapata dhoruba ya ugonjwa wa kansa ya korodani.

Kipindi ambacho urais wake uliingia kwenye majaribio ya kupinduliwa na uasi kuongezeka ni miaka ya 1992 hadi 1997, katika kipindi hicho urais wake haukuwa wa kula bata tena, kwani hata yeye mwenyewe aliona wazi kuwa “Zaire siyo mali yake tena.”

Ni kipindi ambacho hata askari ambao walikuwa watiifu kwake, walianza kumsaliti.

Mwaka 1986, Mobutu alianza kutetea ufalme wake, aliunda kikosi maalumu cha ulinzi wake binafsi kilichojulikana kwa jina la DSP, ambacho kilikuwa katili kwa kila aliyeshukiwa kuwa “mpinzani.”

DSP kilikuwa na wanajeshi wanaokadiriwa kufikia 10,000, huku wengi wao wakitoka kabila la Mobutu la Ngbandi. Wanajeshi hao walikuwa wanapewa mafunzo nchini Israel, pamoja na kuwa na vifaa vya kisasa kabisa.

Ikumbukwe kuwa kabla ya Mobutu, Zaire iliongozwa na rais wake wa kwanza aliyeitwa Joseph Kasavubu, huyu alilindwa na mwanajeshi mmoja au wawili.

Mara nyingi alipokuwa akitembea hakuwa na msafara wowote.

Wanajeshi wa DSP walilipwa vizuri zaidi na Mobutu, na aliwaamini sana. Kila alipokwenda kuishi kijijini kwake ambako baadaye uligeuka kuwa mji, huko Gbadolite alisindikizwa na wanajeshi 300 ikiwa ni kwa ajili ya ulinzi tu.

Ijumaa ya Mei 16, 1997, Mobutu alinusurika kufa, wakati akiwa Uwanja wa Ndege wa Ndiji karibu na Kinshasa. Akiwa ndani ya ndege, dakika za mwisho ndege ianze kuruka, mkuu wa usalama wa Mobutu, Kanali Motoko alipokea taarifa ya kiintelijensia kuwa kwenye shamba kubwa lililokuwa karibu na uwanja huo kuna gari la jeshi aina ya jeep likiwa na vifaa vyote vya kudungulia ndege ya Mobutu.

Kanali Motoko alimwambia rubani wa ndege hiyo ya rais abadili uelekeo wa kurusha ndege hiyo, lakini rubani alikataa akidai upepo hauruhusu kufanya hivyo.

Kanali Motoko anamwambia Mobutu jambo hilo, Mobutu akamwamuru rubani afuate uamuzi wa mkuu wa usalama.

Ndege ilibadili uelekeo, na wale wanajeshi waliokuwa wakisubiri waitungue walihaha na kuanza kukimbia karibu na ndege inakorukia ili waitungue, lakini walipata ajali na wote walikufa papo hapo. Mobutu akaenda zake salama Gbadolite ‘kula bata’.

Jaribio la pili kubwa

Baada ya kufika huko kijijini kwake, mwanajeshi mmoja kutoka kikosi cha DSP, aliomba wasaa wa kumnong’oneza Mobutu na alipaswa kuanzia kwa mkuu wa kikosi hicho ili kupata ruhusa.

Alipofika kwa mkuu huyo, Kanali Motoko alikataa, kumruhusu na baadaye aliamuru askari huyo akaguliwe mwili mzima. Baada ya ukaguzi alikutwa kajifunga mabomu.

Alipoulizwa ya nini anapanga kumuua Rais Mobutu na ametumwa na nani kufanya hivyo? Alijibu kwa kifupi tu kwamba alichoshwa na tabia za Mobutu hivyo alitaka ajitoe muhanga ili wafe wote.

Siku moja msaidizi wa mlinzi mkuu wa Mobutu, Meja Ngani Yanda Mokomba, wakati anafanya ukaguzi wa njia, akiwa huko alikutana na kikosi cha DSP kikirudi kutoka Gbadolite huku wakiimba “Mobutu msaliti, ndugu yake Nzimbi amekimbilia Brazaville katuacha sisi tufe, twendeni tukamkamate Mobutu.”

Meja Ngani alikwenda chumbani kwa Mobutu, alimkuta kiongozi huyo kavaa shati lake bila fulana, na viatu bila soksi, akamwambia watoroke. Mobutu akakataa, akidai anataka kufia nyumbani kwake. Mobutu anawaambia mlinzi huyo awamchukue mkewe na pacha wa mkewe, yeye wamuache afie hapo.

Meja Ngani alikataa kumwacha bosi wake.

Alimbeba Mobutu mgongoni baada ya kumuomba samahani kwa sababu kulikuwa na sheria kali kwamba hairuhusiwi mlinzi wa rais kumshika rais.

Mobutu alibebwa mgongoni huku pia akiwa dhaifu kutokana na maradhi ya kansa ya kibofu yaliyoanza kumtafuna.

Meja Ngani ambaye pia alikuwa rubani, alipofika uwanja wa ndege ambao haukuwa mbali na kwenye hekalu lake, hakukuta ndege ya Rais Mobutu, aliamua kuiteka ndege ya Urusi iliyokuwa imeleta vifaa vya kijeshi kwa Jonas Savimbi (Savimbi alikuwa rafiki mkubwa wa Mobutu), wakati huo alikuwa amempa hifadhi ya ardhi ya Congo kutumika kuihujumu serikali ya Angola.

Makala haya yaliyoandikwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali ikiwamo mitandao, yataendelea wiki ijayo.

Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.

  • Mobutu Sese Seko
  • DRC
  • Zaire
  • Historia

Soma Pia