Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Makala ya Kimataifa

eSwatini yenye tabasamu inavyoficha sura ya hofu

IDADI kubwa ya watu huitazama na kuipa tafsiri eSwatini kupitia nyuso tatu zenye tabasamu; Mfalme Mswati III, Mama Malkia LaTfwala na Waziri Mkuu Russell Dlamini.

Jumatatu, 10 Agosti 2026 · 16:15Dakika 4 kusomaToleo 177, uk. 35 & 36

Nyuma yao kuna milima ya kijani, mabonde yenye kuvutia na mandhari tulivu yanayoifanya nchi hiyo ionekane kama kisiwa cha amani kusini mwa Afrika.

Taswira hiyo huvutia karibu watalii 800,000 kwa mwaka. Wageni, wakiwamo viongozi wa mataifa mbalimbali, hupokewa kwa bashasha na kuonyeshwa uzuri wa ufalme huo.

Hata uamuzi wa Mfalme Mswati wa kubadili jina la nchi kutoka Swaziland kwenda eSwatini mwaka 2018, uliwasilishwa kama kurejesha hadhi na utambulisho wa asili.

Lakini ukitazama nyuma ya tabasamu, milima na sherehe za kifalme, unaiona nchi nyingine; taifa lililofunikwa na hofu, ukimya, umaskini na mamlaka yasiyopingwa.

Chanzo kimoja kilimweleza mwanasayansi wa siasa, Nqobile Mkhatshwa kuwa serikali imejenga hofu, kisha ukimya unaotokana na hofu hiyo hutafsiriwa kwa makusudi kama furaha na amani ya wananchi.

Jeraha la mwaka 2021

Sura hiyo ilijitokeza wazi Juni 2021, maandamano yalipozuka kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, upungufu wa walimu na matumizi makubwa ya viongozi.

Serikali ilijibu kwa nguvu ya dola na kusababisha mtu wa kwanza kuuawa Juni 29, na baadaye zaidi ya watu 60 waliripotiwa kupoteza maisha.

Hadi leo, mauaji hayo hayajadiliwi kwa uwazi na hakuna uwajibikaji unaoonekana.

Baada ya umwagaji damu, mhariri mmoja, Bheki Makhubu alisema hakuna mtu aliyethubutu tena kupaza sauti.

Wabunge hawa; Magawugawu Simelane, Bacede Mabuza na Mthandeni Dube walipoibua suala hilo, waliondolewa bungeni.

Simelane alikimbilia uhamishoni, huku Mabuza na Dube wakifungwa. Mabuza anatumikia kifungo cha miaka 25 na ameeleza hofu kuhusu usalama wake gerezani.

Kiongozi wa chama cha People’s United Democratic Movement, Mlungisi Makhanya, naye aliripotiwa kunusurika jaribio la kuuawa akiwa uhamishoni.

Mwanzoni mwa maandamano, huduma ya intaneti ilizimwa kwa saa 216. Kampuni ya MTN ilishutumiwa kwa kushirikiana na serikali, ingawa haikuwajibishwa.

Tume ya Kimataifa ya Wanasheria iliita hatua hiyo “isiyokuwa ya lazima na isiyolingana na hali,”

ikikadiria kuwa uchumi ulipoteza dola milioni 15.8.

Wachache matajiri, shida za wengi

Mgongano kati ya tabasamu la dola na maisha ya wananchi unaonekana pia katika uchumi.

Mwaka huu, wabunge waliongezewa mishahara kwa asilimia 54, na kufikisha malipo yao zaidi ya Rand milioni moja kwa mwaka. Kiasi hicho ni sawa na Shilingi za Tanzania milioni 162.

Wakati huo, watumishi wa umma waliachwa bila nyongeza na kulazimika kuandamana.

Waziri Mkuu Dlamini mwenyewe amekiri kuwa theluthi mbili ya wananchi wanaishi chini ya mstari wa umaskini. Chini ya Shilingi 3,000 za Tanzania kwa siku.

Elimu na afya zinaendelea kukabiliwa na uhaba wa fedha, huku matumizi ya dola na vyombo vya usalama yakipewa uzito.

Sikhumbuzo Thomo wa Swaziland Solidarity Network anasema kila fedha inayoongezwa kwa vikosi vya usalama inapunguza fedha za zahanati, vitabu vya shule na maafisa ugani wanaohitajika kuongeza uzalishaji wa wakulima.

Mfumo wenyewe unaendeleza pengo hilo. Seneti yenye wajumbe 30, ambao wengi huteuliwa na mfalme, inaweza kuzuia uamuzi wa wawakilishi waliochaguliwa. Hivyo swali linabaki; taasisi hizo zinawatumikia wananchi au kulinda mfumo wa kifalme?

Amani yao, hofu inayoishi

Mfalme Mswati anaendelea kuhubiri amani, lakini wanaharakati wanasema kauli hiyo inalenga kuipamba nchi mbele ya jumuiya ya kimataifa.

Rais wa Umoja wa Kitaifa wa Wanafunzi wa Swaziland, Vusi Simelane, anayeishi uhamishoni, amesema Waswazi wametekwa, kufungwa, kulazimishwa kukimbia na hata kuuawa.

Kisa kinachobeba uzito mkubwa ni mauaji ya wakili wa haki za binadamu na mwandishi wa habari Thulani Maseko. Januari 2023, Maseko alipigwa risasi mbele ya familia yake, muda mfupi baada ya mfalme kutoa kauli kali dhidi ya waliohusishwa na machafuko.

Mjane wake, Tanele Maseko, amesema anaamini mfalme anajua aliyehusika. Hakuna jibu la kuridhisha lililotolewa kuhusu mauaji hayo.

Maseko – kupitia uwezo wake mkubwa wa kuandika na kuzungumza, alipendwa na kufuatiliwa na wengi. Alikuwa akihamasisha mazungumzo ya kitaifa.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa na Mswati waliwahi kukubaliana kuwa sekretarieti ya kikanda isaidie kuanzisha jukwaa la kuleta maelewano, lakini juhudi hizo zimefifia.

Mfalme hajakutana hadharani na waathirika au familia za waliouawa mwaka 2021.

Kwa utamaduni wa Waswazi, kiongozi wao anapaswa kuwa mlinzi wa watu wake, siyo mtawala anayewaacha na majeraha yasiyoponywa.

Afrika inayotazama pembeni

Ukimya wa majirani nao unaisaidia eSwatini kuficha hali yake. Viongozi na mabalozi wa Afrika huahidi kuendeleza ushirikiano na serikali bila kugusia ukiukwaji wa haki za binadamu.

Mwandishi wa habari za uchunguzi, Zweli Dlamini anaamini washirika wa Mswati wanapuuza ukatili kwa sababu ya maslahi yao ya kisiasa na kiuchumi.

Ndani ya nchi, vyama vya siasa vimepigwa marufuku, vyama vya wafanyakazi na harakati za wanafunzi vimebaki nguzo kuu za kudai demokrasia, lakini hukabiliwa na vikwazo.

Serikali ilipiga marufuku maandamano ya Mei Mosi, na mwanaharakati aliyekamatwa kwa kuvaa fulana yenye kuhamasisha amani na mabadiliko, alifariki kizuizini; serikali ikadai alijiua.

Pamoja na mambo mengine, wanaharakati wa nchi hiyo wamekuwa wakiishutumu serikali kwa kutoa pasipoti za kidiplomasia kwa mhubiri Uebert Angel na mfanyabiashara Wicknell Chivayo, ambao siyo Waswazi.

Maswali zaidi yaliibuka baada ya eSwatini kupokea wafungwa 11 kutoka Marekani katika makubaliano yaliyoelezwa kuwa na thamani ya dola milioni 5.1.

Waziri Mkuu Dlamini anasisitiza kuwa wananchi wanapendelea mfumo wa uongozi wa Tinkhundla.

Mfumo huo ulianzishwa mwaka 1973 na Mfalme Sobhuza II baada ya kuvunja Katiba, kufuta vyama vya siasa na kujikusanyia mamlaka makubwa ya kiutendaji, kisheria na kimahakama.

Hata hivyo, utafiti wa Chuo Kikuu cha Swaziland unaonyesha kuwa wanaotaka ubadilishwe ni wengi kuliko wanaouunga mkono.

Hiyo ndiyo eSwatini inayofichwa na tabasamu la kifalme, mandhari ya milima na lugha ya amani.

Nje, ni ufalme mtulivu unaowakaribisha watalii; ndani, ni jamii inayozuiwa kuzungumza, kuandamana na kuamua mfumo wa utawala inaoutaka.

Mpaka hofu itakapoondolewa, haki kutendeka na wananchi kuruhusiwa kushiriki kikamilifu, picha inayouzwa duniani itaendelea kuwa pazia linalofunika uhalisia mchungu.

Mwandishi anaishi Afrika Kusini na imetafsiriwa na Pambazuko kwa ombi lake.

  • eSwatini
  • Haki za binadamu
  • Afrika

Soma Pia