Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Uchumi & Biashara

TTCL yapanua mtandao wa intaneti

KAMPUNI ya Mawasiliano Tanzania (TTCL), imezindua awamu ya pili ya upanuzi wa mtandao wake wa intaneti ya majumbani.

Jumatatu, 7 Septemba 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 181, uk. 19

Awamu hii upanuzi huo unalenga kuwafikia wateja wapya wa majumbani 400,000. Upanuzi wa mradi huo umezinduliwa na Waziri wa Mawasiliano, Angellah Kairuki (pichani).

Mpango huo uliopewa jina la kibiashara la Faiba Mlangoni Kwako, tayari umeunganisha wateja wa majumbani 280,000 katika awamu ya kwanza.

TTCL inazinduza mpango huo wakati taarifa zinaonyesha kuwa idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za intaneti nchini imefikia milioni 62.8.

Lakini katika idadi hiyo, wateja ambao wameunganishwa kwa waya wa faiba majumbani ni 178,904 tu.

Akizindua mpango huo, Kairuki aliiagiza TTCL kuharakisha kazi hiyo ili kuhakikisha kuwa lengo lililowekwa linafikiwa haraka.

Aidha, alisisitiza kuwa kusambaa kwa huduma hiyo ya majumbani kuendane na kupungua kwa gharama zake ili kuwawezesha Watanzania wengi kumudu kuitumia huduma hiyo.

Pia aliiasa TTCL kuhakikisha kuwa intaneti hiyo inakuwa na ubora na kasi kubwa sambamba na huduma bora kwa wateja ili kuhakikisha kuwa wateja wanapata thamani ya fedha wanazotumia kulipia huduma.

Alisema mafanikio ya huduma hiyo hayapaswi kupimwa tu kwa kuangalia ukubwa wa eneo ambalo huduma imefikishwa, bali kwa idadi ya watumiaji wa majumbani ambao wameunganishwa na wananufaika na huduma hiyo.

Waziri Kairuki aliitaka TTCL kusambaza huduma hiyo pia kwenye maeneo ya biashara, viwandani, shuleni, vyuoni, vituo vya afya na ofisi za serikali.

Alisisitiza kuwa hilo litawezekana iwapo TTCL itarahisisha taratibu za usajili, kupunguza muda wa mteja kusubiri kuunganishwa, na kuimarisha ubora wa huduma bila kusahau kuwahudumia wateja wenye matatizo kwa wakati.

Kairuki aliweka vigezo ambavyo alisema TTCL inapaswa kuvizingatia ili kujihakikishia kuwa inatoa huduma stahiki kwa wateja wake.

“Vipimo vya ufanisi viwe ni idadi ya wateja waliounganishwa, muda wa kuunganishwa na huduma, kasi ya intaneti, upatikanaji wa huduma muda wote na kutatua matatizo ya wateja kwa haraka. Kama mkifanya hivi wateja wataridhika kwa sababu wataona thamani ya fedha waliyotumia kujiunga wameipata,” alisema.

Alisema jinsi dunia inavyozama kwenye teknolojia sasa hivi, intaneti yenye kasi kubwa siyo anasa, bali ni huduma muhimu na lazima katika uzalishaji wa kisasa, utoaji elimu na maarifa na pia katika shughuli za kiuchumi kama vile biashara na kwa wafanyabiashara wadogo wadogo.

Akisisitiza umuhimu wa huduma hiyo, Kairuki alisema hata huduma nyingi za serikali hivi sasa zinatolewa kupitia mitandao hivyo kuimarika kwa huduma hiyo kutawasaidia wananchi wanaotafuta huduma za serikali kuzifikia kwa haraka na wepesi.

Utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya utekelezsaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050, ambayo inalenga kuhakikisha kuwa asilimia 70 ya wananchi wote nchini wanaunganishwa na wanatumia huduma za intaneti.

Aidha, dira hiyo inalenga kuhakikisha kuwa aislimia 80 ya huduma zinazotolewa na serikali zitolewe kupitia mtandao ifikapo 2050.

Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.

  • TTCL
  • Intaneti
  • Mawasiliano

Soma Pia