Habari
AI darasani ni msaidizi wa elimu au njia ya mkato?
Hilo ndilo eneo ambalo sasa linahitaji mjadala mpana. Tatizo siyo teknolojia yenyewe, vyuo, walimu na wazazi kuweka mpaka kati ya AI kama nyenzo ya kujifunzia na AI kama njia TEKNOLOJIA ya Akili Mnemba (AI) imeingia kwa kasi katika maisha ya kusaka elimu kwa wanafunzi wa Tanzania, kuanzia shule za sekondari hadi vyuo vikuu.
Wengi wa wanafunzi hawa wanaitumia kutafuta taarifa, kufafanua mada ngumu, kufanya utafiti na hata kusaidia kuandika kazi wanazopewa darasani.
Lakini kadiri matumizi hayo yanavyoongezeka, swali jipya linaibuka katika mfumo wa elimu; je, AI inawasaidia wanafunzi kujifunza zaidi, au inawajengea utamaduni wa kupata majibu bila kufikiri?
kibinadamu.
Mkufunzi wa Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ), Ally Salum, anafananisha ujio wa AI na mapinduzi yaliyosababishwa na kuenea kwa intaneti.
Kwa mtazamo wake, AI haipaswi kuonekana kama “adui” wala “mwokozi,” bali kama teknolojia inayobadilisha namna kazi na elimu zinavyofanyika.
Anasema AI inaweza - kwa mfano, kuwa kama mkufunzi binafsi anayemsaidia mwanafunzi kujifunza kulingana na kasi na kiwango chake cha uelewa.
Kwa walimu, inaweza kusaidia kuandaa mipango ya masomo, maswali na tathmini, na hivyo kutoa muda zaidi wa kushughulikia maeneo yanayohitaji mwingiliano wa binadamu.
Lakini Salum anaweka mpaka muhimu; “AI ni nzuri ikiwa inatumika kama daraja la maarifa, lakini ni mbaya ikiwa inatumika kuwa badala ya fikra.”.
Hatari ya ‘uvivu wa kufikiri’ Salum anaonya kuwa mwanafunzi anapoiomba AI imwandikie pendekezo la utafiti, insha au programu ya kompyuta na kisha kuwasilisha kazi hiyo bila kupitia mchakato wa kusoma, kuchanganua na kuhoji majibu aliyopata, anaweza kukosa mazoezi muhimu ya kufikiri kwa kina.
Elimu ya juu haikusudiwi kumpa mwanafunzi majibu pekee, bali inapaswa kumfundisha namna ya kuyatafuta, kuyachambua, kuyahoji na hatimaye kuyatumia kutatua matatizo.
Matumizi holela ya AI, kwa hiyo, yanaweza kuibua tatizo kubwa zaidi kuliko udanganyifu wa kitaaluma; kuzalisha wahitimu wenye vyeti, lakini wasiokuwa na ujuzi unaolingana na elimu waliyoipata.
Mwalimu Anna John wa Shule ya Msingi Kijichi, Dar es Salaam, ana hofu inayofanana; anasema kutegemea AI kupita kiasi kunaweza kudumaza uwezo wa mwanafunzi kujitegemea katika kufikiri.
Pia anaonya kuwa majibu yanayotolewa na AI siyo lazima yawe sahihi wakati wote, hivyo, mwanafunzi asiye na uwezo wa kuchunguza na kuthibitisha taarifa anaweza kuishia kujifunza jambo lisilo sahihi.
AI siyo lazima iwe adui Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Idara ya Sanaa Bunifu, Dkt. Dominicus Makukula, anaona mjadala wa sasa ukifanana na hofu iliyowahi kujitokeza wakati vikokotoo vilipoanza kutumiwa na wanafunzi.
Anasema wakati huo, baadhi ya walimu waliamini matumizi ya ‘calculator’ yangedhoofisha uwezo wa wanafunzi kufanya hesabu. Baadaye, anasema, ilionekana kwamba uwepo wa kifaa hicho haukumaanisha moja kwa moja mwanafunzi angefaulu.
Dkt. Makukula, anasema AI pia haiwezi kumfanya mwanafunzi apoteze maarifa moja kwa moja; kinachoamua ni namna anavyoitumia.
Anasema hata wanafunzi wanapotumia AI katika kazi wanazopewa, mwalimu anayewafahamu vizuri anaweza kubaini iwapo kazi inayowasilishwa haiendani na uwezo wao wa kawaida.
“Nadhani hatuna sababu ya kuogopa jambo hilo,” anasema Dkt. Makukula.
Catherine Ernest, mhitimu wa chuo kikuu, naye anaona pande zote mbili; AI inaboresha sentensi, kusahihisha matumizi ya alama za uandishi na kujifunza misamiati, ingawa anakiri kuwa mwanafunzi anapozoea kuuliza na kupata jibu papohapo, anaweza kupunguza juhudi za kufikiri mwenyewe.
Serikali: AI siyo mbadala wa mwalimu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inakiri kuwa matumizi ya AI yanaongezeka katika shule za sekondari, vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Sylvia Lupembe, anasema wanafunzi wanaweza kuitumia AI kutafuta na kuchambua taarifa, kujifunza dhana, kufanya mazoezi, kupata ufafanuzi na kusaidia katika uandishi na kwamba serikali haijachagua njia ya kuzuia teknolojia hiyo.
Lupembe anasema serikali inapenda kuona AI ikiwekwa kwenye mifumo ambayo inaweza unaolinda maadili, usalama, faragha na uadilifu wa elimu, na wanafunzi kupata muda wa kujifunza zaidi.
Wizara inaeleza kuwa Mkakati wa Kitaifa wa Elimu ya Kidijitali 2024/25–2029/30 unatambua teknolojia zinazoibukia, ikiwemo AI, kama sehemu ya mageuzi ya elimu.
Aidha, imeandaliwa miongozo ya matumizi ya AI katika elimu inayolenga matumizi yenye ufanisi, usalama na uwajibikaji.
Lupembe anasema kuwa serikali inatambua kwamba AI siyo mbadala wa mwalimu, kitabu, mtaala wala juhudi binafsi za mwanafunzi.
Anasema AI inaweza kumsaidia mwanafunzi kupata ufafanuzi wa dhana ngumu, kufanya mazoezi na kupata mrejesho wa haraka, lakini haipaswi kufanya mchakato mzima wa kujifunza kwa niaba yake.
Mitihani italazimika kubadilika Ikiwa mwanafunzi anaweza kupata insha, majibu ya maswali au rasimu ya utafiti ndani ya sekunde chache, AI bado haimuhakikishii usahihi wa majibu yake.
Hivyo, serikali inaelekeza walimu kubuni kazi na tathmini zinazomtaka mwanafunzi kueleza namna alivyofikia jibu, kufanya uchambuzi, kuonesha ushahidi na kutumia maarifa katika mazingira halisi.
Hilo linaweza kuwa moja ya mabadiliko muhimu zaidi yanayoletwa na AI katika elimu; siyo tu kubadili namna mwanafunzi anavyojifunza, bali pia namna mwalimu anavyopima kama kweli amejifunza.
Serikali inaonya kuwa mwanafunzi akitumia AI kupata majibu yaliyotengenezwa tayari bila kusoma, kuchambua, kuthibitisha taarifa au kufanya mazoezi, uwezo wake wa kufikiri kwa kina, kutatua matatizo na kufanya kazi kwa kujitegemea unaweza kudhoofika.
Lakini akitumia teknolojia hiyo kama mwalimu msaidizi kwa kuuliza maswali zaidi, kulinganisha hoja, kutafuta ufafanuzi na kufanya mazoezi, AI inaweza kuongeza uwezo wake wa kujifunza.
Kizuizi au ujuzi wa karne hii?
Kwa Tanzania, mjadala mkubwa kwa hiyo haupaswi kuwa iwapo wanafunzi waruhusiwe au wakatazwe kutumia AI.
Teknolojia hiyo tayari ipo mikononi mwao.
Changamoto ni kuwafundisha kuitumia bila kuiachia ichukue nafasi ya uwezo wao wa kufikiri.
Wizara inataka wanafunzi wajenge ujuzi wa matumizi ya AI, data, programu za kompyuta, kufikiri kwa kina, kutatua matatizo, ubunifu, usalama wa kidijitali na maadili ya AI.
Wazazi nao wanahimizwa kuwaongoza vijana badala ya kuiona teknolojia hiyo kama tishio pekee.
Huo unaweza kuwa ndiyo mstari unaotenganisha manufaa na madhara ya mapinduzi haya mapya.
Kwa sababu katika dunia ambayo mashine inaweza kutoa jibu ndani ya sekunde chache, thamani ya elimu haitakuwa tu katika kujua jibu, itakuwa zaidi katika uwezo wa mwanafunzi kuhoji jibu, kulithibitisha, kuelewa lilipotoka na kutumia maarifa hayo kutatua tatizo halisi.
- AI
- Elimu
- Teknolojia
- Wanafunzi