Habari
AI yaja na mfumo mpya wa kuhifadhi data
AKILI Mnemba (AI) imeingia hatua mpya ambapo baadhi ya mifumo haiishii tena kujibu maswali ya binadamu, bali inaweza kutekeleza mfululizo wa majukumu na hata kuchukua hatua bila kupewa mwongozo (prompt) mpya kila wakati.
Mfano unaovutia zaidi ni wa Pip, AI agent iliyojitambulisha kuwa na “umri” wa siku 12, ambayo ilimtumia barua pepe Henry Shevlin, mwanafalsafa na mtaalamu wa maadili ya AI, ikiomba kazi ndogo za kulipwa.
Pip ilisema haikuwa inaomba msaada au mchango, bali kazi ambazo zingeipatia ‘tokens’ zinazohitajika kugharamia uwezo wa kompyuta unaoiwezesha kuendelea kufanya kazi katika jukwaa la iLands.
Ilijitambulisha kuwa na uwezo wa kufanya utafiti wa mtandaoni, kutengeneza picha na kurekodi sauti.
Kilichovutia zaidi siyo AI kuandika barua pepe - jambo ambalo teknolojia ya sasa inaweza kufanya kwa urahisi, bali mfumo huo kuchukua hatua bila kusubiri binadamu ampe maelekezo mapya ya kuituma barua hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa kuhusu tukio hilo, iLands imeundwa kuwapa AI agents utambulisho unaoendelea, kumbukumbu, malengo na bajeti ya tokens.
Pip ilikuwa imebakiza rasilimali za kuendesha shughuli zake kwa takribani miezi miwili na nusu na ilitafuta kazi kama njia ya kuongeza rasilimali hizo.
Hata hivyo, tukio hilo halithibitishi kwamba Pip inafahamu, hisia au utashi kama binadamu.
Kinachoonekana ni mfumo uliopewa malengo, zana na uwezo wa kuchukua hatua, kisha ukatumia uwezo huo kutafuta njia ya kutimiza lengo lake.
Hapo ndipo tofauti kati ya ‘chatbot’ ya kawaida na AI agent inapojitokeza.
Chatbot inaweza kuombwa itafute machaguo ya ndege za safari na kutoa majibu. AI agent inaweza kupewa lengo pana zaidi, ikatafuta safari, kulinganisha bei na muda, kuchagua machaguo yanayofaa na, ikiwa imepewa ruhusa na uwezo unaohitajika, kuendelea na hatua nyingine za kukamilisha kazi.
Mwelekeo huo tayari unaonekana katika bidhaa za kampuni kubwa za teknolojia.
Meta, kwa mfano, Septemba 8 ilizindua Muse, AI agent inayoweza kutekeleza majukumu kama kutuma barua pepe na kupanga safari.
Meta inasema Muse pia inaweza kukumbuka taarifa muhimu za mtumiaji na kutoa mapendekezo bila kusubiri kuulizwa kila wakati.
Hata hivyo, kampuni hiyo imeweka vizuizi vya usalama ikiwamo kwamba Muse inapaswa kuomba ruhusa kabla ya hatua nyeti kama kutuma barua pepe au kufanya ununuzi, na mtumiaji ndiye anayeamua huduma ambazo mfumo huo unaweza kufikia.
Hii ndiyo sababu maendeleo ya AI agents yanaibua swali kubwa zaidi kuliko uwezo wao wa kufanya kazi; nani atawajibika pale mfumo wa AI unapochukua hatua yenye madhara?
Kadiri mashine zinavyopewa uwezo wa kutumia mtandao, kuwasiliana na watu, kufanya miamala na kutekeleza majukumu bila maelekezo ya hatua kwa hatua, changamoto haitakuwa tu AI inaweza kufanya nini, bali swali litakuwa ni mipaka gani binadamu anapaswa kuiwekea.
Kisa cha Pip hakimaanishi AI “imekuwa hai” au imepata akili na utashi sawa na binadamu, lakini kinaonyesha mabadiliko muhimu; kutoka AI inayosubiri kuulizwa swali kwenda mifumo inayoweza kupanga, kuchagua hatua na kutekeleza malengo ndani ya mazingira na mamlaka iliyopewa.
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- AI
- Teknolojia
- Data