Jicho la Tai
Bodaboda acheni fujo, epusheni vifo
KUNA wakati ukiwa barabarani Dar es Salaam unaweza kujiuliza kama kweli tunatumia barabara moja au kila mtu ana sheria yake.
Ukiwa nyuma ya usukani wa gari, unawasha taa ya kuashiria kupinda kona, unapunguza mwendo na kusubiri nafasi salama, lakini ukitazama upande mmoja, bodaboda anapita katikati ya magari kana kwamba amepewa barabara hiyo na babu yake!
Bodaboda wamekuwa sehemu muhimu ya usafiri katika miji mikubwa, wanawasaidia wananchi kufika kazini, sokoni, hospitalini na maeneo mbalimbali kwa haraka, hasa wakati foleni inapokuwa imekaa barabarani kama mkutano wa dharura, hili halina ubishi.
Tatizo linaanza pale baadhi yao wanapoamini kwamba kazi ya bodaboda inawapa pia leseni ya kuvunja kila sheria.
Taa nyekundu za barabarani zinaonekana, magari yanasimama, lakini bodaboda anaendelea, tena hawajali na wanaona wako juu ya sheria.
Yaani alama za kuzuia kupinda zinaonekana, lakini madereva wa bodaboda wanaamua kuwa alama hizo zilikuwa zinashauri tu na kuruhusu waendelee kwa fujo zao.
Inashangaza kuona kwamba askari wa usalama barabarani yupo mbele, lakini badala ya kupunguza mwendo, dereva wa bodaboda anapita kwa kujiamini kana kwamba askari huyo ni mpita njia.
Na hapo ndipo tunapofika kwenye swali la msingi; barabara hizi zina sheria au zina mapendekezo?
Baadhi ya waendesha bodaboda wamekuwa wakibadilisha njia bila tahadhari, kupita kwenye nafasi finyu kati ya magari, kupakiza abiria zaidi ya uwezo salama na kuendesha kwa mwendo usiozingatia mazingira.
Wengine huendesha bila vifaa muhimu vya usalama – ikiwamo kofia ngumu (helmet) huku abiria nao wakati mwingine wakikubali safari bila kuuliza hata kama kuna kofia ya usalama.
Matokeo yake ni ajali, majeraha, ulemavu na vifo. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba ajali nyingi zinaweza kuzuilika iwapo sheria zingezingatiwa na kufuatwa.
Hatutaki kusema kila mwendesha bodaboda ni mhalifu wa barabarani, wapo wengi wanaoheshimu sheria, wanavaa kofia, wanaendesha kwa uangalifu na kuwaheshimu watumiaji wengine wa barabara, lakini tabia za wachache zimeanza kuwapa taswira mbaya hata wale wanaofuata taratibu.
Serikali, kupitia vyombo vinavyosimamia usalama barabarani, inapaswa kukazia utekelezaji wa sheria bila upendeleo. Sheria inapovunjwa, hatua stahiki zichukuliwe.
Suala la ukaguzi wa leseni, vifaa vya usalama, hali ya pikipiki na mwenendo wa dereva unapaswa kuwa sehemu ya utekelezaji wa kawaida, siyo zoezi linalofanyika baada ya ajali kutokea.
Lakini jukumu hili siyo la serikali pekee, waendesha bodaboda wanapaswa kuelewa kwamba maisha ya abiria yako mikononi mwao.
Abiria naye ana haki ya kukataa kupanda pikipiki ambayo dereva wake anaonekana kutokuwa tayari kuendesha kwa usalama.
Ieleweke kuwa barabara siyo mashindano ya nani atafika kwanza, wala siyo eneo la kuonyesha ujasiri wa kupita taa nyekundu mbele ya askari.
Ni wakati sasa kwa bodaboda kuheshimu sheria, askari na watumiaji wengine wa barabara. Maana mwisho wa safari siyo muhimu kuliko kufika salama.
Sheria za barabarani hazikuwekwa kumkomoa mtu, ziliwekwa kulinda maisha, na maisha ya Mtanzania mmoja yanapaswa kuwa na thamani kuliko dakika chache tunazotaka kuokoa barabarani.
- Bodaboda
- Usalama Barabarani
- Dar es Salaam