Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Tahariri

Ukarabati wa barabara Dar uharakishwe

UJENZI na ukarabati wa barabara unaoendelea katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam ni uwekezaji muhimu kwa mustakabali wa maisha ya wananchi.

Jumatatu, 17 Agosti 2026 · 03:15Dakika 2 kusomaToleo 178, uk. 2

Barabara nzuri hupunguza gharama za usafiri, huharakisha biashara, huunganisha jamii na kurahisisha utoaji wa huduma. Zikijengwa kwa kiwango kinachostahili, zinaweza kupitika mwaka mzima bila kujali vipindi vya mvua.

Hata hivyo, faida hizo hazipaswi kutufanya tufumbe macho mbele ya madhara yanayosababishwa na miradi inayochukua muda mrefu kuliko ilivyopangwa.

Barabara inapochimbwa na kuachwa kwa miezi mingi, haiwi tena mradi wa maendeleo pekee; hugeuka kikwazo cha ustawi wa wananchi na serikali yenyewe.

Katika maeneo yenye ujenzi, wananchi hutumia muda mrefu barabarani, magari huharibika, mafuta hutumika kupita kiasi na nauli huongezeka.

Wafanyakazi hufika kazini wakiwa wamechelewa na kuchoka. Wanafunzi hukosa vipindi, wagonjwa huchelewa kufikishwa hospitalini, huku wafanyabiashara wakipoteza wateja kwa sababu maduka yao hayafikiki kwa urahisi.

Mfanyabiashara mdogo anayefungua duka kando ya barabara hawezi kuambiwa asubiri maendeleo bila kujulikana yatafika lini. Ana kodi ya pango, mishahara, leseni na familia inayomtegemea.

Vumbi likifunika bidhaa, mitaro ikaziba njia na mashine zikazuia wateja, mapato yake huporomoka. Huo ni uchumi wa kaya unaoumia kwa jina la mradi unaopaswa kuuimarisha.

Serikali pia hulipa gharama ya ucheleweshaji huo. Msongamano hupunguza uzalishaji, huongeza matumizi, huathiri ukusanyaji wa mapato na kuongeza gharama za usimamizi.

Miradi inayoongezewa muda inaweza kuhitaji fedha zaidi kutokana na kupanda kwa bei za vifaa, mabadiliko ya usanifu au kurekebisha sehemu zilizoharibika kabla hata mradi haujakamilika.

Jiji lenye watu milioni kadhaa haliwezi kuendeshwa kana kwamba muda wa wananchi hauna thamani. Kila saa inayopotea kwenye foleni ina gharama kwa uchumi, afya, familia na maisha ya wakazi wa Dar es Salaam na wageni.

Pambazuko halipingani na ujenzi wa barabara. Tunatambua kuwa ujenzi wenye ubora unahitaji muda, fedha, utaalamu na umakini, lakini muda huo lazima uwe wa kazi inayoonekana, siyo wa mitambo iliyopaki, maeneo yaliyochimbwa na kalenda inayosonga bila maelezo kwa wananchi.

Makandarasi wanapaswa kutekeleza mikataba kwa weledi, kuwa na vifaa na wafanyakazi wa kutosha, kupanga kazi kwa zamu inapowezekana na kutengeneza njia mbadala salama.

Nayo serikali kwa upande wake, ihakikishe malipo ya wajenzi yanafanyika kwa wakati, huduma kama maji na umeme zinahamishwa mapema, na usimamizi wa kila siku unaimarishwa.

Pale mkandarasi anaposhindwa bila sababu ya msingi, masharti ya mkataba yatumike.

Pale taasisi ya serikali inapochelewesha uamuzi au fedha, nayo iwajibike.

Hakika siyo haki lawama zote kumwangukia mkandarasi ikiwa chanzo ni urasimu; wala siyo busara serikali kumkingia kifua mkandarasi asiye na uwezo.

Wananchi pia wanastahili taarifa za wazi kuhusu muda wa kuanza, hatua iliyofikiwa, sababu za kuchelewa na tarehe mpya ya kukamilisha mradi. Uwazi hupunguza uvumi na kuwasaidia watu kupanga shughuli zao.

Tunaihimiza serikali na makandarasi kufanya haraka kukamilisha miradi hii ya kimkakati bila kuvuruga ubora wake.

Barabara bora iliyokamilika kwa wakati ni maendeleo, lakini barabara inayojengwa bila mwisho ni jeraha linalotafuna biashara, muda, mapato na matumaini ya wananchi.

  • Barabara
  • Dar es Salaam
  • Miundombinu

Soma Pia