Habari
NSSF ipo tayari kufufua Mradi wa Dege
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, akizungumza na wahariri alipokutana nao jijini Dar es Salaam kuelezea mafanikio ya mfuko huo. — Picha na Hughes Dugilo MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umezidi kuimarisha nafasi yake kama nguzo kuu ya kiuchumi na maendeleo ya kijamii nchini Tanzania.
Katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2025/26, mfuko huo umeshuhudia ukuaji wa thamani ya vitega uchumi vyake ukitoka Shilingi trilioni 4.62 hadi kufikia trilioni 9.60.
Mafanikio haya yanayodhihirisha uwezo wa NSSF katika usimamizi madhubuti wa fedha za wanachama na uelekezo wa rasilimali katika miradi yenye tija zaidi yalielezwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba alipokutana na wahariri jijini Dar es Salaam.
Mradi wa Dege Eco Village Akijibu swali la mmoja wa wahariri aliyetaka kujua kuhusu maendeleo ya Mradi wa Dege Eco Village, Mushimba alisema mradi huo bado unapitiwa na taasisi nyingine za serikali, hasa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Lakini alisema hatua hiyo inakaribua kufikia mwishoni na wakato wowote uamuzi wa mwisho kuhusiana na mradi huo utatolewa.
Alipouliwa iwapo NSSF itakuwa tayari kuuchukua tena mradi huo na kuuendeleza, Mshomba alisema hilo linawezekana, lakini italazimu kufanya mabadiliko makubwa kuhusu uendeshaji wa mradi huo, kwani uchunguzi wa awali ulionyesha matatizo makubwa kwenye mpango wa awali.
Dege Eco Village ni mradi mkubwa wa nyumba za makazi na biashara uliopo eneo la Kigamboni, Dar es Salaam.
Mradi huo ambao kwa miaka kadhaa ulikabiliwa na changamoto mbalimbali na kusimama, uliwekwa katika mkakati maalum wa uamuzi wa kiutawala na kisera ili kulinda maslahi ya mfuko na fedha za wanachama.
Mshomba alisema kuwa baada ya tathmini za kina za kisheria na kiuchumi, mfuko ulifanya uamuzi wa kimkakati wa kuachana na uendeshaji wa moja kwa moja wa mradi huo na kuanza mchakato wa kuuuza kwa wazabuni binafsi.
“Lengo kuu la hatua hiyo lilikuwa ni kuondoa athari za kiundani za kifedha na kuwekeza rasilimali hizo kwenye miradi yenye mzunguko wa haraka na tija ya kiuchumi,” alisema.
Alibainisha kuwa kupitia uamuzi huo wa kisheria na kibiashara, NSSF imefanikiwa kuondoa mzigo wa miradi iliyokwama na kuelekeza nguvu zake kwenye maeneo yenye usalama zaidi wa mtaji na faida endelevu kwa wastaafu.
Miradi iliyokuwa imesimama Mbali na Dege Eco Village, Mshomba alisema NSSF ilichukua hatua madhubuti za kufanya ukaguzi maalum na kurejesha utekelezaji wa miradi mingine ya nyumba na majengo ya biashara iliyokuwa imesimama.
Mathalan, mwaka 2023, mfuko ulirejelea rasmi ujenzi na ukamilishaji wa nyumba za makazi katika maeneo ya Dungu, Toangoma, na Mtoni Kijichi, pamoja na jengo la kibiashara la Mzizima.
“Miradi hii ya majengo na makazi ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji na inatarajiwa kukamilika kikamilifu kati ya Desemba 2026 na Machi 2027,” alisema.
Ukamilifu wa miradi hii siyo tu kwamba utaongeza thamani ya mali za mfuko, bali pia utasaidia kupunguza changamoto ya makazi bora na nafasi za kibiashara katika Jiji la Dar es Salaam.
Mafanikio ya Sukari Mkulazi Mshomba aliwaambia wahariri kuwa katika sekta ya viwanda na uzalishaji, NSSF imepiga hatua kubwa kupitia uwekezaji wake katika Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi.
“Mradi huu wa kimkakati umedhihirisha tija kubwa kifedha na kiuchumi kwa kusaidia kupunguza pengo la uhaba wa sukari nchini,”.
alisema.
Akifafanua, Mushomba alibainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26 pekee, Kiwanda cha Mkulazi kilifanikiwa kuzalisha tani 45,594 za sukari ya majumbani, hatua iliyokiiwezesha kuingiza mapato ya Shilingi bilioni 107.90 na kupata faida ya Shilingi bilioni 4.56.
Alisema mafanikio haya yanathibitisha ufanisi wa mikakati ya mfuko katika kuwekeza kwenye miradi inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi na uchumi wa taifa.
Mfuko unakua Kwa mujibu wa Mshomba, ukuaji wa makusanyo ya michango ya NSSF kutoka Shilingi trilioni 1.17 mwaka 2020/21 hadi trilioni 2.90 mwaka 2025/26 umechangiwa pia na ushirikishwaji wa mfuko katika miradi mikubwa ya kitaifa.
Miradi ya kimkakati kama vile ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP), Reli ya Mwendo Kasi (SGR), Mgodi wa Dhahabu wa Nyanzaga, Kiwanda cha Mbolea cha Intracom, na Kituo cha Biashara cha Ubungo (EACLC) imekuwa chanzo kikuu cha ajira rasmi na zisizo rasmi.
“Utekelezaji wa miradi hii umeongeza idadi ya wafanyakazi na wawekezaji wanaochangia NSSF, ambapo wanachama wapya 1,486,930 wameandikishwa na kufikisha jumla ya wanachama wachangiaji 2,144,906 kufikia Juni 2026,” alisema.
Sekta isiyo rasmi na Dira Ili kupanua wigo wa uwekezaji wa kijamii, Mushiomba alisema NSSF ilizindua Skimu ya Hifadhi Februari 2026 maalum kwa ajili ya wananchi waliojiajiri katika sekta isiyo rasmi kama vile wakulima, wavuvi, waendesha bodaboda, na mamalishe.
“Mpaka kufikia Juni 2026, zaidi ya wanachama 592,791 walikuwa wameshajisajili,” alisema.
Kupitia Mpango Mkakati wa Nane (2026– 2031) unaoenda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, NSSF inalenga kuendelea kuwekeza kwa umakini na usalama wa hali ya juu, huku ikilenga kuongeza thamani ya Mfuko kufikia Shilingi trilioni 24.75 na kuvutia wanachama wapya milioni 5.8 ifikapo mwaka 2031.
Usimamizi huu wa miradi unaonyesha dhamira ya Mfuko ya kuendelea kuwa nguzo imara ya hifadhi ya jamii na maendeleo ya taifa.
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- NSSF
- Mradi wa Dege
- Uwekezaji
- Dar es Salaam