Tahariri
Usafi usisubiri filimbi ya Rais Samia
KAULI ya Rais Samia Suluhu Hassan kukemea uchafu uliokithiri katika miji yetu, hasa Dar es Salaam, inapaswa kuwatafakarisha kwa kina viongozi na watendaji wa serikali katika ngazi zote.
Septemba 2, 2026, Rais Samia aliwataka wakuu wa mikoa kusimamia usafi na kuondoa wakandarasi wasio na uwezo wa kufanya kazi za umma kwa ufanisi na ubora.
Hata hivyo, pamoja na karipio, lakini swali kubwa linabaki; kwa nini lazima Rais Samia aseme ndipo viongozi walioajiriwa kwa kazi hiyo waamke na kuanza kukimbizana, ina maana hawaoni uchafu kwenye maeneo yao?
Tuna wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, maofisa afya, watendaji wa kata, mitaa, vitongoji na vijiji. Wote wana mamlaka, ofisi, bajeti na mishahara, hata hivyo, ni kama hawafanyi kazi.
Inashangaza wanaona kabisa kwamba taka zinaziba mifereji, masoko yananuka, mitaro inageuka dampo na maeneo ya makazi yanazungukwa na uchafu, lakini hawa wakubwa wetu wanaendelea kukaa ofisini wakiburudishwa na viyoyozi kana kwamba tatizo hilo linamhusu Rais Samia pekee.
Hali hii ni aibu. Rais hawezi kuwa afisa usafi wa kila mtaa. Hawezi kutoka Ikulu kwenda kukagua pipa la taka, mfereji uliozibwa au jalala lililoachwa katikati ya soko, haya ni majukumu ya wengine.
Viongozi wa maeneo yao wanaposubiri “maagizo kutoka juu” ndipo wachukue hatua, basi umma unapaswa kujiuliza uwezo wao wa kuona, kupanga na kuwajibika unaanzia wapi na kuishia wapi?
Uchafu siyo dosari ya sura ya mji pekee. Ni tishio kwa afya, mazingira, biashara na heshima ya taifa. Mifereji iliyozibwa huongeza mafuriko.
Taka zinazooza huvutia nzi na wadudu, huku maji machafu yakichochea magonjwa.
Pambazuko linatambua kwamba serikali hutumia fedha nyingi kutibu matatizo ambayo yangeweza kuzuiwa kwa usimamizi wa kawaida, ratiba thabiti ya ukusanyaji taka na utekelezaji wa sheria bila upendeleo.
Sisi tunawataka viongozi hawa watoke kwenye viti vyao. Watembelee masoko, stendi, mitaa na maeneo ya kutupia taka. Wakague mikataba ya wakandarasi, wafuatilie magari ya taka na waeleze wananchi mapato ya ada za usafi yanavyotumika.
Mkandarasi asiye na vifaa aondolewe; mtendaji anayefumbia macho uchafu awajibishwe. Urafiki, undugu au maslahi ya kisiasa yasiwekwe mbele ya afya ya wananchi.
Ieleweke kuwa uongozi wa eneo maana yake ni kugundua tatizo kabla halijafika Ikulu. Kila halmashauri iweke ramani ya maeneo hatarishi, ratiba zinazoonekana hadharani na namba za kupokea malalamiko.
Wakuu wa mikoa na wilaya wapimwe kwa matokeo, siyo hotuba. Vikao vya usafi visiishie kwenye makabrasha; vitoe majina ya waliowajibika, hatua zilizochukuliwa na muda wa kurekebisha kasoro. Bila hivyo, uzembe utaendelea kulindwa na ukimya wa ofisi zetu kila siku.
Wananchi nao wana wajibu wa kutotupa taka ovyo, kulipa ada halali na kutoa taarifa wanapoona uzembe, lakini huwezi kumlaumu mwananchi pekee wakati taka hazikusanywi, mapipa hayapo na mifereji haisafishwi. Uwajibikaji lazima uanze kwa wenye mamlaka.
Rais Samia amepiga filimbi na sasa hatutarajii kuona usafi wa siku mbili kwa ajili ya kamera, kisha uchafu urudi baada ya “vumbi kupoa,” tunataka mifumo ya kudumu, malengo yanayopimika na taarifa za wazi kwa umma.
Kiongozi anayeshindwa kutatua hata tatizo linaloonekana, atatuaminisha vipi kwamba anaweza kusimamia maendeleo makubwa? Kama kazi yake ni kusubiri mshahara na agizo la Ikulu, basi hana sababu ya kuendelea kushikilia ofisi ya umma. Aondolewe.
- Usafi
- Samia Suluhu Hassan
- Utawala bora
- Dar es Salaam