Mitindo & Urembo
Celine Dion ndani ya gauni la kifahari la ‘Haute Couture’
MWANAMUZIKI maarufu duniani, Celine Dion, amerudi kwa kishindo jukwaani baada ya kuugua kwa muda mrefu na kutingisha ulimwengu wa mitindo kwa kuvalia mfululizo magauni ya kifahari ya mtindo wa Haute Couture.
Mtindo wa Haute Couture ni ubunifu wa mavazi duniani, ambapo kila gauni hushonwa kwa mkono mahsusi kwa ajili ya mteja mmoja huku kitambaa chake ikiwa ni ya gharama kubwa zaidi na ushonaji wake huchukua zaidi ya saa 100.
Septemba 12, 2026, Celine akiwa katika onesho lake nchini Ufaransa katika ukumbi wa Plenitude Arena nje kidogo ya Jiji la Paris, aligeuza jukwaa hilo kuwa onyesho la mavazi ya kihistoria.
Mwanamama huyo ambaye anatarajiwa kuwa na ‘show’ 26 barani Ulaya hadi Mei 2027, alitokelezea akiwa amevaa gauni jeusi lililotengenezwa maalum na mkurugenzi wa ubunifu wa chapa ya Dior, Maria Grazia Chiuri.
Gauni hilo lina sehemu ya juu iliyobana bila kamba na sketi yenye marinda ya kipekee yaliyopangana kwa muundo wa petali za maua.
Muundo wa sketi hiyo umeongozwa na gauni la kihistoria la Christian Dior la mwaka 1950, imesukwa kwa kutumia vitambaa vyeusi laini vilivyopangwa kwa safu nyingi kupata umbo nene na la kishua.
Celine alikamilisha muonekano huo kwa mkufu wa kito cha almasi kutoka nyumba ya kifahari ya Boucheron “The Address”.
Mkufu huo ulitengenezwa kwa saa 1,107 na una almasi kubwa ya carats 10.01 katikati.
Mwanamuziki huyo pia alibadilisha mavazi kutoka kwa wabunifu wengine wakubwa duniani kama Schiaparelli, Alaïa, Givenchy na Tom Ford.
- Mitindo
- Celine Dion
- Haute Couture
- Urembo