Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Kona ya Dkt. Bisimba

Demokrasia ina maana gani kwa Watanzania?

KESHO Septemba 15 dunia itaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Demokrasia kama ilivyopitishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2007.

Jumatatu, 14 Septemba 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 182, uk. 11

Siku hii huadhimishwa kila mwaka, lakini kuna maswali mengi kuhusu manufaa ya kuiweka siku hii.

Je, imetusaidia kujenga taifa kidemokrasia? Tujiulize iwapo demokrasia ni ya wananchi ni kwa kiwango gani wananchi wenyewe wanashiriki katika kuijenga, kuilinda na kuidai?

Hivi tunatafakari tunachotaka ndani ya maisha ya kila siku ya Mtanzania yatokanayo na demokrasia?

Unaweza kuyajibu maswali haya kwa kuangalia hali halisi ya Tanzania kwa kutumia matukio mbalimbali likiwemo majeraha yaliyotokana na Uchanguzi Mkuu wa mwaka 2025. Majeraha ambayo hayajatibiwa na kupona.

Taarifa na tuhuma nzito kuhusu yaliyotokea katika uchaguzi ule zikiwemo vurugu, vifo na hata vizuizi kwa baadhi ya vyama vya siasa kushiriki uchaguzi ni masuala yaliyo katika mijadala hadi sasa.

Taarifa iliyotolewa na Shirika la Human Rights Watch inabainisha kuwa vurugu za kipindi cha uchaguzi huo zilisababisha vifo vya watu wengi na Tume iliyoundwa na Rais kuchunguza vurugu hizo ilitoa taarifa kuwa vilitokea vifo 518 katika mikoa 11 nchini.

Tunapoadhimisha Siku ya Demokrasia Duniani hatuwezi kabisa kuacha kuyaangalia mambo haya yaliyotokea katika tukio muhimu la kidemokrasia.

Tusidhani masuala haya yanaweza kufunikwa na tuweze kuendelea kama vile hayakutokea au yalikuwa ni ndoto tú.

Maswali yote haya yanadhihirika tukiangalia mijadala iliyoendelea wiki zilizopita mmoja ukiongozwa na Chama cha Mawakili Tanganyika na ule wa Jukwaa la Demokrasia Tanzania (TCD).

Mijadala hiyo inatulelekeza kwenye mazungumzo, mageuzi ya kisiasa na umuhimu wa kuimarisha taasisi za kidemokrasia, kama njia ya kutibu majeraha hayo.

Tumesikia sauti za wadau wakiwemo watu wanaoheshimika sana nchini wakihimiza kuondokana na lawama na kutafuta njia mahsusi za kuzuia hali iliyotokea mwaka uliopita.

Lakini hata katika midahalo hiyo bado kuna ombwe kwa vile suala zima la demokrasia tuitakayo halijaonekana kwa uwazi.

Siku moja ya kupiga kura na baada ya hapo wananchi wanabaki kuwa watazamaji kwa miaka mitano baadaye hiyo haiwezi kusemekana kuwa ni demokrasia.

Ukweli wa demokrasia ni pale kunapokuwepo na uhuru wa kutoa maoni, uhuru wakujumuika, uwezo wakuandaa mikutano na hata maandamano ya amani, uhuru wa vyombo vya habari na asasi za kiraia kuhoji na kufuatilia masuala ya kisera na hata kisheria huku zikiwakumbusha wenye mamlaka wajibu wao bila hofu yoyote.

Demokrasia itoe nafasi ya kutokukubaliana.

Mpinzani kisiasa asionekane adui, mwanaharakati asipewe jina baya, mwananchi muuliza maswali asionekane mkosaji.

Ujenzi wa demokrasia ni pamoja na ujenzi wa taasisi za kuilinda hiyo demokrasia. Katika siku hii mjadala wa kijasiri upite kuhusu uhuru na uadilifu wa taasisi za uchaguzi, nafasi ya Katiba na ukuu wake, uhuru wa Mahakama, nguvu ya Bunge katika kuisimamia serikali, mazingira ya ushiriki wa wananchi katika masuala yanayowahusu bila hofu.

Inabidi katika haya maadhimisho tafakari ya kina ifanyike kuangalia kama yapo tunayofanya vizuri, tuone tumekosea wapi na tuangalie umuhimu na utayari wa kujifunza kutokana na yaliyotokea.

Demokrasia isiwe ni kwa ajili ya kushinda chaguzi tu bali ihusu ujenzi wa taifa ambapo kila mwananchi ataweza kujiona ni sehemu ya taifa hili, hapo tutakuwa tunaiendea demokrasia ya kweli.

Mwandishi wa safu hii ya kila wiki, ni mwanaharakati wa demokrasia, haki za binadamu na mwanazuoni wa falsafa ya sheria.

  • Demokrasia
  • Haki za binadamu

Soma Pia