Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Kona ya Dkt. Bisimba

Maswali mengi kujiuzulu Nchimbi, kuvuliwa uanachama

KATIKA siasa kuna matukio mengi ambayo ni vigumu kuyatabiri. Tukio moja huweza kutokea na maswali yakijitokeza jibu lake likawa rahisi.

Jumatatu, 31 Agosti 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 180, uk. 11
Dkt. Emmanuel Nchimbi
Dkt. Emmanuel Nchimbi — Kutoka Maktaba ya Pambazuko.

Lakini wakati mwingine tukio hilo hilo likaweza kuzaa maswali ambayo majibu yake ni vigumu kupatikana.

Kujiuzulu kwa aliyekuwa Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi, kumeibua maswali mengi ambayo majibu yake ni vigumu kuyapata haraka.

Jumane ya Agosti 25, 2026 ambayo ilikuwa sikukuu ya Maulid, Watanzania tulipokea taarifa kwamba Dkt. Nchimbi amejiuzulu nafasi ya Makamu wa Rais na ameamua kustaafu siasa na utumishi wa umma, kuanzia Septemba 4, 2026 ambazo ni siku kama kumi baada ya taarifa.

Katika taarifa yake, alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuridhika kwamba Rais Samia Suluhu Hassan anatamani mabadiliko katika nafasi hiyo. Mara Rais naye akatangaza kukubali kujiuzulu kwake.

Lakini kabla Watanzania hawajapata muda wa kutafakari maana ya kujiuzulu huko, likatokea jambo jingine kubwa zaidi; yaani, chama chake CCM kikaitisha vikao na kumfukuza Dkt. Nchimbi uanachama.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Asha-Rose Migiro, vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu vilijadili suala la nidhamu na maadili na kubaini kuwa Katiba, Kanuni na taratibu za chama zilikuwa zimekiukwa.

Hata hivyo, maelezo ya kina kuhusu kosa hilo hayajawekwa wazi kwa umma. Hapa ndipo ninapojiuliza; kulikoni?

Ikiwa Dkt. Nchimbi aliamua kujiuzulu kwa sababu alitambua kuwa rais anataka mabadiliko, kwa nini ndani ya muda mfupi namna hiyo afukuzwe na chama chake?

Je, kujiuzulu kulikuwa uamuzi wake mwenyewe, au kulikuwa na jambo jingine nyuma yake ambalo Watanzania hatujaambiwa?

Na kama kulikuwa na suala la nidhamu na maadili, ni muhimu kwa umma kuelewa; ni kosa gani hasa lililofanyika? Siyo kwa nia ya kumhukumu Dkt. Nchimbi, bali kwa sababu alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyepitia katika uchaguzi mkuu na hadi akitangaza kujiuzulu alikuwa mmoja wa viongozi wakuu wa nchi.

Jambo jingine linalostahili kutafakariwa ni kasi ya matukio. Kujiuzulu kwa Makamu wa Rais, kufukuzwa kwake CCM na kupitishwa kwa jina la mrithi wake, aliyekuwa Waziri wa Nishati, Dkt. Deogratius Ndejembi, vimetokea kwa kasi kubwa sana.

CCM imempendekeza Ndejembi kwa nafasi hiyo na tayari ameapishwa rasmi juzi.

Kwa jicho la kawaida huoni kabisa hiyo kasi ilitokea kwa sababu zipi zaidi ya kudhani ilikuwepo katika mlolongo wa matukio kwa ndani na yalipojitokeza watazamaji ndiyo tunashangaa.

Hii haimaanishi kwamba tunakosoa uteuzi wa mrithi. Kasi ndiyo imezua swali la msingi liendelee kusikika; Je, haya yalikuwa yamepangwa tayari, au yalitokana na matukio yaliyotokea ghafla?

Dkt. Nchimbi aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM kabla ya kuwa mgombea mwenza wa Rais Samia katika uchaguzi wa 2025.

Amekaa katika nafasi ya Makamu wa Rais kwa siku 295 tu. Kwa hiyo, kuondoka kwake si jambo dogo.

Ni tukio linalostahili maelezo ya kutosha, hasa kwa kuwa limefuatiwa na hatua kali ya kufukuzwa chama.

Chama kilijua ana hatia za kimaadili kikasubiri atangaze kujiuzulu ndiyo kiamue kumfukuza au kujiuzulu ndilo kosa la kimaadili?

Ingefaa tukajua kulikoni. Katika demokrasia, siyo lazima wananchi waambiwe kila jambo la ndani ya hicho chama.

Mwandishi wa safu hii ya kila wiki, ni mwanaharakati wa demokrasia, haki za binadamu na mwanazuoni wa falsafa ya sheria.

  • Emmanuel Nchimbi
  • CCM
  • Demokrasia

Soma Pia