Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Kona ya Dkt. Bisimba

Tunaweza kuwa huru tukiogopa kuzungumza?

WIKI hii tuliadhimisha Siku ya Demokrasia Duniani na likawepo kongamano kubwa lililoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ambapo palikuwa na mjadala mzuri kuhusu suala la Katiba na tunachoweza kujifunza kutokana na uchaguzi wa mwaka 2025.

Jumatatu, 21 Septemba 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 183, uk. 11

Siku hiyo pia ilizinduliwa kanzidata ya Katiba ikiwa na Katiba za nchi nyingi ulimwenguni na machapisho mengi ya Katiba.

Mgeni rasmi aliyewahi kuwa Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu Afrika na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini, Bahame Tom Nyanduga, alitoa tafakari kubwa kuhusu nafasi ya demokrasia nchini akiangaliza misingi ya demokrasia kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Afrika wa Demokrasia.

Jopo lililochokoza mada hii lilijikita katika kuonyesha kuwa kabla ya kuzungumzia uwepo wa mchakato wa Katiba bora, ni vyema tukaangalia yaliyotusibu mwaka uliopita na kujua tunachojifunza ili tutafute kupona.

Masuala ya jinsia yaliongelewa pia kuonyesha kiasi ambacho inaonyesha tumerudi kinyumenyume. Nami nilipata fursa ya kuchangia kutokana na yaliyosemwa na wanajopo hao.

Baada ya mchango wangu kufika kwa jamii kupitia vyombo vya habari nilipokea simu na hata ujumbe mbalimbali.

Katika simu na ujumbe nilizopata ikanionyesha kuwa tupo katika kipindi ambacho tunahitaji sana kujitafakari kama taifa.

Katika waliowasiliana nami wapo walioniuliza iwapo nipo salama, na wapo walioniuliza iwapo siogopi na wengine walinishauri kuwa nisiwe nazungumzazungumza kama hivyo ni hatari.

Nikajiuliza, kwa nini hii jamii yetu inayopaswa kujenga demokrasia, kutoa mawazo uliyonayo yasiyomdhuru mtu, iwe jambo la kuogopesha?

Ninachofahamu mimi uhuru wa kujieleza siyo anasa bali ni kati ya misingi mikuu ya demokrasia.

Kama hatutaweza kuwa na uwezo wa kuuliza, kukosoa, kupendekeza na hata kutokukubaliana inapobidi, tunawezaje kuwa washiriki katika mambo yanayotugusa kama wananchi wa nchi hii.

Inatupasa kufahamu kuwa ipo tofauti kati ya hofu na uwajibikaji. Katika haki hii ya kujieleza mtu hasemi tu chochote. Haki hii hutumiwa bila kuingilia uhuru wa mtu mwingine na kikubwa ni kuwa na ukweli na si vinginevyo.

Inavyoonekana watu wanaonekana kutaka kujinyamazisha kabla hata hawajasema kwa kuogopa madhara yanayoweza kuwapata.

Hapa ndiyo tujihoji tuna uhuru wa kujieleza kweli au ni suala la maandishi tu? Inasikitisha kuwa kama taifa inaelekea tumefikia mahali ambapo mtu kusema ukweli kwa uwazi inakuwa ni jambo la kushangaza kuliko kukaa kimya kwa hofu.

Nimeona pia kauli ya vijana ya kuniita “Bibi Gen Z”, ilibidi nicheke na zaidi pia imenifikirisha.

Nimepokea ujumbe huo wa “Bibi Gen Z” kama zawadi yakuwagawia watanzania katika kipindi hiki tunachotafuta njia yakujikwamua katika hali iliyotufika.

Hata hivyo, nimeona kutoka kwa hawa vijana kuna ujumbe mzito kuliko utani. Hapa tuone kizazi cha zamani na kizani kipya vinavyoweza kukutana katika jambo moja lakutaka Tanzania ambayo watu wanaweza kuzungumza, kuhoji, kushiriki katika kujenga nchi yao bila kuishi kwa hofu.

Nisingependa kizazi kijacho kirithi ujasiri unaoonekana kwangu, bali ningetamani kirithi mazingira ambayo hakihitaji kuwa jasiri kupita kiasi ili kusema ukweli.

Ukweli usemwe kwa kuwa ni ukweli na upokewe bila tashwishwi. Kama tunataka kujenga demokrasia ya kweli tuijenge jamii ambayo haitatawaliwa na hofu.

Vilevile, tujenge utamaduni wa demokrasia ambao utawawezesha watanzania kuwa waaminifu, wenye uadilifu wakusema lile wanaloliamini na kuona linaweza kuisaidia nchi na watu waliomo nchini.

Mwandishi wa safu hii ya kila wiki, ni mwanaharakati wa demokrasia, haki za binadamu na mwanazuoni wa falsafa ya sheria.

  • Demokrasia
  • Uhuru wa Kujieleza
  • Haki za Binadamu

Soma Pia