Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Kona ya Dkt. Bisimba

Tanzania bado upo ujasiri wa kuuliza maswali?

KILA siku ninapoitazama nchi yetu na mambo yanayoibuka, ninawiwa kuuliza iwapo mimi na wenzangu wa nchi hii tumewahi kutulia na kujiuliza maswali.

Jumatatu, 7 Septemba 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 181, uk. 11

Nilipomsikiliza Askofu Benson Bagonza akieleza jinsi ambavyo inaelekea ukweli hautakiwi katika nchi hii na pia rushwa imekosa askari wa kuishughulikia, nikahisi kuwa sisi wenye nchi tumeshindwa kutekeleza wajibu wetu tukiwa raia.

Katika demokrasia matarajio yaliyopo ni kuuliza maswali magumu, kujiuliza binafsi, hatimaye kuwahoji wenye dhamana ya kuongoza nchi ili kupata majibu na njia sahihi ya kurekebisha yanayoonekana kwenda mrama.

Siyo lazima kupata majibu, lakini kwa raia la muhimu ni uwezo tulionao na ujasiri wa kuuliza maswali magumu.

Kama taifa linalojiamini na lenye raia wanaojiamini, maswali ni lazima yaulizwe na kujiuliza na hii ni njia mojawapo ya kutafuta ukweli ambao utatuwezesha kusonga mbele kama taifa.

Tunaendelea kushuhudia mabadiliko na matukio yakiendelea hasa kwenye uwanja wa siasa na kuibua minong’ono kutoka kwa wananchi wa hali na rika mbalimbali.

Wapo waliosema, kwa nini hayo yametokea na wengine, kwa nini wakati huu na kulikoni? Je kuna mambo yanayofichwa kama raia hatujaambiwa.

Ili mradi yanawazwa mengi, nikamsikia mtu mwingine akisema, hivi katika nchi hii bado mnataka kuuliza maswali? Kwani raia bado tuna nafasi ya kuuliza maswali magumu bila kuonekana kuwa tunapinga uongozi wa nchi? Hili swali si dogo.

Ibara ya 3 ya Katiba inaitaja Tanzania kama nchi ya kidemokrasia na demokrasia huwa haizuki tu bali inajengwa.

Ili kuijenga demokrasia haiwezekani watu wote kuwa na mawazo yanayofanana. Ujenzi wa demokrasia ya kweli hutokana na uwezo wa watu kuwa na mawazo yanayotofautiana, kuhoji, kujadili na ikibidi kuweza kukosoa bila hofu.

Serikali ikikosolewa haiachi kuwa serikali inabaki kuwa serikali na inapaswa kusikiliza. Hata vyama vya siasa vinaweza kuulizwa maswali na hata kukosolewa, hii haivibadilishi kuwa kitu kingine, navyo hubaki kuwa vyama vya siasa.

Inawezekana pia kiongozi akaulizwa swali kuhusu uamuzi alioufanya naye pia anapaswa kujibu na kutoa maelezo bila kudhani muuliza swali ana kisa naye.

Uzoefu wangu katika nchi hii, nimegundua mara nyingine, kama si mara nyingi, tunachanganya mambo haya; kukosoa na kuchukia, kuhoji na kupinga.

Hali kama hii inatupeleka katika kupoteza kitu muhimu sana katika demokrasia ambacho ni fursa ya mazungumzo.

Ikitokea raia akakutana na jambo asilolielewa anapaswa afanye nini? Je, ni sawa kunyamaza? Au inabidi aulize? Tukiwaangalia waandishi wa habari nao, wakikutana na jambo linalogusa maslahi ya umma, je waache kuuliza kwa kuwa wakiuliza huenda swali lao likamuudhi mtu mwenye mamlaka anayeulizwa?

Na kwa mtu kama mtetezi wa haki za binadamu, akiuangalia mfumo fulani unaoonekana kuweza kumdhuru mwananchi, je, wajibu wake ni kuwa kimya au kuinua sauti na kuuliza bila yeye kueleweka vibaya?

Ninavyoona mimi kuuliza inapobidi ni wajibu na si hiari. Nchi yetu haitaweza kujengwa kwa watu kuwa kimya kwa hofu ya kuuliza maswali.

Tufike mahali ambapo swali gumu liwe fursa na si tishio, mwananchi aweze kuuliza swali bila hofu, mwanahabari achunguze bila kutishiwa.

Mwishowe ijulikane wazi kuwa taifa kuulizwa maswali si udhaifu ni kujiamini. Kwa wiki hii tujiulize sote ‘Bado tuna ujasiri wa kuuliza maswali?’ Mwandishi wa safu hii ya kila wiki, ni mwanaharakati wa demokrasia, haki za binadamu na mwanazuoni wa falsafa ya sheria.

Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.

  • Demokrasia
  • Haki za binadamu
  • Uwajibikaji

Soma Pia

Tanzania bado upo ujasiri wa kuuliza maswali? | Pambazuko