Kimataifa
Dunia: Hapa na Pale
Japan yaruhusu kaptula ofisini kukabili joto, mafuriko yaua zaidi ya 633 Nepal na China, wahuni waendelea kumvuruga Rais William Ruto, na Jenerali Muhoozi aibua mzozo wa kifamilia Uganda.

Waamua kuvaa kaptula ofisini
WAFANYAKAZI nchini Japan wameanza kuvaa kaptula ofisini, ili kukabiliana na majira ya joto kali la kiangazi nchini humo.
Katika mji mkuu wa Japan, Tokyo, kampeni ya muda mrefu ya serikali ya jiji la Tokyo inayohimiza wafanyakazi kutovaa tai na makoti, imekosa nguvu na sasa wafanyakazi wanahimizwa kuacha kuvaa suruali ndefu na hata kujaribu kuvaa fulana na viatu vya michezo.
Kadiri joto linavyozidi kuikumba Ulaya, wafanyakazi wengine wameanza kuiga mfano wa Tokyo, wakati mwingine kwa kuungwa mkono na mamlaka za waajiri, na maeneo mengi wameanza kuunga mkono.
Maafa Nepal na China
MAAFA yanayotokana na mafuriko huko Nepal na China, yanatajwa kusababisha zaidi ya vifo vya watu 633 na wengine zaidi ya 3,000 kupotea, huku waokoaji wakiendelea kutafuta miili katika vijiji vinavyozunguka eneo la Himalaya mpakani wa nchi hiyo na Tibet.
Mafuriko hayo ya ghafla yameripotiwa kusomba vijiji baada ya mvua ambazo hazikutarajiwa. Kwa upande wa Tibet, watu saba wameripotiwa kufariki dunia na wengine 554 hawajulikani walipo.
Takwimu zinaeleza idadi ya waliopotea nchini Nepal inaendelea kuongezeka, baada ya mamlaka kuongeza wafanyakazi 933 wa miradi ya kuzalisha umeme kwa maji katika orodha hiyo.
Watalii, wafanyakazi wa kigeni na mahujaji waliokuwa wakielekea Mlima Kailash nchini Tibet pia ni miongoni mwa waliopotea.
Wahuni wazidi kumvuruga Ruto
RAIS William Ruto anaendelea kukabiliana na vizingiti kutoka kwa makundi ya wahuni wanaotaka kukwamisha kampeni yake ya kurejea madarakani katika uchaguzi mkuu mwakani, baada ya fujo zilizosababisha majeruhi kadhaa katika Kaunti ya Narok mwishoni mwa wiki.
Ghasia za kisiasa zilizoibuka kwa watu wenye mishale kuvamia katika kituo cha biashara cha Mamboleo kabla ya hafla ya rais kuanza, zilitia doa ziara yake, hali iliyomlazimu Ruto kuwakemea viongozi hasimu hadharani na kuwataka kumaliza tofauti zao za kisiasa mara moja.
Mapigano hayo yalihusisha wafuasi wa Mbunge wa Emurua Dikirr, David Keter na mpinzani wake wa kisiasa Bernard Ng'eno ambao walikabiliana kwa kutumia silaha kali ikiwemo mishale.
Muhoozi avuruga mashemeji
MKUU wa majeshi ya Uganda, Jenerali Kainerugaba Muhoozi, ameibua mzozo wa kifamilia baada ya kumkashifu hadharani shemeji yake, Drek Rwabwogo, ambaye ni mume wa askofu Patience Museveni Rwabogo.
Katika mzozo huo ambao umetokea hadharani, Jenerali Muhoozi alitishia kimkamata shemeji yake huyo, huku akisema kwamba atazungumza na dada zake wawili, Patience na Natasha kutatua mzozo uliopo.
Jenerali Muhoozi ambaye pia ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni aliandika katika mtandao wa X, akizungumza kwa ukali kuhusu shimeji yake huyo ambaye pia ni mshauri mwandamizi wa Rais Museveni na mwenyekiti wa Kamati inayoshughulikia mauzo ya nje na maendelo ya kiviwanda nchini Uganda (PACEID).
- Kimataifa