Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Kimataifa

Dunia: Hapa na Pale — Toleo 178

Habari fupi kutoka pembe mbalimbali za dunia.

Jumatatu, 17 Agosti 2026 · 04:15Dakika 2 kusomaToleo 178, uk. 4
Midoli ya AI tishio jipya
Midoli ya AI tishio jipya — Picha na BBC

Mpango wa Iran kumuua Trump

MAMLAKA za Marekani, zimesema zimepokea onyo la tahadhari kutoka kwa vyombo vya Israel, kuwa Iran inasuka mpango wa kumuua rais wao, Donald Trump.

Mpango unaodaiwa kusukwa ili kumuua Trump umeelezwa kutumia mdunguaji aliyefuzu au kwa kutumia mshambuliaji maalumu aliyefunzwa kutumia kisu kwenye mkusanyiko wa watu wengi.

Imeelezwa kuwa mpango huo umekuwa ukiandaliwa kwa muda mrefu, tangu kumalizika kwa mashambulizi ya siku 12 ya Marekani na Israel kwa Iran mwaka 2025.

Imeelezwa mpango huo ulikuwa ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa Iran kulipiza kisasi cha kuuawa kwa aliyekuwa kamanda mkuu wa kijeshi wa Iran, Qassem Soleiman mwaka 2020.

Nyangumi asaka penzi Tanzania

WATAALAMU wa viumbe wa bahari, wameeleza kushangazwa kwao na nyangumi mwenye nundu aliyerekodiwa kutoka Colombia kwa ajili ya kutafuta majike Tanzania, ikiwa ni uhamiaji mkubwa na wa kipekee kuwahi kurekodiwa.

Wanazuoni wanaofuatilia viumbe ndani ya maji wameeleza kuwa huenda safari ya nyangumi huyo imechochewa na mabadiliko ya tabia nchi, yanayosababisha kupungua kwa hifadhi za chakula au pengine ni safari ya kutafuta wenza.

Imebainika kuwa nyangumi huyo alionekana katika Bahari ya Pasifiki karibu na Colombia mwaka 2017, kisha kuzuka tena miaka kadhaa baadaye kisiwani Zanzibar katika Bahari Hindi — umbali wa kilomita 13,000.

Ekaterina Kalashnikova anayesimamia programu ya mamalia wa baharini Tanzania amesema kwamba tukio hili ni ‘’la kushangaza na la kipekee hata kwa aina hii ya wanyama wanaohama sana.

Midoli ya AI tishio jipya

TAHARUKI imeikumba Ujerumani, baada ya kuibuka kwa taarifa kuwa watu wataweza kuagiza midoli yenye akili bandia (AI) ambayo itawekwa kufanya kazi kwenye madanguro.

Midoli hiyo itachukua nafasi ya wanawake ambao wamekuwa wakifanya kazi hiyo katika maeneo ya starehe na anasa.

Wateja wataweza kukutana na kuzungumza na midoli hiyo na”kumaliza haja zao,” hatua inayoibua mjadala mkubwa kwa watu wa Ujerumani na duniani kote.

Ripoti ya Kampuni ya Teknolojia ya SplitMetrics imebaini kuwa programu za akili bandia zimepakuliwa mara milioni 225 kwenye mtandao wa Google Play na kwamba wanaopakua, wamo wanaofanya kazi ya kuunda midoli na kuiwekea akili bandia.

Kenya na mkakati wa nyuklia

KENYA inajiandaa kuanza kuzalisha nishati kwa kutumia nyuklia huku kiwanda chake cha kwanza kikipangwa kuzinduliwa rasmi Machi mwaka ujao, 2027.

Kwa mara ya kwanza, mkakati huo uliwekwa hadharani na Rais William Ruto aliyetangaza kuhusu mpango huo wa nyuklia katika kongamano la kimataifa kuhusu nishati ya nyuklia lililoandaliwa jijini Nairobi, Machi 25, 2026.

Tayari maandalizi yameshika kasi, kwa ajili ya mradi huo unaokadiriwa kugharimu takriban Shilingi bilioni 500 za Kenya (karibu Shilingi trilioni tisa za Tanzania) na utazinduliwa katika Kijiji cha Lenya, Kaunti ya Siaya.

  • Kimataifa

Soma Pia