Kimataifa
Dunia: Hapa na Pale — Toleo 179
Habari fupi kutoka pembe mbalimbali za dunia.
Dhamira pete ya uchumba
MICHERRE Fox (31) amedhihirisha msemo huu; “penye nia, pana njia,” baada ya kunuia kupata pete ya kushika uchumba, bila kununua kwa sonara.
Mmarekani huyo alinuia kupata pete ya almasi kwa kuisaka mwenyewe ardhini na siyo kununua dukani ili kumvisha mchumba wake Trevor Ballou.
Alijitosha kwenye machimbo ya Murfreesboro, eneo la Arkansas, na kuanza kusaka ndoto yake, na ndani ya wiki tatu, akaibua almasi yenye uzito wa karati 2.3.
Furaha yake haikuwa kifani na alishukuru nafsi yake kwa kupigania ndoto yake na hatimaye kufanikisha matamanio yake.
Sayansi ya vita balaa
USALAMA wa binadamu unaendelea kuwa shakani baada ya wataalamu wa vita kuendelea kujipanga kutengeneza silaha kali zaidi.
Mabadiliko zaidi yanaendelea ya kutengeneza silaha za nyuklia, vilipuzi, silaha nzito, makombora ya masafa marefu, na ndege za kasi kwa kutumia teknolojia ya silaha zisizoonekana, kupitia akili unde, umeme, na anga ya juu hivyo kupunguza nguvu ya matumizi ya risasi. Wataalamu wameelekeza nguvu zao katika silaha za miale, mawimbi ya umeme, akili unde, silaha za sauti, bunduki za kielektroniki zinazotumia makombora ya chuma, miale ya joto, mashambulizi yanayotumia satelaiti, ndege zisizo na rubani na silaha za akili na neva.
Rais Biya arejea Ikulu
RAIS wa Cameroon, Paul Biya (93) amerejea nchini humo baada ya kukaa nje ya nchi kwa zaidi ya miezi miwili, hali iliyozua maswali kuhusu afya yake na mustakabali wa ombwe la uongozi.
Biya aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Yaoundé kutoka Geneva, Uswisi mwishoni mwa wiki, baada ya kukaa nje ya nchi kwa zaidi ya wiki 10.
Kiongozi huyo, anayetajwa kuwa rais mwenye umri mkubwa zaidi duniani, aliondoka Cameroon Juni 7 kwa kile ofisi yake ilichokiita “mapumziko mafupi ya binafsi barani Ulaya.”
Hofu vurugu za uchaguzi
WANANCHI wa Kenya wameanza kuonyesha hofu yao kuwa huenda kukaibuka vurugu za uchaguzi wakati wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Agosti, 2027.
Hofu hiyo inazidi kuongezeka kutokana na vurugu zilizoibuka kwenye maeneo ya Homa Bay kabla ya mkutano wa upinzani wiki iliyopita, ambapo baadhi ya watu waliokuwa wamebeba marungu na mapanga walifunga barabara, kuchoma matairi, kushambulia wapita njia na kupora mali.
Tayari Wakfu wa Kofi Annan unaonya kuwa Kenya ina uwezekano mkubwa wa kushuhudia vurugu za uchaguzi mwaka 2027, ikikadiriwa kuwa Kenya ina uwezekano wa asilimia 84.1 wa kushuhudia aina fulani ya vurugu za uchaguzi japokuwa siyo lazima zitokee.
- Kimataifa