Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Kimataifa

Dunia: Hapa na Pale

Habari fupi kutoka pembe mbalimbali za dunia.

Jumatatu, 10 Agosti 2026 · 03:15Dakika 2 kusomaToleo 177, uk. 4

“Jesus I Love You” yamponza

DEREVA mmoja nchini Uingereza, Simeon Chandra, amejikuta matatani baada ya kampuni ya bima kumtaka afute neno “Jesus I Love You” kwenye gari yake, kwa maelezo kwamba haitaendelea kumhudumia iwapo hatafuta neno hilo.

Kampuni hiyo ya bima ya GoSkippy, ilieleza kuwa dereva huyo amekiuka mkataba wao, kwa kuwa wakati akilisajili gari hilo neno hilo halikuwepo, hivyo haitomtambua kutokana na maboresho hayo aliyoyafanya baadaye, kwa kuweka neno hilo ubavuni mwa gari.

Dereva huyo hakuwa na namna zaidi ya kukubaliana na maelekezo ya mteja wake, ili aweze kuendelea kupata haki yake ya bima, wakati mwenyewe akiendelea kuwasiliana na wanasheria wake hasa kuhusu uhuru na haki yake ya kueleza imani yake hadharani.

Meta yaingia matatani

KAMPUNI ya Meta inayoendesha mitandao ya kijamii ya Facebook na Instagram, imeingia matatani baada ya jaji wa Marekani katika Jimbo la New Mexico kuiamuru kulipa dola milioni 567 (pauni milioni 421).

Hukumu hiyo ni baada ya kushindwa kuionya jamii kuhusu hatari ambazo majukwaa yake yanawahusu watoto, ikiwa ni hukumu kubwa zaidi dhidi ya kampuni hiyo kuhusiana na usalama wa watoto mtandaoni.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa mwishoni mwa wiki, Jaji Bryan Biedscheid alisema kuwa kampuni ni “kero kwa umma” inayofanana na uchafuzi wa hewa, na kwamba lazima iweke fedha hizo kwenye mfuko unaolenga kupunguza madhara ya baadaye.

Hukumu hiyo inaongezeka juu ya faini ya dola milioni 375 ambayo Meta ilikuwa tayari imeamriwa kulipa katika kesi hiyo, na kufanya jumla ya malipo kuwa dola milioni 942.

Kunguru wazua hofu Kenya

KUNDI la kunguru weusi wanaojulikana kwa kuharibu mazingira na kuangamiza ndege wa asili, limezua hofu baada ya kuonekana kwa mara ya kwanza jijini Nairobi.

Hii imewalazimu wataalamu wa uhifadhi wa mazingira kuingia kazini kutafuta chanzo cha ujio wao.

Ndege hao wavamizi ambao asili yao ni India, walionekana awali katika Soko la Burma na taarifa kuwafikia wataalamu wa uhifadhi, ambao walifika na kuthibitisha hofu hiyo bada ya kueleza kuwa ni ndege wanaotoka Mombasa, zaidi ya kilomita 400 kutoka pwani ya jiji hilo.

Kuzaliwa siyo kigezo cha “Umarekani”

HAKI ya kuzaliwa Marekani sasa haitamhakikishia mtoto kupata uraia moja kwa moja wa taifa hilo kubwa kiuchumi na kijeshi duniani.

Hii ni baada ya Rais Donald Trump kutia saini amri mbili mpya, zinazolenga kupunguza haki ya uraia wa kuzaliwa nchini humo.

Hatua hiyo inakuja wiki chache baada ya Mahakama Kuu kukataa jaribio lake la awali la kufuta haki hiyo, amri inayopanua orodha ya raia wa kigeni ambao watoto wao wanaozaliwa Marekani, kuwa hawatapata uraia wa moja kwa moja wa Marekani.

Amri ya pili inapiga marufuku kile kinachoitwa “utalii wa kujifungua” ambapo wanawake wajawazito husafiri kwenda Marekani kujifungua ili watoto wao wapate uraia wa Marekani kwa kuzaliwa. Trump amesema’ “Hatua hii ilipaswa kuchukuliwa miaka mingi iliyopita.”

  • Kimataifa
  • Habari fupi

Soma Pia