Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Kimataifa

Dunia: Hapa na Pale

Uvumi wa wizi wa sehemu za siri wachochea mauaji ya zaidi ya watu 80 barani Afrika, mwanamke Marekani ashinda kamari kwa namba zilezile, mgomo wa wauguzi wagharimu maisha ya wajawazito Kenya, na mtafiti wa Ani aliyejiuzulu Anthropic aonya juu ya hatari ya teknolojia hiyo.

Jumatatu, 14 Septemba 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 182, uk. 4

Tanuru la vifo vya wajawazito.

WAJAWAZITO hawako salama nchini Kenya.

Tayari wajawazito 22 wameripotiwa kufariki dunia kutokana na matatizo yanayohusiana na uzazi ndani ya wiki moja, huku mgomo wa wauguzi ukiendelea nchini humo.

Pamoja nao, watoto wachanga 44 wameripotiwa kupoteza maisha pamoja na watoto 130 waliofariki kabla au wakati wa kuzaliwa, hivyo kufichua janga jipya la kiafya linaloikumba Kenya.

Wahudumu wa afya katika hospitali za umma, wamekuwa kwenye mgomo baridi wa kazi ulioanza Julai 29, 2026, na huenda hali ikawa mbaya zaidi iwapo madaktari nao watatekeleza tishio lao la kugoma.

Chanzo ni mzozo kuhusu utekelezaji wa Mkataba wa Pamoja wa Kazi wa mwaka 2017, marupurupu na ajira za kudumu kwa wahudumu wa Mpango wa Afya kwa Wote.

Wizi bandia wa ‘nyeti’ hatari.

IMEBAINIKA kuwa madai ya uongo kuhusu wizi wa sehemu za siri yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 80 kati ya Oktoba 2025 hadi Julai 2026.

Imeelezwa kuwa takwimu za polisi kutoka nchi sita za Afrika, zinaonyesha mauaji hayo yamechochewa na uvumi unaodai kuwa kuguswa tu na mtu asiyejulikana kunaweza kusababisha sehemu za siri za mwanaume kusinyaa au kutoweka.

Taarifa hizo potofu zimeenea kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii, zikisababisha hofu, vurugu na mashambulizi ya umati, kutokana na watu kujitokeza na kupiga kelele kwamba wameibiwa sehemu za siri, hivyo kusukuma mashambulizi ya umati na kusababisha vifo.

‘AI yahatarisha maisha ya watu’.

TEKNOLOJIA ya akili mnemba (AI) inazidi kuzua mambo, huku mtafiti maarufu katika eneo hilo, Jacob Coxon akiibuka na kushutumu kampuni za Marekani kwa “kucheza na maisha ya watu.” Anasema sasa mifumo ya kompyuta inayoundwa inatishia uwezo wa binadamu.

Coxon amekuwa mtafiti katika kampuni ya AI ya Anthropic nchini Marekani, lakini sasa amejiuzulu, baada ya kuchapisha onyo kali kupitia mtandao wa X siku ya Jumanne wiki iliyopita, akisema kwa siku za usoni AI siyo tu itakuwa na uwezo wa kudukua kila kitu, bali pia itaweza “kuwa na mamlaka halisi kila mahali.”

Mtafiti huyo ameeleza kuwa watengenezaji wa AI wanaunda mifumo ya kompyuta itakayokuwa na uwezo unaozidi ule wa binadamu, akisisitiza kuwa itafika wakati wa kutishia uhai wa watu kwani hawatawweza kudhibiti.

Mcheza kamari aduwaa!

MWANAMKE mmoja kutoka Maryland, Marekani, amekutana na muujiza baada ya kushinda mfululizo michezo ya kamari ya bahati nasibu, akitumia seti namba za aina moja kwa miaka 20.

Mwanamke huyo amesema amekuwa akitumia seti ileile ya namba katika kamari hiyo, akiwa amenunua tiketi tatu zenye namba hizohizo katika droo moja ya mechi tano za nyongeza na kujishindia jumla ya dola 150,000.

Mkazi huyo wa White Plains, aliwaambia maofisa wasimamizi wa kamari huko Maryland kwamba amekuwa akicheza kwa kutumia namba hizohizo tano za ‘bonas’ kwa kipindi cha miaka 20.

  • Kimataifa

Soma Pia