Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Kimataifa

Dunia: Hapa na Pale

Mwalimu China aokoa mtoto aliyening'inia ghorof ya sita, jasusi wa Iran anyongwa kwa kufanyia kazi ujasusi Israel, wazazi Kenya wamsamehe muuaji wa binti yao, na Trump avipiga marufuku vyombo vya habari kama CNN Ikulu.

Jumatatu, 21 Septemba 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 183, uk. 4

‘Muuaji wetu asamehewe’.

WAZAZI wa mwanafunzi wa chuo cha Rongo aliyeuawa, Sharon Otieno, wameomba Mahakama Kuu imsamehe aliyekuwa Gavana wa Migori, Okoth Obado na kumpa adhabu isiyohusisha kifungo gerezani, kwa kuwa aliwapa msaada wa kifedha.

Douglas Zacharia Otieno na Melida Auma waliwasilisha ombi hilo mbele ya Jaji Cecilia Githua wakati wa hatua ya kumpa Obado adhabu baada ya kupatikana na hatia ya kumuua binti yao wakiiomba mahakama izingatie mazingira yote ya kesi hiyo.

Walisema licha ya maumivu yaliyosababishwa na kifo cha Sharon, wamechagua kumsamehe Obado na wanataka mahakama izingatie msamaha wao kwa kuwa alijitokeza baadaye na kuwapa msaada wa kifedha.

Mwalimu ajizolea umaarufu.

MWALIMU katika shule moja mjini Huai’an, China, Hou Jinxi ameonyesha ujasiri wa pekee kwenye mitandao ya kijamii baada ya video kusambaa ikimuonyesha akihatarisha maisha yake kwa kumuokoa mvulana aliyeanguka kutoka kwenye ghorofa ya sita.

Mvulana mwenye umri wa miaka 12 kutoka Huai’an alikuwa ameachwa peke yake katika nyumba hiyo na kwenda kwenye ghorofa kuchukua baadhi ya shuka zilizokuwa zimeanikwa, lakini aliteleza na kuning’inia kichwa kutoka kwenye kifaa cha kutundikia nguo.

Hou alionekana kwenye ghorofa, ambapo mara moja alikimbia hadi eneo hilo, kushika fremu ya dirisha kwa mkono mmoja na kuutoa mwili wake nje ya dirisha ili kumshikilia mvulana huyo kwa karibu dakika 20, hadi askari wazima moto walipofika.

RAIS wa Marekani, Donald Trump ameingia kwenye malumbano na chombo cha habari nchini humo, CNN kwa kukipiga marufuku kuripoti kutoka Ikulu.

Pamoja na CNN, Trump amevipiga marufuku pia vyombo vingine vikubwa, ikiwemo MSNBC na Politico akisema hazitaruhusiwa kuingia White House, huku akitumia mtandao wake wa Truth Social kutoa agizo hilo.

Tangu aliporeja madarakani awamu yake ya pili, Trump amepanua wigo wa vyombo vinavyopata fursa ya kuripoti kutoka White House kwa kuwakaribisha wanablogu wenye misimamo ya kihafidhina, watu wenye ushawishi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.

CNN imekosoa vikali tangazo hilo, ikilitaja kuwa “shambulio lisilo halali” dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Marekani. Hatua hiyo pia inatarajiwa kukabiliwa na changamoto za kisheria.

Jasusi wa Israel kunyongwa.

JASUSI ambaye ni raia wa Iran, Hossein Pedaran amenyongwa ikiwa ni utekelezaji wa hukumu ya kifo baada ya kushtakiwa na kuhukumiwa kwa kupatikana na hatia ya kuifanyia kazi ya ujasusi Israel.

Shirika la Habari la Mizan, linaeleza kuwa Pedaran alishtakiwa kwa kuipatia Mossad, Shirika la Ujasusi la Israel, taarifa kuhusu maeneo nyeti ya kijeshi katika Mkoa wa Isfahan.

Mizan ilisema ushahidi uliowasilishwa dhidi yake ulijumuisha vifaa vilivyokamatwa pamoja naye na maelezo ya kukiri makosa.

  • Kimataifa

Soma Pia