Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Tafakuri ya Bagonza

Enyi CCM tujifunze kuweka akiba ya maneno

SIKU chache kabla na baada ya vikao vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) huko Zanzibar – Julai 28-29, 2026), wana CCM tumekuwa na maneno yanayovuka heshima kubwa tuliyo nayo kuliongoza taifa.

Jumatatu, 10 Agosti 2026 · 05:15Dakika 2 kusomaToleo 177, uk. 10

Naomba niwakumbushe kwamba ni hatari kujifanya kuhisi kuzorota kwa uhusiano kati ya rais, makamu, Rais wa Zanzibar na waziri mkuu. Hata inapotokea kuhisi; tusiwe wepesi kushtaki au kuleta hoja ya kujua zaidi ya wao wanavyojuana. Ukijiweka mbele halafu wao wakapatana? Utaomba hifadhi Malawi?

Yanayozungumzwa sasa kuhusu makamu wa rais hayawezi kuwa yametokana na inayoitwa hotuba kwa wanaharakati. Siyo mwanzo na siyo kilele.

Katika mihemko ya mjadala unaogusa hizo nguzo nne, usitumie neno ambalo utakosa pa kuweka uso wako baada ya kinachoitwa mgogoro kuisha.

Urais na umakamu havitenganishwi kihivyo.

Ukimkashifu makamu, na rais amekashifiwa na kinyume chake. Msividhalilishe hivyo viti viwili katika kimoja kwa namna ambayo itavifanya visitamike tena. Kuna maisha baada ya mjadala huu.

Mfumo wa mgombea mwenza ulikuja baada ya mjadala mkali ulioongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere katikati ya changamoto kali za Muungano. Chokochoko za sasa ndani ya chama zirudi nyuma na kujielimisha hekima iliyotumika.

Maswali niliyouliza kuhusu hotuba ya Katiba mpya yamejibiwa. Wanaozuia Katiba mpya ni makundi mawili; kwanza, ni wana CCM wanaomchukia mwana CCM anayewapa watu matumaini ya Katiba mpya. Pili, ni wapinzani wanaokimbilia Katiba mpya kabla ya maridhiano ya KWELI. Upo kundi gani?

Rais na makamu ni mali ya Watanzania wote. Wakiishaapishwa siyo mali ya CCM pekee. CCM tusile na kipofu tukamgusa mkono.

Makamu wa rais ni mwanasiasa. Ni sauti ya rais na mwakilishi wake ndani na nje. Ni msaidizi wa rais, siyo msaidiwa wa rais. Ni rais tu, mwenye haki isiyohojiwa, kutilia shaka anavyosaidiwa. Wengine tupunguze viherehere vyetu vinavyokuza tatizo.

Kwao wote wawili, watambue kuwa wanaongoza nchi iliyojeruhiwa. Nchi inahitaji kutunzwa kuliko nchi kuwatunza wao. Siasa iko mikononi mwa vyombo na wana harakati. Propoganda zinajenga wapinzani na mabeberu kuliko zinavyowabomoa. Mungu awape ujasiri wa kukubali ukweli kuwa kuna kitu hakiko sawa.

Agenda ya Gen Z isiishie kuiundia wizara.

Vijana ni agenda ngumu na tete. Tumewaona Amecea wakijadili. Mashirika yote ya dunia yameweka mikakati kwa vijana. Tushtuke tunapomuondoa “Millenial” na kumleta “Baby Boomer.” Kwa Gen Z tuache itikadi wala mikopo. Tunawatumia, hatuwasililizi. Tutaumia!

Mwandishi wa safu hii ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe. Ni mchangiaji maalum wa safu na makala ndani ya Pambazuko.

  • CCM
  • Siasa
  • Katiba Mpya

Soma Pia