Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Jicho la Tai

Naogopa Mungu, teknolojia na sasa CCM

NINA hofu tatu kubwa katika maisha. Namwogopa Mungu. Naiogopa teknolojia. Na sasa, nakihofia Chama Cha Mapinduzi—CCM.

Jumatatu, 31 Agosti 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 180, uk. 5
Jicho la Tai
Jicho la Tai — Kutoka Maktaba ya Pambazuko

Lakini hofu hizi hazifanani, Mungu namwogopa kwa uchaji. Namwabudu. Nampa heshima yake. Najua anaona ninapotenda mema na ninapojifanya mwema kwa sababu kamera ipo karibu.

Mungu hahitaji taarifa ya Kamati Kuu. Hajadiliani na wajumbe. Hukumu yake haina kikao cha dharura wala taarifa kwa vyombo vya habari.

Teknolojia nayo naiogopa. Hii ni “kiumbe” kisicholala. Unazima simu, minara inakumbuka ulipokuwa. Unakana sauti yako, wataalamu wanaipima. Unaficha picha, mtu tayari amepiga “screenshot.” Teknolojia haina huruma kwa siri iliyolelewa kwa miaka. Huivua nguo hadharani, kisha inaiwekea tarehe, saa na mahali.

Zamani mtu angeweza kusema, “Sikuwahi kutamka hivyo.” Leo video inamjibu kabla hajamaliza sentensi, hata kama anaweza kudai imenakiliwa vibaya. Simu ndogo inakuwa shahidi mkubwa. Hakuna kiapo. Hakuna hongo. Inakumbuka tu.

Sasa nimeongeza CCM kwenye orodha.

CCM ni chama kikongwe. Kimejengwa na watu. Kimebeba watu. Kimewalea, kimewapandisha na kuwapa majina makubwa, lakini usidanganyike. Chama kinaweza kumgeukia hata fundi aliyesaidia kujenga ukuta wake. Leo unaweka tofali. Kesho ukuta unakuzibia mlango.

Ukikizengua, kinakuzengua mara mia. Wewe una hoja moja; chenyewe kina kamati saba. Una barua; kina katiba, kanuni, taratibu na msemaji mwenye uso usiosoma huruma. Unasema unaondoka mwenyewe. Chama kinakuwahi kutangaza kwamba kimekuondoa. Unataka kuaga kwa heshima. Kinaongeza muhuri wa nidhamu kwenye koti lako.

Hatari sana chama hiki, yaani kinaweza kukupa gari, walinzi na jukwaa, halafu siku moja kikakuachia kiti. Waliokuwa wakikuita “mheshimiwa” huanza kuuliza kama kweli walikuwa wanakufahamu.

Picha zako zinaondolewa ukutani kwa kasi ambayo hata teknolojia yenyewe inaweza kuionea wivu. Jana ulikuwa historia. Leo umekuwa tahadhari hai.

Ndani yake, cheo kinaweza kuwa mwavuli wakati wa jua na radi wakati wa mvua, leo wanakupiga kofi. Kesho kofi inakuwa kura ya kauli moja ya kukutoa.

Waliokuita “jembe la chama” wanaweza kugundua ghafla kwamba jembe hilo limepinda. Hakuna anayekumbuka mashamba uliyolima. Wote wanakumbuka ulipokataa kuchimba walipotaka.

CCM ina kumbukumbu ndefu kuliko simu. Ina masikio mengi kuliko teknolojia. Ina macho yanayoweza kuona mkutano ambao hukuitisha na kusikia maneno ambayo hukuyasema hadharani.

Ukikaa kimya, wanatafsiri ukimya. Ukizungumza, wanapima sauti. Ukicheka, wanauliza ulicheka na nani. Ukikosa kucheka, wanafungua faili.

Ndiyo maana naiogopa, lakini hofu yangu siyo ibada. Mungu pekee ndiye anayestahili kuabudiwa. Teknolojia inapaswa kueleweka na kutumiwa kwa busara.

Chama kinapaswa kuheshimiwa, kuhojiwa na kukumbushwa kwamba nacho kimeundwa na binadamu. Hakipaswi kuwa miungu ya kisiasa.

Tatizo huanza chama kinapotaka utii kuliko ukweli. Mwanachama anapolazimika kuchagua kati ya dhamiri na kadi, taifa hupoteza. Chama kinakuwa salama, lakini siasa zinakuwa wagonjwa.

CCM naiogopa nikitazama historia yake. Mungu husamehe anayeomba. Teknolojia wakati mwingine husahau baada ya “update.” Lakini CCM, mhhh! Hicho kinaweza kukumbuka kosa ambalo hata wewe hukujua umetenda.

Usikizengue. Utazenguliwa kwa kauli moja.

  • CCM
  • Teknolojia
  • Siasa

Soma Pia