Habari
Jaji Mshibe asisitiza maandalizi kukabili athari za El Niño
MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Jaji Mshibe Ali Bakari, amezitaka sekta zote nchini kutumia ipasavyo taarifa za mamlaka hiyo kufanya maandalizi ya kisekta ya kukabili athari zinazoweza kusababishwa na uwepo wa El Niño.

Jaji Mshibe aliyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa 25 wa kujadili Utabiri wa Msimu wa Mvua za Vuli, Oktoba hadi Desemba 2026, uliofanyika mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa Mikutano wa PSSSF, Dodoma.
“Tunapojiandaa kupokea taarifa ya utabiri wa mvua za vuli, Oktoba hadi Desemba 2026, ni muhimu kila mmoja wetu kufuatilia kwa karibu na kuelewa taarifa hizo ili kuanza maandalizi ya hatua za kuchukua kukabiliana na athari za hali ya hewa zinazotarajiwa kujitokeza katika sekta yake, kwa kutambua kuwa upo uwezekano mkubwa kwa El Niño kuendelea kuimarika kuelekea mwishoni mwa mwaka 2026,” alisema Jaji Mshibe.
Alisema Tanzania, kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani, inaendelea kukabili athari za mabadiliko ya hali ya hewa yanayodhihirishwa kupitia ongezeko la joto, ukame, upepo mkali, vimbunga na vipindi vya mvua kubwa vinavyoweza kusababisha mafuriko.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt.
Ladislaus Chang’a, alisema TMA imeendelea kuboresha utoaji wa taarifa za hali ya hewa, ikiwemo kuandaa utabiri mahsusi kwa maeneo madogo kwa wilaya 86 zilizopo katika mikoa inayopata mvua za vuli.
Aidha, Dkt. Chang’a alisisitiza kuwa taarifa za utabiri na tahadhari zinapaswa kuzingatiwa katika sekta zote za kiuchumi na kijamii, kwa lengo la kuongeza tija na kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa itakayotokana na uwepo wa El Niño nchini.
“Nitumie fursa hii kuwajulisha kuwa mwaka huu 2026 tunakabiliwa na changamoto ya El Niño ambayo inatarajiwa kuendelea kuimarika kuelekea mwishoni mwa mwaka na hivyo kuchagiza mvua za vuli, hivyo basi matumizi sahihi na kwa wakati ya taarifa za hali ya hewa ni muhimu kwa Kila sekta katika kukabiliana na changamoto hii,” alisema Dkt.Chang’a.
Naye, mwakilishi wa wadau mbalimbali kutoka Zanzibar, Makame Makame, akiwa Mkurugenzi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, alisema utabiri wa hali ya hewa ni jambo muhimu zaidi hasa katika kipindi cha El Niño ambapo jamii na sekta zote muhimu zinahitaji kujikinga, kujiandaa, kukabiliana na majanga au maafa yanayoweza kutokea sambamba na kurejesha hali baada ya maafa.
Mkutano huo uliobeba kaulimbiu; “Kupunguza Pengo la Uelewa wa Tahadhari za Hali ya Hewa kwa Pamoja.” Ulihusisha pia utoaji wa mrejesho kutoka kwa wadau kuhusu utabiri wa msimu wa mvua za Masika uliokuwa na usahihi wa asilimia 94.1”
Jaji Mshibe asisitiza maandalizi kukabili athari za El Niño Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Jaji Mshibe Ali Bakari.
- TMA
- El Nino
- Tabianchi
- Mvua