Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

Uganda yaweka karantini siku 21 kudhibiti Ebola

Hakika ugonjwa wa Ebola unatisha, sasa ili kuudhibiti usisambae nchini Uganda, Serikali ya Rais Yoweri Museveni imeweka karantini ya siku 21 kwa wageni wanaoingia ama kupita wakitokea DRC. Soma zaidi.

Jumatatu, 26 Oktoba 2026 · 06:07Dakika 1 kusoma
Rais Museveni
Rais Museveni — Picha kutoka Maktaba ya Pambazuko

SERIKALI ya Uganda imetangaza hatua kali za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Ebola, ikiwataka raia wake wote wanaorejea kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kukaa karantini kwa siku 21, huku wakijigharamia wenyewe huduma hiyo.

Uamuzi huo umetangazwa jana - Jumapili, Oktoba 25, 2026, na Waziri wa Afya wa Uganda, Dkt. Chris Baryomunsi, kufuatia kuendelea kwa mlipuko wa Ebola nchini DRC na kubainika kwa visa vya maambukizi nchini Kenya na Nigeria.

Baryomunsi amesema raia wa DRC wanaosafiri kwenda Uganda kwa shughuli zisizo za lazima watarejeshwa nchini kwao, huku wasafiri wanaotoka DRC wakizuiwa kuitumia Uganda kama njia ya kupitia kwenda mataifa mengine.

Aidha, mamlaka zimeimarisha ukaguzi wa afya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe na vituo vyote vya mipakani, ili kubaini watu wanaoweza kuwa na maambukizi.

Wasafiri wote wanaoingia Uganda watalazimika kujaza fomu maalumu zinazowezesha mamlaka za afya kufuatilia mienendo yao.

Hatua hizo zimechukuliwa licha ya Uganda kutangaza kumalizika kwa mlipuko wake wa Ebola Julai 28, 2026.

Waziri Baryomunsi amesema watu 60 waliokuwa wamekutana na mgonjwa wa Ebola aliyesafiri kwenda Kenya, wamekamilisha siku 21 za ufuatiliaji bila kuonyesha dalili za ugonjwa huo.

Ugonjwa wa Ebola huambukizwa kupitia mgusano wa moja kwa moja na damu au majimaji mengine ya mwili wa mtu mwenye maambukizi.

Muda wa siku 21 unatokana na kipindi cha juu kinachojulikana cha virusi hivyo kuanza kuonyesha dalili baada ya mtu kuambukizwa.

Uganda imesisitiza kuwa hatua hizo ni za tahadhari, zinazolenga kuzuia mlipuko mwingine unaoweza kuhatarisha maisha ya wananchi na shughuli za kiuchumi.

Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.

  • Ebola
  • Uganda
  • DRC
  • Museveni

Soma Pia