Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Makala

Stadi za maisha zinavyochochea ustawi wa Watanzania

WATENDE Ramadhani Botea, miaka 44, malezi bora hayatoshi kwa chakula, mavazi na elimu. Mtoto anahitaji pia uwezo wa kufikiri, kujiamini, kuwasiliana na kutatua changamoto za kila siku.

Jumatatu, 17 Agosti 2026 · 17:15Dakika 4 kusomaToleo 178, uk. 32 & 33

Watende, mkazi wa Makulunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Migiro wilayani Bagamoyo, Pwani, anasema mafunzo yanayotolewa na Uwezo Tanzania yamebadili mtazamo na mbinu zake za malezi.

Kabla ya hapo, hakuelewa maana ya stadi za maisha wala nafasi yake katika ukuaji wa mtoto. Kupitia Mradi wa Stadi za Maisha na Maadili Afrika Mashariki (ALiVE), alitambua kuwa ni mahiri wezeshi za kukabiliana na mazingira na changamoto za kila siku.

Mafunzo yalimjengea uelewa kuhusu mawasiliano, ushirikiano, kujiamini na utatuzi wa matatizo.

Anaamini mtoto hapaswi kupewa kila jibu, bali aongozwe kulifikiria tatizo, kuchunguza chanzo na kupendekeza suluhisho.

“Nilijifunza kuwa unapokabiliwa na tatizo, hatua ya kwanza ni kulitambua vizuri. Baada ya hapo unafikiria njia mbalimbali za kulitatua na kuchagua inayofaa zaidi,” anasema.

Maarifa hayo ameyahamishia kwa watoto wake.

Badala ya kuingilia kati haraka, huwauliza wanaweza kuikabili vipi changamoto. Njia hiyo imewajengea ujasiri, kujiamini na kufanya maamuzi.

Watende aliwashirikisha wazazi wengine kupitia mikutano ya kijiji na wengi wakavutiwa. Anasema wazazi wana wajibu wa kukuza stadi hizi kwa watoto kwa sababu ndizo huweka msingi wa malezi bora.

Katika kukuza utatuzi wa matatizo, wazazi walifundishwa kuwaacha watoto wajaribu kukabili changamoto kulingana na umri wao. Mtoto akileta tatizo, mzazi amuulize: “Unafikiri unaweza kulitatua vipi?”

Kisha amsaidie kutafuta taarifa, kupendekeza njia, kuchagua mbinu na kuijaribu. Ikishindwa, atafakari sababu na njia mbadala.

Watende anaiomba Serikali na jamii kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wazazi na watoto wengi zaidi.

Bagamoyo pekee, zaidi ya wazazi vinara 40 walipata mafunzo na baadaye kuwafikia wenzao.

“Elimu ya stadi za maisha na maadili ni muhimu kwa kila mtu. Watoto wote wanapaswa kufundishwa shuleni na nyumbani,” anasisitiza.

Ripoti ya utekelezaji ya mwaka 2025 inaeleza kuwa kampeni ya wiki 10 iliendeshwa na Uwezo Tanzania, OCODE, Milele Zanzibar na SAZANI Trust. Ililenga kuimarisha ushiriki wa jamii katika kuwajengea watoto uwezo wa kutatua matatizo na kukuza udadisi, ubunifu, ustahimilivu na ujifunzaji endelevu.

Kampeni iliwahimiza wazazi kuruhusu watoto kuuliza maswali na kufikiri kwa kina. Shughuli za vitendo, sanaa na michezo zilitumika kujenga kujiamini na uwezo wa kubuni suluhisho mbadala.

Zanzibar, watu 3,144 walifikiwa moja kwa moja; wanaume 1,063 na wanawake 2,081. Walikuwamo wazazi 949, wanafunzi 1,917, walimu 193, viongozi wa dini 30 na wadau wengine. Wazazi 2,607 walifikiwa kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Bagamoyo, wazazi 1,464 walielimishwa, pamoja na wanafunzi 40 wa Shule ya Msingi Nianjema, wanafunzi 54 wa Chuo cha Baqwina, wanachama 92 wa vikundi vya akiba na waumini 239. Wanajamii zaidi ya 15,000 walifikiwa kupitia vyombo vya habari.

Matokeo yalionekana katika familia na shule.

Baadhi ya wazazi walianza kuwashirikisha watoto katika majadiliano kuhusu maamuzi ya kifamilia na kuboresha mawasiliano nyumbani. Wengine waliacha adhabu kali na kutumia mwongozo chanya, unaowapa watoto nafasi ya kuuliza maswali na kueleza mawazo yao.

Pia, wazazi waliongeza mahudhurio katika mikutano ya shule, kufuatilia maendeleo ya kitaaluma na kuwasaidia watoto kujifunza nyumbani. Kwa wanafunzi, ripoti ilibaini kuimarika kwa udadisi, fikra makini, tabia ya kusoma na kuchambua vitabu, uwezo wa kujieleza, ubunifu na utatuzi wa matatizo.

Mahudhurio shuleni yaliongezeka baada ya utoro na kuchelewa kupungua.

Mtaalamu wa saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt Daniel Marandu, anasema mtoto anapozaliwa na kukua huhitaji maarifa ya kumsaidia kukabiliana na changamoto. Maarifa hayo ndiyo stadi za maisha. Kwa maelezo yake, watoto wenye kiwango kikubwa cha stadi hizo wana nafasi nzuri zaidi ya kufanikiwa kuliko wenye kiwango kidogo.

Naye Ofisa na Mtaalamu wa Mitaala kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Mwanahamisi Jokolo, alieleza mwaka 2025 kuwa ushirikiano kati ya TET na mashirika yasiyo ya kiserikali unaweza kusaidia kukuza stadi za maisha na maadili kwa wanafunzi.

Kupitia mradi wa ALiVE, Uwezo Tanzania na washirika wake wamefanya kazi na wizara zinazohusika na elimu Tanzania Bara na Zanzibar, TET na taasisi nyingine. Ushirikiano huo umechangia kuingizwa kwa stadi za maisha katika mtaala ulioboreshwa na kuwajengea walimu uwezo wa kuzifundisha.

Umuhimu wa hatua hiyo unaungwa mkono na utafiti wa mwaka 2015 wa Jumuiya ya Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki. Ulibaini kuwa wahitimu wengi walikuwa na maarifa ya kitaaluma, lakini walikosa uwezo wa kuyatumia kazini. Waajiri walitaja ma za maisha.

pungufu katika mawasiliano, ubunifu, kujitambua, utatuzi wa matatizo na fikra tunduizi. Tanzania, wahitimu sita kati ya 10, sawa na asilimia 61, walionekana kukosa stadi hizo muhimu, hali iliyopunguza nafasi zao za kuajiriwa.

Utafiti wa ALiVE wa mwaka 2022 pia ulionyesha kuwa shule zina mchango mkubwa katika ukuaji wa stadi za maisha. Vijana wa madarasa ya juu, hasa sekondari, walionyesha umahiri mkubwa zaidi kuliko waliokuwa katika ngazi za chini za elimu.

Ushahidi huo umechangia maboresho ya elimu nchini. Mtaala ulioboreshwa, ulioanza kutumika Januari 2024, umezipa stadi za maisha nafasi katika masomo mbalimbali. Miongoni mwazo ni fikra tunduizi, utatuzi wa matatizo, mawasiliano na ushirikiano.

Lengo ni kumjenga mwanafunzi anayeweza kutumia elimu yake kukabili hali halisi za maisha, kujenga mahusiano bora, kubuni ajira, kushirikiana na jamii tofauti, kukuza uchumi na kuimarisha amani.

Simulizi la Watende linaonyesha kwamba mageuzi hayo hayawezi kubaki darasani pekee. Mzazi, mlezi, mwalimu na jamii lazima washirikiane kumjenga mtoto anayeweza kuuliza, kufikiri, kujaribu na kujifunza kutokana na makosa.

Hapo ndipo elimu inapogeuka kuwa nyenzo ya kujenga kizazi chenye maarifa, ujasiri, uwajibikaji na suluhisho endelevu.

Swali linabaki: wewe kama mzazi au mlezi unafanya nini kumsaidia mtoto wako kukuza stadi hizi muhimu za maisha? Na umejifunza nini kutokana na makala haya? Tuma maoni yako kupitia anuani ya mhariri wa gazeti hili.

  • Elimu
  • Stadi za maisha
  • ALiVE

Soma Pia