Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

Jaji Warioba atabiri magumu 2030

MAKAMU wa Kwanza wa Rais (mstaafu) wa Tanzania, Jaji Joseph Warioba ametabiri kuwa Tanzania haitafanya uchaguzi ujao kwa katiba mpya.

Jumatatu, 17 Agosti 2026 · 12:15Dakika 4 kusomaToleo 178, uk. 22 & 23
Jaji Warioba atabiri magumu 2030
Jaji Warioba atabiri magumu 2030 — Picha Kutoka Maktaba

Warioba ambaye pia aliwahi kuwa waziri mkuu amesema kwa mtiririko wa matukio unaoendelea sasa kwenye utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2029 na Uchaguzi Mkuu wa 2030, utafanyika bila Katiba mpya, hivyo kulazimika kutumia katiba iliyopo kukamilisha chaguzi hizo.

Jaji Warioba alisema utabiri huo unatokana na uzoefu wake, hasa akiangalia msongamano wa matukio na muda uliopo hasa kwa kuzingatia mapendekezo ya Tume ya Jaji Othman Chande, ambayo iwapo yatafuatwa kwa mtiririko kama ilivyoelekezwa.

“Na ikiwa hivyo, tutafika 2029 hatuna Katiba mpya na tutafanya uchaguzi huu wa 2029 na 2030 kwa kutumia Katiba hii hii na tume hii hii ya uchaguzi, na tukifika hapo tutarajie kupata matatizo huenda makubwa kuliko yaliyojitokeza 2025,” amesema.

Jaji Warioba ametoa utabiri huo wakati akizungumza katika kipindi cha Mizengwe, kinachorushwa na Kipindi cha Jenerali Ulimwengu, kuhusu mwelekeo wa utekelezaji wa baadhi ya mapendekezo ya Jaji Chande unaoendelea, hatua inayoonesha serikali imekubali mapendekezo hayo.

Akifafanua, Jaji Warioba alieleza kuwa moja kati ya mapendekezo ni kuwa na tume ya maridhiano, na kwamba ratiba hadi kufikia mwaka 2028 yawe yamekamilika yote pamoja na kuwa na Katiba mpya ili iweze kutumika kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2029 na Uchaguzi Mkuu 2030.

“Nimefuatilia ratiba ya mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande, kwanza ilikuwa kuunda tume ambayo itafanya uchunguzi wa mambo yaliyotokea nani anahusika na tume hiyo imeundwa na imeshaapishwa…”

“Mwanzoni waliteuliwa majaji wa hapa nyumbani lakini sasa wamefikia sita, baada ya kuongeza mmoja kutoka Uganda na mwingine kutoka Namibia ambao wamepewa miezi mitano kufanya uchunguzi na kama ikihitajika wataongezewa muda…”

“Ukimaliza hiyo kuna kamati ya wataalmu kuangalia na kulinganisha Katiba ya sasa, rasimu ya tume ya mabadiliko ya katiba na Katiba iliyopendekezwa na bunge, hatujui watapewa muda gani kuifanya hiyo kazi…”

“Lakini wakimaliza, kutokana na maelezo ya Jaji Chande, watakwenda kwa wananchi kuwauliza na wakifika kwa wananchi siyo suala la muda mfupi, litachukua muda ukishamaliza hilo ndiyo itafanya kuunda tume ya maridhiano,” alisema.

Alisema tume ya maridhiano ikimaliza ratiba yake ndipo utaanza mchakato wa kutafuta katiba mpya, ratiba ambayo yeye binafsi anaiona haiwezekani kuitekeleza katika muda wa miaka miwili na anaamini hata watu ndani ya serikali wakiifuata ratiba hiyo, katiba haitaweza kukamilika mwaka 2028.

“Nikianza na tume ya maridhiano, kuna mambo mengi ambayo lazima kukubaliana na moja, kama Tume ya Jaji Chande ilivyosema, hili ni suala mtambuka ambalo litahusu watu wengi, hii siyo tume ya kawaida ya rais kwamba atateua tume na kuipa hadidu za rejea…”

“Tukiangalia kama tume ya mabadiliko ya Katiba, rais alipata mawazo ambapo watu wengi walisema hawataamini tume ambayo imeteuliwa na rais bila kupata ushauri kwa sababu wanaohusika na matatizo ndio wanataka ushiriki wa watu wengi zaidi ili waweze kutoa mawazo, siyo wachache walioteuliwa,” alieleza.

Jaji huyo mstaafu alisema katika hilo wapo wanasiasa, vyama vya siasa, taasisi za kidini, taasisi za kiraia, lakini kuna makundi mengine ambayo yanataka tume ishughulikie masuala hasa ya vijana kwa sababu matatizo tuliyo nayo vijana wakisema wanaandamana unaota serikali inavyochukua hatua.

“Hii siyo rais ateue tu, kwanza apate ushauri, kama anataka wawakilishi kutoka taasisi za kidini awaulize wao wenyewe, kama ni taasisi za kiraia, wenyewe wapendekeze kwa sababu wanajua mawazo yao ni nini, ndiyo ninayosema h i y o …”

“Watakapokutana suala la kwanza ni kutengeneza hadidu rejea zao, wajue ni masuala gani watazungumza na watakayozungumza juu ya Katiba yatakuwapo nayo yatakuwa muhimu.

Pia muda wenyewe utakuwa mrefu sasa wasije wakafikiri maridhiano wataweza kuyapata kwa miezi sita…”

“Sasa hivi hatujaweka mazingira ya kuweza kusema ni akina nani watakaoshiriki na ukiona malumbano yanayotokea huna uhakika kwamba wote wanaohusika watashiriki na wakiwepo ambao hawatashiriki tutaendelea na hali kama h i y o …”

“Katika haya maridhiano ni lazima itafutwe njia vijana wawepo na raia wengine, ukichukua kwa mfano masuala yatakayozungumzwa ni pamoja na matatizo yanayowahusu wananchi nwenyewe, ambapo ukiangalia kwa sasa hawana uhuru, Watanzania wanaishi kwa woga siyo kama ilivyokuwa,” alisema.

Alisema wengi, wanaeleza kuwa wanaogopa kutekwa, kupotea, kwa hiyo hawawezi kutoa maoni kwa kuwa wanaogopa.

Warioba alieleza kuwa inafikirisha zaidi hivi sasa kubainika kuwa watu ambao – angalau wanaweza kuwa huru, wakiwamo wanafunzi wa vyuo vikuu na wahadhiri wanakamatwa na kupewa kesi za uhaini.

“Kuna wakati mimi mwenyewe, kama nilivyowahi kusema niliwahi kupigiwa simu tu kwamba zima simu yako hadi tutakapokwambia, hawakwambii kwa sababu gani wala sheria inayotumika, wakaniita kwenye mkutano nikapigiwa simu usiende,” alisema.

Utendaji wa bunge

Jaji Warioba pia aligusia utendaji wa bunge kwa sasa na kueleza kushangazwa kwake na namna linavyofanya kazi zake, akisisitiza umuhimu wa mgawanyo wa madaraka na kuitenga serikali na bunge.

“ Awali tuliwahi kupendekeza wakati ule ila ukiona sasa kwa jinsi serikali ilivyo na nguvu, wabunge wamekuwa ni machawa, kila mmoja akizungumza ni lazima amtaje rais, lakini husikii wakizungumzia watu wao, maana ya ubunge ni kama haipo. Wangekuwa ni wabunge haswa, wangekuwa wanapata mawazo yao kutoka kwa wananchi…”

“Kwa yaliyotokea mwaka jana, watu wengi wa nchi hii wamekufa, lakini hukusikia bunge likizungumzia hili, husikii sauti yake, hivi hawa wabunge huko walikotoka hakuna watu waliouawa?” Alihoji.

Alidai kuwa kwa sasa bunge halina madaraka kamili kwa sababu ya serikali, limemezwa.

  • Jaji Warioba
  • Katiba Mpya
  • Uchaguzi
  • Bunge

Soma Pia