Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

Mijadala TCD waibua mahitaji Tanzania mpya

Wadau hao kutoka asasi za kiraia, vyama vya siasa, wanataaluma, wadau wa maendeleo, taasisi za serikali, wanasheria, wasomi, vijana na makundi Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Stephen Wasira MJADALA mzito kuhusu hatma ya Tanzania baada ya matukio ya Oktoba 29, 2025, umeibua mahitaji ya wadau kuhusu namna nchi inavyoweza kujengwa upya na kuepuka madhara yatokanayo na mwenendo wa baadhi ya wanasiasa.

Jumatatu, 14 Septemba 2026 · 06:00Dakika 4 kusomaToleo 182, uk. 20

Aidha, mjadala huo umeweka msisitizo kwenye ulazima wa kutafuta namna bora ya kuiweka nchi pamoja.

Katika mjadala wa kitaifa ulioandaliwa na kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) uliomalizika wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, wadau walioshiriki walitumia fursa hiyo kushauri kuhusu yanayopaswa kufanyika kutatua changamoto zinazoikumba nchi na kuiweka Tanzania bora zaidi sasa na baadaye.

maswali kuhusu mwelekeo na mustakabali wa nchi “baada ya kupitia vipindi vigumu.”

Kwamba nini kifanyike kuhusu mwelekeo wa siasa za nchi, uhusiano baina ya vyama, dini, wanasiasa na kuangalia mustabali wa taifa, namna ya kujenga maridhiano na hatua zinazohitajika kurejesha imani miongoni mwa Watanzania kutokana na matukio ya Oktoba 29, 2025 na yaliyofuata.

Akizungumzia kuhusu mwelekeo wa taifa, waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, alieleza kuwa hadi sasa umoja na mshikamano ambao ulijengwa kwa gharama kubwa na kuwekewa misingi tangu ulipopatikana uhuru wa Tanganyika unaonekana kuvurugwa na watu wachache, hivyo kushauri kurejea katika misingi ya awali.

Alisema ni jambo la kushangaza kuona sasa hivi suala la amani linachukuliwa kuwa la kulindwa kwa mtutu wa bunduki, hasa baada ya kukiukwa kwa misingi iliyowekwa awali ya amani ya kweli iliyojengwa chini ya kufutwa kwa ubaguzi wa aina zote, ikiwemo wa kidini, kiitikadi, kikanda na kikabila, suala ambalo linaonekana kupuuzwa kwa sasa.

“Amani hailindwi kwa mtutu wa bunduki… ni lazima kurudi kwenye msingi, kuwe na usawa, kusiwe na ubaguzi wa aina yoyote…”

“Hapa amani ni jambo la msingi na lazima tukubaliane, kama kuna kitu kinakuja kutisha amani yetu lazima wote tukiache. Vyama vihakikishe vinaunganisha wananchi, tusifikiri kuwa amani italetwa kwa mgawanyiko, hapana,” alisema Jaji Warioba.

Alisisitiza kuwa Tanzania inahitaji kurejea katika misingi ya usawa, uadilifu, uwajibikaji na uzalendo, huku akizitaka taasisi na vyama vya siasa kutafuta njia za kuwaunganisha wananchi.

Alisema siku hizi viongozi wakisimama wanaita mikutano ya hadhara ya wanachama wao, wanakuwa na sare yao, wa sare za vyama vingine hawasogei pale, wakisogea ni ugomvi kwa hiyo wanasiasa wamewagawa wananchi katika siasa na katika jamii, ikiwa ndio chanzo cha matatizo ya amani ya nchi.

“Pia hivi sasa zimeanza jitihada za kuzua ukabila na sasa hivi tunazungumza hata mambo ya maadili tunasema machifu wasimamie maadili, tumeanza kuzungumza maadili ya makabila wakati tulikuwa tumeshajenga maadili ya kitaifa, tunarudisha ukabila kwa njia nyingine…”

“Hata kwenye masuala ya imani, sasa kuna mpasuko wa dini kwa sasa hivi na unaanza kutugawa na kuwagawa viongozi na pia ukanda umezidi, watu wanaanza kujitazama kwa msingi wa kanda. Utaifa umezuka, u-Zanzibari na u-Tanganyika, tunaanza kujiona sisi Wazanzibari sisi Watanganyika na tunadai haki zetu,” alisema.

Makamu wa kwanza wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman alisema baadhi ya mambo yanaendeshwa kwa mazoea na kujuana, badala ya kufuata Katiba, hali ambayo, kwa maoni yake, inaweza kuleta vurugu iwapo mtu ataamua kudai utekelezaji wa Katiba kikamilifu.

Sheikh Issa Ponda, Kiongozi wa Shura ya Maimamu, alisema kizazi cha sasa kinataka kuona Tanganyika ikiwa na nafasi yake ndani ya Muungano, akirejea hoja ya serikali tatu iliyowahi kujadiliwa na Tume ya Jaji Warioba.

Waziri wa zamani, Profesa Anna Tibaijuka, amesema utambulisho wa Tanganyika hauwezi kuondolewa kwa kuimarisha utambulisho wa Zanzibar.

Tibaijuka alisema yeye binafsi angependa kuona serikali moja, akisisitiza umuhimu wa umoja wa kitaifa.

Jaji Warioba Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wasira, kwa upande wake alihoji sera ya ACT Wazalendo ya “Zanzibar yenye mamlaka kamili”, akitaka kufafanuliwa kama mamlaka hayo yanamaanisha Zanzibar kuwa dola yenye mamlaka kamili au bado kuwa sehemu ya Muungano.

Kwa upande mwingine, kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, anayekabiliwa na mashtaka ya uhaini katika Mahakama Kuu, iliibuliwa katika mkutano huo, ambapo Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu Ado, alisema kumuachia Lissu ni miongoni mwa hatua muhimu zinazoweza kujenga mazingira ya maridhiano.

Ado alisema ni dhahiri kuna sauti kubwa inayotaka Tanzania ifikie maridhiano, lakini akaonya kuwa maridhiano ya kweli yana masharti na misingi yake na yatafanikiwa tu kwa kumuachia Lissu, kushughulikia kesi anazodai kuwa na mwelekeo wa kisiasa, kuweka ukweli, haki na uwajibikaji mbele katika kushughulikia vifo vilivyotokea baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025,”alisema.

Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, alitoa mwito kwa CCM kusimamia hatua ya kufutwa kwa kesi zenye viashiria vya kisiasa, akisema hilo linaweza kuwa sehemu ya mchakato wa uponyaji wa taifa.

Mwabukusi alionya dhidi ya kukimbilia mchakato wa Katiba Mpya bila kwanza kujenga mazingira ya maelewano, akisisitiza kuwa haoni uwezekano wa kuandika Katiba Mpya kwa utulivu ikiwa taifa bado halijaweza kukubaliana kuhusu yaliyotokea.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa), Profesa Elgidius Ichumbaki, alihoji utekelezaji wa ahadi ya CCM ya kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya ndani ya siku 100, akiuliza kwa nini wanachama wa chama hicho wanaozungumzia suala hilo wanaonekana kukumbana na matatizo.

Ichumbaki alimtaja Dkt. Emmanuel Nchimbi kama mfano wa mwanasiasa ambaye msimamo wake wa hadharani kuhusu Katiba Mpya umehusishwa na hatua zilizochukuliwa dhidi yake ndani ya CCM. Hata hivyo, Wasira alipinga hoja hiyo, akisema si kweli kwamba mwanachama anayezungumzia mambo yanayotakiwa na wananchi “anashughulikiwa” kwa sababu hiyo, akisisitiza kuwa CCM yenyewe ndiyo imeahidi Katiba Mpya.

  • TCD
  • Katiba Mpya
  • Demokrasia

Soma Pia