Habari
Kigogo Udasa ahofu Katiba Mpya, aibua Tanganyika
KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (Udasa), Dkt. Dominicus Makukula, haamini endapo Katiba Mpya itapatikana kabla ya mwaka 2030.
Akizungumza na Pambazuko katika mahojiano maalum ofisini kwake Dar es Salaaam, wiki iliyopita, Dkt. Makukula amesema wasiwasi wake unatokana na kutokuwepo kwa maandalizi yoyote ya msingi na ya wazi hadi sasa kuhusu mchakato huo.
Mwanazuoni huyo amesema mchakato wa kupata Katiba Mpya - kwa kawaida, huchukua muda mrefu, hivyo kwa muda uliosalia kufika 2030, ni mfupi. Ni chini ya miaka minne kuanzia sasa.
Aidha, katibu huyo amesema katiba Mpya ya Tanzania inapaswa kutanguliwa na Katiba ya Tanganyika kwa sababu mbia mwingine wa Muungano; Zanzibar, tayari ana katiba yake.
Akifafanua, Dkt. Makukula amesema ili Muungano uonekane kuwa wa usawa, ni vyema kila mbia kuwa na nafasi sawa. Kwamba kwa kuwa Zanzibar ina Katiba yake, basi na Tanganyika nayo inapaswa kuwa na katiba yake.
“Ili Tanganyika na Zanzibar ziweze kuungana vizuri, basi na Watanganyika lazima wadai vitu vyao vinavyowahusu ili pande mbili zitakapoungana kila moja ijue inaleta nini mezani,”
amefafanua. Ameshangaa wahusika wa kuandaa mchakato wa Katiba Mpya kuwa na kigugumizi kuanza mchakato huo mapema licha ya wadau vikiwamo vyama vya siasa kudai suala hilo na kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeahidi suala hilo ndani ya ilani yake.
“Ninashangaa wapi tunakwama, kwa sababu jambo lenyewe hilo la Katiba Mpya limeguswa tayari kwenye maeneo makubwa matatu...”
“Kwenye mashirika ya kiraia tayari huko inaonekana ndiyo kama watu walikuwa wameanza kuzungumza wao wenyewe, lakini ukifika kwenye ofisi ya serikali, yaani kwa maana ya rais, tayari rais ameshazungumzia suala hilo kwamba kutakuwa kuna mabadiliko ya katiba...”
“Lakini ukienda kwenye Ilani ya CCM, hilo limetajwa waziwazi, na hata ilani za vyama vingine vya siasa vyenyewe vilikuwa tayari vimekwishazungumzia mambo hayo...”
“Kama mnakumbuka mwaka jana, sisi tuliendesha mdahalo wa vyama vya siasa ambavyo vilikuwa vinatarajia kwenda kushiriki uchaguzi mkuu wa udiwani, wabunge na rais...”
“Na juzi kwenye kongamano la Tanzania Democracy Forum lililoandaliwa na TLS (Chama cha Wanasheria Tanganyika), walikuwepo watu mashuhuri; kina mzee Warioba, Profesa Shivji, Rose Mwakitwange, James Mbatia, Profesa Tibaijuka na wengine wengi, lakini sikuona uwakilishi wa kutosha kutoka kwenye chama tawala, nafikiri kulikuwa kuna baadhi ya wajumbe ila hawakuwa wale mashuhuri, ”amesema Dkt. Makukula.
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- Katiba Mpya
- Udasa
- Muungano
- Tanganyika