Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

Utata alipo Dkt Nchimbi

NANI anajua alipo Dkt. Emmanuel Nchimbi, Makamu wa Rais wa Tanzania aliyetangaza kujiuzulu na kuachana na siasa na utumishi wa umma?

Jumatatu, 31 Agosti 2026 · 06:00Dakika 4 kusomaToleo 180, uk. 8
Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi
Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi — Na Mpigapicha Wetu

Ni swali lililoanza kusikika miongoni mwa Watanzania kupitia mitandao ya kijamii, mazungumzo ya wazi kwenye mijadala ya wasomi, wana harakati na hata “vijiweni.”

Swali hili limegubikwa na kivuli na utata wa kiini hasa cha kujiuzulu kwa kiongozi huyo namba mbili nchini.

Dkt. Nchimbi ameshikilia wadhifa huo kwa kipindi cha chini ya miezi kumi, baada ya kuapishwa Novemba 3, 2025, akichukua nafasi ya Dkt. Philip Mpango, ambaye naye aliomba kupumzika kabla ya muda wake kwa sababu za kiafya.

Mara ya mwisho Dkt. Nchimbi kuonekana hadharani ilikuwa Agosti 22, 2026 kwenye ufunguzi wa mradi wa umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHP) wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani.

Kwenye shuguli hiyo, kiongozi huyo alifanya kazi ya kumkaribisha Rais Samia Suluhu Hassan, na licha ya kupewa dakika 10 za kuzungumza, aliamua kutumia chini ya dakika moja kumkaribisha rais ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi.

Mawasiliano mengine ya Dkt. Nchimbi na Watanzania ni Agosti 25, 2026 kupitia akaunti yake ya Instagram ambako alipitisha barua yake fupi ya kutangaza kujiuzulu kwake nafasi ya makamu wa rais na siku iliyofuata, yaani Agosti 26, 2026 Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikamfutia uanachama.

Hata hivyo, imebainika kuwa akaunti hiyo ya kijamii aliyoitumia kuujulisha umma kujiuzulu kwake ilikuwa hajaitumia tangu mwaka 2023.

Hili lilisababisha utata juu ya usahihi na uhalali wa barua hiyo ya kujiuzulu kutokana na kutokuwa hewani kwa muda mrefu.

Taarifa za kina zinaeleza kuwa mpaka sasa Dkt. Nchimbi hajulikani alipo, na hata mawasiliano yake ya simu ya kiganjani hayapatikani. Pambazuko lilijaribu kupiga simu ya mkononi ya Dkt. Nchimbi ambayo huitumia siku zote bila mafanikio.

Agosti 27, 2026 mmoja wa wasaidizi wake binafsi, alipoulizwa na Pambazuko kama amewasiliana na bosi wake, alikana kuwa msaidizi wake, lakini aliahidi kutoa namba ya msaidizi wa Dkt Nchimbi. Hata hivyo, tangu wakati huo hadi sasa hajawahi kutuma mawasiliano hayo.

Aidha, Waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, akiwa kwenye kongamano lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia (TCD), Agosti 28, 2026 alisema tangu Dkt. Nchimbi alipoandika barua ya kujiuzulu Agosti 25, 2026 amekuwa akimtafuta kwenye simu bila mafanikio.

Katika kongamano hilo, Jaji Warioba, ambaye aliongoza tume ya kukusanyua maoni ya Katiba Mpya, alisema aliwasiliana na Dkt. Nchimbi baada ya kuona taarifa ya kujiuzulu kwake mitandaoni, na alipompigia simu kumuuliza, alimthibitishia kuwa ni kweli.

“Nilipoona kwenye mtandao kuna barua ya Nchimbi, binti yangu akaja, akasema Nchimbi ameandika barua ya kujiuzulu, nikakataa...”

“Binti yangu mwingine akaja akasema ni kweli, ndipo nikampigia simu Nchimbi. Nikamuuliza kuna barua ina trend, nikamuuliza je, ni kweli umeandika barua ya ku-resign (kujiuzulu)? akasema ni kweli mzee, nikamuuliza, rais reaction yake ni nini (amepokeaje)? akasema bado... nikasema basi tutazungumza kwa urefu zaidi nijue kwa nini ume-resign...”

“Siku ya pili nikasikia halmashauri kuu inakutana, nikampigia, simu haikupokelewa... basi nikajua kwa kuwa bado ni makamu basi anaweza kuwa kwenye vikao vya Halmashauri Kuu...”

“Jioni likatoka tangazo kuwa kuna press conference ya CCM, nikampigia simu tena, lakini haikupokelewa, nikapeleka ujumbe, haukujibiwa. Kwa kawaida nikiandika alikuwa ana respond (anajibu) mapema tu...”

“Baadaye nikaona yaliyosemwa kwenye press conference, nikajaribu tena kupiga simu.. haikupokelewa...”

“Baada ya kuona tamko la Katibu Mkuu wa CCM kwamba chama kimemfukuza uanachama, nilimtafuta tena Dkt. Nchimbi lakini simu haipokelewi,” amesema Jaji Warioba.

Jaji Warioba akaongeza; “Ndiyo nikaona wanasema amenyang'anywa simu zake. Sasa mimi inanishangaza kidogo maana nilikuwa kwenye chama, tulikuwa tunachukua hatua za nidhamu kwa utulivu, sasa waliponiambia sijui yuko kizuizini, bado sijaamini kwa kuwa sioni msingi yake...”

“Moja ya matatizo tuliyo nayo, ukiangalia ahadi zetu wana CCM, moja inasema nitasema kweli daima, fitina... mwiko, ipo kwenye ahadi zetu, lakini siku hizi ukisema ukweli, unazushiwa fitina.”

Aidha, Jaji Warioba, ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania katika serikali iliyoongozwa na Mwalimu Nyerere, anasema anaona kuna tatizo linalokwamisha kupatikana Katiba Mpya licha ya CCM kuahidi suala hilo kwenye ilani yake ya uchaguzi mwaka 2025.

Anasema anaona kilichofanya CCM imwadhibu Dkt. Nchimbi ni hatua yake ya kuwaambia Watanzania wapambanie Katiba Mpya.

“Katika tuhuma ambazo amepewa ni kusema hilo, na hiyo ndiyo inanipa wasiwasi, kweli tuna utashi wa siasa, ama tunataka tuendee hivi tusahau. Tutafika mwaka 2030 bila Katiba Mpya inayotumika. Na hali ninavyoiona kunaweza kuwa na mlipuko,” ameonya Warioba.

Kauli tata za Nchimbi

Julai 24, 2026 katika mkutano mkuu wa 15 wa Mtandao wa Watetezi wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Dkt. Nchimbi aliwataka watanzania wapambane kuipata Katiba Mpya.

Kauli hii ilizua utata, huku baadhi ya watu wakihoji wananchi wapambane na nani iwapo iwapo serikali na CCM wote wanaitaka katiba hiyo mpya.

Ziara kwa wastaafu

Katika wiki za karibuni, Dkt. Emmanuel Nchimbi alikwenda kumtembelea Jaji Warioba, na siku chache baadaye alikwenda nyumbani kwa rais mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete. Hata hivyo haijulikana wazi juu ya uzito wa kile walichokizungumza.

  • Emmanuel Nchimbi
  • CCM
  • Joseph Warioba
  • Katiba Mpya

Soma Pia