Habari Kuu
Lissu aibwaga Jamhuri kosa la uhaini, ahukumiwa miaka minne jela kwa uchochezi
Hatimaye Mahakama Kuu ya Tanzania imefunga ukurasa wa kesi ya uhaini iliyokuwa ikimkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kwa kueleza halijatbibitika, lakini imemfunga miaka minne kwa kosa lililoelezwa kuwa limo ndani ya kesi kubwa.

MWENYEKITI wa Chadema, Tundu Lissu ameibwaga Jamhuri katika kesi ya uhaini iliyokuwa ikimkabili, kisha kutiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka minne jela kwa kesi ndogo ya uchochezi iliyozalishwa ndani ya kesi hiyo.
Hukumu hiyo ya kifungo cha miaka minne kwa Lissu imetolewa na Jaji wa Mhakama Kuu - Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, Dustan Ndunguru ambaye alieleza kuwa upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha uhaini aliodaiwa kuufanya Lissu kama ilivyoelezwa kwenye hati ya mashtaka, lakini mahakama imemtia kosa dogo la uchochezi lililoibuliwa kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi wa Jamhuri.
Kabla ya kutoa hukumu hiyo, Jaji Ndunguru alisema wameangalia ushahidi kuhusu kauli zilizotolewa na mshtakiwa na na kuona kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa mshtakiwa alilenga kuitishia serikali kama ilivyoelezwa katika hati ya mashtaka, hasa kwa kuzingatia tafsiri ya baadhi ya mashahidi.
“Tumeona kwamba ushahidi uliotolewa na mashtaka unashindwa kuthibitisha shitaka la uhaini hivyo katika kiini hiki cha pili tunaona ushahidi haujakidhi kuonyesha nia ya uhaini…”
“Kwa mujibu wa kifungu cha 39(2)(d) kuna vitu vitatu ikiwemo factuai issues (uhalisia), mahakama lazima iangalie ushahidi kujiridhisha na tatu ni ushahidi upi umetolewa…”
“Mahakama inaona kwamba tafsiri ya maneno ya Lissu bila tangible evidence (ushahidi thabiti) tumeongozwa na kanuni kwamba nia ni internal state of mind lazima liambatane na ushahidi wa kimazingira na vitendo vya kufanya uhaini…”
“Nia ovu siku zote inakuwa inferred kutoka kwa maneno na matendo ya mshtakiwa,” ameeleza Jaji Ndunguru.
Hata hivyo, alifafanua kuwa mahakama imeelekeza kwenye kifungu cha 319(1) na (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kinachoeleza uwezo wa mahakama kubadilisha shitaka na kutoa uamuzi kuhusu kosa dogo zaidi pale ushahidi unapothibitisha uwepo wa kosa hilo, hivyo kumtia hatiani kwa kosa la uchochezi.
Akitoa utetezi wake, Lissu alieleza kuwa amekaa gerezani kwa siku 577 kwa tuhuma za kosa la uhaini ambalo ndilo kosa kubwa kuliko yote katika Jamhuri ya Muungano, ambalo kwa mujibu wa kifungu cha 39(2)(d) adhabu yake inaweza kuwa ni kifo, na baada ya wingu jeusi kosa hilo limeshindwa kuthibitishwa na amepewa kosa la uchochezi, ambalo halikuwepo kwenye hati ya mashtaka.
“Hii maana yake ni nini waheshimiwa majaji? mmesema wenyewe hakukuwa kosa. Kwa hiyo nimekaa gerezani siku 577 bila kosa lolote. Ushahidi wangu umethibitisha kwamba hii ilikuwa kesi ya kisiasa...”
“Kwa sababu ni political persecution (mashtaka ya kisiasa) inabidi visababu vitangenezwe vya kumfunga huyu mgomvi wetu. Visababu vya kumfunga huyu mpinzani wetu. Hili kosa la uchochezi kosa ambalo ninyi waheshimiwa majaji mmelitengeneza. Mimi nilishitakiwa kwa uhaini na kusambaza taarifa za uongo. Mmetafuta kosa ambalo halikuwepo, mmenipa...”
“With all due respect (kwa heshima zote) mmefanya hivyo kwa sababu za kisiasa na kwa maelekezo ya kisiasa tu. Ni kama mmeambiwa, huyu mtu hana kosa, lakini tafuteni kosa lingine dogo, isije ikaonekana serikali imepata aibu. Mimi ninajua mtanihukumu. Na mnaonekana tayari mnayo hukumu, l feel it in my heart.”
“Uamuzi wa kunitia hatiani kwa kosa ambalo sikushtakiwa nalo na ambalo sikupata fursa ya kujitetea dhidi yake kwa lengo la kubalansisha tu (kuweka uwiano)una athari kubwa, ni kwamba mmewapa kinga wale waliohusika na mauaji kwa sababu watasema kwamba wale waliochochea wamekutwa na hatia...”
“Waheshimiwa majaji ninamalizia kwa kusemna toeni hukumu mliyo nayo, mliyoelekezwa kuitoa,” alieleza Lissu akihitimisha maelezo yake.
Lissu alifikishwa mahakamani Aprili 10, 2025 na kufunguliwa kesi ya uhaini namba 000019605 ya mwaka 2025, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam. Hukumu ya kesi hii, endapo angekutwa na kosa aliloshitakiwa nalo, ingekuwa ni kunyongwa hadi kufa.
Umebakiwa na makala 1 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- Lissu
- Uhaini
- Hukumu
- Mahakama Kuu
- Kifungo